Wadau washauri namna bora kukifufua kiwanda cha Urafiki

Muktasari:
- Kutokana na ongezeko la watu na ucha-kavu wa miundombinu yake, Profesa Sem-boja anasema hakuna haja ya kuwekeza zaidi kwenye kiwanda hicho na itapendeza endapo eneo husika litabadilishiwa matu-mizi.“Kiwanda cha leo kinahitaji teknolojia ya juu na miundombinu ya kisasa. Hiki kilichopo kilikuwa kinategemea watu wengi zaidi.
Wakati uzalishaji ukiwa umesi-tishwa kwa zaidi ya miezi sita sasa, wataalamu wameshauri namna bora ya kukifufua Kiwanda cha Urafiki chenye zaidi ya miongo sita tangu kianzishwe.Kwa ilivyo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja anasema ipo haja ya kubadili mtazamo juu ya kiwanda hicho muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Kutokana na ongezeko la watu na ucha-kavu wa miundombinu yake, Profesa Sem-boja anasema hakuna haja ya kuwekeza zaidi kwenye kiwanda hicho na itapendeza endapo eneo husika litabadilishiwa matu-mizi.“Kiwanda cha leo kinahitaji teknolojia ya juu na miundombinu ya kisasa. Hiki kilichopo kilikuwa kinategemea watu wengi zaidi.
Ikiwezekana eneo lile liuzwe na matumizi yake yabadilishwe kisha hela itakayopatikana itumike kujenga kiwanda cha kisasa sehemu nyingine,” anasema.
Msomi huyo anapinga suala la kukifufua kiwanda hicho na anapendekeza litafutwe eneo jingine sehemu ambako kuna nafasi ya kutosha ili kiendelee kutumia rasilimali zinazozalishwa nchini.Licha ya kukiondoa mjini, anasema:
“Yanahitajika mabadiliko makubwa kuan-zia menejimenti, teknolojia hata miun-dombinu mingine muhimu.”Anasema umefika wakati kwa Serikali kujielekeza kwenye uwekezaji wa viwanda vya maeneo mengine kama gesi na madini na kuiachia sekta binafsi kuzalisha nguo na bidhaa zinazofananazo.
“Sekta binafsi inaweza kupata mtaji wa kutosha kujenga kiwanda cha kisasa zaidi. Zipo njia nyingi za kufanya hivyo, inawe-za kuwa kwa kuuza dhamana, hisa hata kukodisha mitambo kutoka kwa waten-genezaji wakubwa duniani,” anasisitiza mwanazuoni huyo.
Mchumi na mtafiti mwandamizi, Profesa Samwel Wangwe anasema Urafiki ni mion-goni mwa viwanda vinavyopaswa kupewa kipaumbele hasa kipindi hiki Serikali iki-tekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Badala ya kutumia nguvu nyingi kujenga viwanda vipya maeneo mengine, anasema ipo haja ya kutumia miundombinu imara iliyojengwa katika kiwanda hicho kwa kutumia rasilimali nyingi za Taifa.
“Awali kiwanda hiki kilikuwa kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Kuna somo muhimu tunajifunza hapa, tunapokaribisha wawekezaji ni lazima tuwasimamie kwa ukaribu kuhakikisha wanatekeleza makubaliano kwa wakati uliowekwa,” anasema.
Taarifa kwamba kiwanda hicho kimesitisha uzalishaji tangu Desemba 2017 anasema zinadhihirisha kukosekana kwa umakini kwani ni suala ambalo lilipaswa kuripotiwa na bodi ya wakurugenzi ili hatua za makusudi zichukuliwe.
“Tunapokaribisha mwekezaji kutoka nje ni lazima asimamiwe kwa ukaribu. Aongeze mtaji, alete teknolojia mpya na aongeze ajira. Haya yote yafanywe ndani yamuda uliokubaliwa, akishindwa kuyatekeleza basi mkataba usitishwe,” anasisitiza.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikitembelea kiwanda hicho na kukuta hali isiyoridhisha na kubainisha kwamba Serikali hairidhiki na ubia uliopo uliodumu kwa zaidi ya miaka 22 sasa.
