TUONGEE KIUME: Tunavunja ndoa wenyewe tunasingizia Ma MC

Kuna video mbili za harusi zimekuwa gumzo sana kwenye mitandao ya kijamii.

Moja ilikuwa ni kwenye Send Off, mke anamuita mume wake mtarajiwa aende mbele, mume anakwenda.

Mke akiwa na kipaza sauti anaanza kumtambulisha mume wake mtarajiwa kwa mbwembwe, lakini kabla hajafika kokote mume anainama kidogo na kumnong’oneza, “sitaki show off”, akimaanisha hataki ‘mbwembwe.’

Lakini ubaya ni kwamba, kipaza sauti si kilikuwa kinawaka, kwa hiyo ukumbi mzima ukasikia alichokisema mume.

Video nyingine ni tukio kama hilo, mwanamke amemuita mume wake mtarajiwa mbele ampe zawadi ya simu. Mume anapofika mke anaanza kuelezea sababu ya kutoa zawadi hiyo, “mume wangu kazi zake za mbali. Kwa hiyo nataka tukiwa mbali awe na kitu kitakachotusaidia kuwa karibu. Nikitaka kumpigia nimpate, nikitaka kumuona apige picha nzuri kwa sababu simu hii inapiga picha nzuri, anitumie.”

Kisha anamgeukia mume mtarajiwa: “Natumaini utaituma simu hii kwa usahihi. Natumaini unayafahamu matumizi sahihi ya simu.”

“Ndiyo mke wangu mtarajiwa,” jamaa anajibu. “Ni yapi?” mke anauliza kwa sauti ya kuamrisha kama mwalimu wa zamu.

“Nayafahamu,” mume anajibu kwa aibu aibu kidogo. “Ni yapi. Nambie,” mwalimu wa zamu anakazania.

Mume anajichekesha kidogo kisha anasema, “nitajaza simu hii kwa picha zako tu.”

Video hizo zimezua mijadala mingi sana. Lakini kabla ya kufika kwenye mijadala hiyo, tuanzie kwenye video hizo zinafikaje mtandaoni.

Siku hizi kumekuwa na kawaida ya washehereshaji wa sherehe, maarufu MC kusambaza picha na video za matukio ya sherehe walizofanya kazi. Na wanafanya hivi kwa lengo zuri tu kutangaza biashara zao, lakini kwa sababu siku hizi kila mtu ni MC, kupata wateja inahitaji utumie nguvu kwa kiasi fulani. Moja ya nguvu wanayotumia ni kusambaza video au picha zinazoonyesha matukio yanayoweza kuwa gumzo mjini.

Mijadala iliyozuka ni mingi, lakini mmoja unasema kwamba Ma-MC wanachokifanya sio sahihi. Wanasambaza video ambazo kiukweli zinaweza kusababisha ndoa kuvunjika.

Ndoa zetu tunazivunja wenyewe. Tunataka kuingia kwenye ndoa kwa kukurupuka. Kama unafikia hatua ya kuoa mtu ambaye hujui kama anapenda ‘mbwembwe’ maana yake unaoa mtu usiyemfahau na kuna gharama ya kulipa unapooa mtu usiyemfahamu.

Kwa hiyo MC asambaze video au asisambaze uwezekano wa ndoa yenu kuishia njiani ni mkubwa.

Kama unaoa mwanamke ambaye anakupelekesha tena mbele za watu, hiyo haiwezi kuwa ni tabia ngeni, ni kwamba alishawahi kukufanyia sio mara moja, sio mara mbili. Kwa hiyo kama unamjua na unaamini mnaweza kudumu, hilo sio tatizo. Lakini kama humjui, hilo ni tatizo kubwa haijalishi MC alisambaza video au hajasambaza.Kama MC kasambaza video yako bila ridhaa yako mpeleke mahakamani, lakini usimshushie MC matatizo ya ndoa yako.