Vyungu vinasogea na swaumu inaachia

Muktasari:

  • Ukali wa swaumu ni pale unapoianza na unapoimalizia. Waswahili husema mzigo huelemea pale unapokaribia kuutua.

Mambo si mabaya maana naona vyungu vinasogea na swaumu inaachia mdogomdogo. Mwaka huu tena kama miaka mingi tu iliyotangulia, mifungo miwili mikuu Ramadhani na Kwaresima imeumana. Usishangae makulaji huku mtaani yanaendelea kama ada, lakini wenye imani zao wanaendelea na utaratibu wakiwaacha wazee wa kujipasua wakihangaika na michemsho yao.

Ukali wa swaumu ni pale unapoianza na unapoimalizia. Waswahili husema mzigo huelemea pale unapokaribia kuutua.

Maana yake unapoanza kufunga unakatiza utaratibu wa mwili kupokea chakula katika nyakati ulizozoeshwa. Kama unakula rakaa moja kwa siku, muda ukifika ni lazima tumbo liungurume. Lakini hata kama unakula rakaa nne, kila muda wa kupata utalisikia.

Mwili wa binadamu unafanana na jogoo la shamba. Kila alfajiri lazima litawika. Wakulima hulichukulia hiyo kama alama ya muda wa kwenda shamba. Lakini jogoo la Manzese haliko hivyo; umeme ukirudi saa nane za usiku na lenyewe litawika likidhani kumeshakucha! Hapa nazungumzia jogoo la uswahilini; yale ya uzunguni sijui hata kama yanajua kuwika.

Lakini unapokaribia kumaliza mfungo swaumu inashika kwelikweli. Ndio kiza kinene kinapoashiria mapambazuko. Sasa kabla hatujarudi kwenye maisha yetu ya “mchemsho wa kuku na kabia ka baridi” tujikumbushe kidogo mawili matatu kuhusu utamu wa kufunga. Wengi tunajua kuwa kufunga ni nguzo muhimu kwenye dini zote, lakini wapo wasioelewa kuwa kufunga ni nguzo ya maisha pia.

Chakula ni kitu muhimu kwenye maisha yetu. Wanyama hula wanga, protini, vitamini, mafuta na kadhalika. Kuna wanyama walao majani, wengine hula nyama na wengine wanatumia vyote. Na kila mmoja huwa na chakula chake cha mazoea kulingana na mazingira.

Kwa kuwa jamii nyingi duniani hula vyakula kutoka kwa wakulima, wawindaji na wavuvi, wengi hutumia wanga, vitamini na protini. Ulaji wa mazoea hukusanya virutubisho vya aina moja kwa wingi mwilini. Kwa mfano ulaji wa ugali kwa nyama uliopitiliza husababisha wanga, protini na mafuta kuzidi mwilini. Hii mara nyingi huleta shida kwani kila kinachozidi mwilini hugeuka sumu.

Kila siku mwili hupokea sumu nyingi kupitia chakula. Mwili hupigana na sumu hii kupitia viungo vyake (kama moyo, mapafu, maini, na figo) kwa muda mrefu sana wa maisha ya mwanadamu. Kwa kutokuelewa, mwanadamu huyo huongeza sumu zaidi wakati mapambano yakiendelea. Mwisho wa siku viungo hivi huchoka na kuzima data, ndipo tunapoona matatizo sugu yakijitokeza na hatimaye kumdhuru mwanadamu huyu.

Kufunga kuna faida kubwa mwilini. Kwanza unapunguza kwa kiasi kikubwa mapokezi ya sumu mwilini; huwezi kufuturu chipsi-yai (hata nafsi itakataa), bali utaanza na maji kidogo na baadaye vyakula laini, hata vya wastani visivyojazwa mafuta wala madebe ya chumvi. Ndivyo vyenye faida zaidi mwilini na hasa wakati unaukarabati. Wengi tunajali kukarabati magari kabla na baada ya safari, lakini tunaiacha miili yetu ikichoma plagi.

Ni wazi kuwa binadamu hatujui kufanya mawasiliano mazuri na miili yetu. Mtu akihisi maumivu ya kichwa atakimbilia vidonge bila kufikiria kuwa tangu juzi anakunywa mipombe, tena kwenye makelele ya klabu za usiku. Asubuhi akiamka na mning’inio (hangover) atakimbilia makwasukwasu bila hata kutathmini ni kiasi gani cha maji mwili wake ulihitaji, na kiasi gani aliupa.

Ngoja kwanza nikuambie kitu. Kama unatumia vitu vigumu jaribu kufanya zoezi hili: Kunywa shoti yako mapema asubuhi kisha jisikilize kwa dakika chache. Utasikia tumbo likiunguruma, mwenyewe utasema “Ah! Kiboko ya gesi”. Lakini kabla hujamaliza kusema, haja ndogo  itakubana. Utakwenda maliwato na kuiondoa kero hiyo, kisha moja kwa moja utarudi ukaendeleze libeneke.

Kwanza uijue ishara hiyo. Mwili umeumbwa na soketi zote zinazoulinda. Ulipoingiza kinywaji mdomoni ukaona mapokezi magumu ya kinywaji hicho mwilini (ngumu kumeza), ujue hamu inataka lakini mwili unakataa. Ukilazimisha tumbo litapokea, lakini kwa taarifa yako tumbo hupokea kila kitu. Lakini halina ruksa ya kuulisha mwili kila kinachoingia kwake. Ukijisikia kwenda haja ndogo baada ya kunywa “nusu uwanja”, mwili wako uligundua kuwa kuna sumu iliyoingia mwilini.

Ulimi umekataa, tumbo likakataa, lakini kwa sababu wewe umetaka, basi lazima jambo liwe. Figo itatafuta maji ili mwili usidhurike. Kwa haraka maji yatakopwa popote mwilini. Hapo ujue ushapoteza maji kwenye maeneo yako mengi mwilini. Yaliyokwenda kusaidia mzunguko wa damu, kusaidia macho yaone vizuri, kuifanya ngozi iwe na afya njema na mambo mengine.

Shoti ya pili haitakupeleka maliwato. Utasikia hanjamu na hamu ya kuendelea na kinywaji chako. Sasa kumbe hapo ndo unapoharibu. Unaendekeza matamanio bila kuusoma mwili wako unachikihitaji na unachokikataa. Wanasema si kila kinachong’aa ni dhahabu, na ndivyo sio kila unachokitamani kinakufaa.