“Serikali haturidhiki na huyu mbia aelewe kwamba Serikali haturidhishwi na kinachoendelea hapa kiwandani,” alisema Waziri Majaliwa.
Tangu kilipoanzishwa mwaka 1966 kiwanda hicho kilikuwa nguzo ya uchumi wa Taifa lakini utekelezaji wa sera ya ubinafshaji uliilazimu Serikali kuikaribisha kampuni ya Changzhou State owned Textile Assets Operations kutoka China ili kupata mtaji, teknolojia na kuongeza ajira lakini hali imekuwa kinyume kabisa.
Kiwanda hicho kina uwezo uliosimikwa wa kuzalisha mita milioni 33 za vitambaa mbalimbali lakini kwa sasa, kinazalisha kati ya mita milioni nne mpaka tano. Hali hiyo inasababishwa na kuondolewa kwa baadhi ya mashine zilizokuwapo bila kubadilishwa.
Naibu meneja mkuu wa kiwanda hicho, Shadrack Nkelebe anasema hali itakuwa mbaya zaidi mwaka huu kwani uzalishaji umesimama tangu Desemba 2017 kupisha ukarabati wa mitambo na mashine zilizopo ambazo hata hivyo vipuri vyake bado havijawasili.
“Tanzania inaathirika zaidi kiwanda hiki kisipofanya kazi. Pamba ya wakulima inakosa soko la uhakika la ndani, wafanyabiashara wanalazimika kutafuta bidhaa nje ya nchi huku ajira zikipotea pia. Wananchi nao wananyimwa haki ya kutumia bidhaa zao,” anasema Nkelebe.
Ubinafsishaji
Ubia wa Serikali na kampuni ya Changzhou State owned Textile Assets Operations ulianza mwaka 1996 ili kukiongezea uwezo kiwanda cha Urafiki kuzalisha zaidi.
Kabla ya ubia huo, takwimu zinaonyesha kiwanda hicho kilikuwa kimewahi kuzalisha mpaka mita milioni 31 ambazo ni zaidi ya asilimia 93 ya uwezo wake uliosimikwa.
Wakati kinabinafsishwa, kwa Serikali kupitia Hazina kumiliki asilimia 49 na kampuni hiyo ya Kichina asilimia 51, uzalishaji ulikuwa kati ya mita milioni tisa mpaka 15. Zaidi ya watumishi 3,000 walikuwa wanafanyakazi kiwandnai hapo wakiingia kwa kupokezana. Kwa sasa, wamebaki watumishi 726 tu.
Badala ya kuongeza ajira, watumishi wa kiwand ahicho walikuwa wanapunguzwa wakati menejimenti ikiwa na matumaini ya kushusha gharama za uendeshaji. Lakini kitu ambacho hakikuangaliwa kwa umakini ni watu wanaopaswa kuwapo ili kiwanda kijiendeshe.
Nkelebe anasema wakati huo, kulikuwa na shifti tatu zenye zaidi ya wafanyakazi 1,000 kila moja lakini walipokuja Wachina hao mambo yalianza kubadilika taratibu.
“Kwanza walipunguza idadi ya shifti, zikabaki mbili. Baadaye wakapunguza tena ikabaki moja. Hata hivyo gharama za uendeshaji ziliendelea kuwa juu hivyo wakapunguza idadi ya wafanyakazi kwenye hiyo shifti iliyobanki,” anasema.
Kutokana na kupungua kwa idadi kubwa ya watumishi hao hata kuwa chini ya wastani ya wanaohitajika, uzalishaji ukaanza kupungua kwa kukosa nguvukazi ya kutosha.
