Zungu awaahidi wajasiriamali kuwa na siku yao
Naibu Spika wa Bunge,Mussa Azan "Zungu" (wapili kulia) akipokea zawadi kutoka kwa mkuu wa mauzo na huduma kwa wateja wa kampuni ya Mr UK Electronics, Nasra Mwembe (kushoto) wakati alipotembelea banda hilo katika maonyesho ya wajasiliamali wa mkoa wa Dar es Salaam leo Septemba 13, 2023. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja baada ya uwepo wa maombi ya wajasiriamali hao kutaka uwepo wa siku za maonyesho kama ilivyo kwa wafanyabiashara (Sabasaba) na Wakulima (Nanenane).
Dar es Salaam. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu amewaahidi wajasiriamali walioshiriki maonyesho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam uwepo wa siku yao mahsusi kwa ajili ya maonyesho.
Hatua hiyo inakuja baada ya uwepo wa maombi ya wajasiriamali hao kutaka uwepo wa siku za maonyesho kama ilivyo kwa wafanyabiashara Sabasaba na Wakulima Nanenane.
Akizungumza leo Septemba 13 katika viwanja vya mnazi mmoja wakati akifunga maonyesho yaliyoratibiwa na CRDB Bank Foundation pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala amesema atawasilisha maombi hayo kwa Rais Samia Hassan huku akihakikisha kuwa atayasikia na yatapita.
"Tumelisikia ombi lenu tutalipeleka juu na niwahakikishie litapita. CRDB wamejitolea hivyo ni lazima tuwaunge mkono," alisema Zungu.
Vilevile, amekemea vikali tabia ya migambo wa jiji kuwasumbua wajasiriamali wanaotafuta riziki kwa tabu na kuwataka askari mgambo hao wakifanya hivyo wakamatwe pia wafukuzwe kazi.
"Mkuu wa Wilaya najua mnautaratibu wenu mmeshauweka ila hawa migambo wanasumbua ni wakorofi wanataka hata faida ndogo anayoipata mjasiriamali huyu mjasiriamali. Wakamateni muwafukuze kazi," amesema.
Aidha ameishauri Benki hiyo kujikita zaidi katika kuwakopesha wajasiriamali wadogo ambao kimsingi ni wengi ambao katika urejeshaji benki hiyo itapata faida kubwa.
"Muache kuwakumbatia wafanyabiashara wakubwa ambao wengine ni wagumu kulipa," amesema.
Akizungumza awali, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema maonyesho hayo yatakuwa ni endelevu yatakayoendelea kila mwaka. Alisema asilimia 90 ya wakazi wa Ilala ni wajasiriamali hivyo maonyesho hayo yameleta tija.
"Tutashiriki sabasaba tutashiriki nanenane kisha tutashiriki na maonyesho mwakani mwezi kama huu. Lengo letu ilikuwa ni wajasiriamali 3000 lakini wamekuja zaidi ya 3500 na mwakani tunataka tufikie 5000," amesema Mpogolo.
Naye Ofisa Maendeleo Wilaya ya Ilala, Fransisca Makoye ametoa tathimini ya maonyesho hayo na kusema asilimia kubwa wametaka maboresho yakiwemo umeme, kuongeza matangazo, kuongezwa siku pamoja na utaratibu wa utambuzi kwa wafanyabishara kama mamalishe.
"Siku ya mjasiriamali itakuwa ni nzuri, tutafurahi sana kwasababu itatuwezesha sisii wajasiriamali wadogo wadogo tuweze kunufaika kwakuwa tunatengeneza faida," amesema Coreta.
Alisema Coreta Jonas mtengenezaji wa Pilipili za karoti na ukwaju kutoka Segerea jijini hapa.
Naye Suzan Hyera, amesema amefurahiswa kwakuwa itawapanulia masoko ziaid ya bidhaa zao. Alisema siku hizo tatu zimekuwa za kipekee kwakuwa wamepata nguvu ya mikopo ya CRDB pamoja na kupata tenda na soko.
"Tumepata ujuzi mpya kutoka kwa wafanyabiashara wenzetu jambo ambalo tulikuwa hatuna nafasi," alisema Suzan.
Pia, Simba Simba muuzaji wa dawa za asili yeye alizungumzia namna ya kuweka wazi eneo husika ambalo limezibwa alisema mwakani wafungue pawe wazi sambambamba na kufanya zaidi matangazo.