Kutokana na wingi wa hisa, mbia huyo ndiye anayefanya uamuzi mwingi kwa ajili ya kiwanda hicho. Mwaka 2002 takriban mashine 90 ziling’olewa kwenye magodauni matatu na zikauzwa kama vyuma chakavu kwa matumaini ya kuleta mpya ambazo mpaka leo hazijaja.
Alipotembelea kiwandani hapo, Majaliwa alielezwa kuwa mitambo iliyonunuliwa na mwekezaji kati ya miaka mitano au sita iliyopita haifanyi kazi tangu ilipoletwa nchini na akataka majibu menejimenti kutoka kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji.
Nkelebe anasema: “Kuna mashine zilizonunuliwa kinyume na utaratibu zililetwa lakini mpaka leo hazijafungwa ili zifanye kazi iliyokusudiwa. Baadhi zimechoka, zipo zilizopitwa na wakati pia.”
Uhakika wa soko
Mwanzoni mwa mwaka jana, katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira alikitembelea kiwanda hicho akiw apamoja na wakuu wa vikosi vya majeshi yaliyo chini yake.
Kuhamasisha uchumi wa viwanda, Rwegasira alikipa kiwanda hicho zabuni ya kushona sare zote za askari wake nacho kikaipokea zabuni hiyo kubwa.
Lakini, pamoja na upendelea huo, Urafiki haijawahi kufanya chochote tangu ipewe zabuni hiyo na kwa miezi sita iliyopita, kimesimamisha uzalishaji kabisa.
“Ni kama mgonjwa aliyezidiwa. Anapewa chakula lakini anashindwa kula. Lazima apekelwe (chumba cha uangalizi maalumu) ICU. Hatuna uwezo wa kuihudumia zabuni ya wizara hiyo,” anasema Nkelebe.
Uwekezaji
Imeshabinika kuwa ubia uliopo hauna tija kwani mwekezaji huyo ameshindwa kukidhi matarajio yaliyokuwapo kwa muda mrefu. Hajaongeza mtaji wa kiwanda wala kuleta teknolojia mpya kama ilivyokusudiwa.
Mbaya zaidi, amepunguza ajira alizozikuta, ameshsusha uzalishaji hivyo kuathiri sekta ya uzalishaji nguo na mnyororo wake wa thamani kwa kiasi kikubwa.
Kuondoa changamoto zinachokikabili kiwanda hicho na kukirudisha kwenye hadhi ilichokuwa nacho, Nkelebe anasema uwekezaji mkubwa unahitajika ambao ama unahitaji kujitoa kwa Serikali au kutafuta mbia mpya mwenye uwezo unaostahili.
Naibu meneja huyo anasema: “Kiwanda kinahitaji Sh100 bilioni mpaka Sh110 bilioni kununua mitambo muhimu inayohitajika. Mbia hana uwezo huo na yeye mwenyewe anakiri kuwa ipo haja kwa Serikali kuchukua hatua kukinusuru kiwanda hicho.”
Katika jitihada za kukinusuru, Waziri Mkuu alisema kiwanda kilikopa fedha kutoka Benki ya Exim ya China lakini hazijaletwa nchini kutekeleza lengo lililokusudiwa. Hata hivyo, Serikali inachunguza matumizi ya mkopo huo.
Kaimu msajili wa Hazina, Maftah Bunini anasema bado wanaendele akufanya tathmini kujua kinachohitajika kufanywa ili kukinusuru kiwanda hicho.
Anasema kwa kuwa uendeshaji wake ni wa ubia, ni lazima pande zinazohusika zikutane na kujadiliana changamto zilizopo kwa kina kabla ya kupata majibu ya kina.
“Hazina peke yake haiwezi kufanya uamuzi mpaka tutakapokutana na mbia mwenzetu. Baada ya kikao chetu Serikali itasema mikakati itakayoafikiwa ili kukifufua kiwanda hicho,” anasema Bunini.