Ukweli kuhusu maziwa na uondoaji vumbi mwilini

Dar es Salaam. Umewahi kusikia mtu anayefanya shughuli kwenye eneo lenye vumbi akisema amejiwekea utaratibu wa kunywa maziwa kila siku, ili kupunguza uwezekano wa madhara yanayoweza kujitokeza kwa vumbi hilo kuingia kwenye mfumo wa hewa?

Inawezekana jambo hili tumelisikia mara nyingi na wengi tunaamini kwamba maziwa yanaweza kuwa tiba ya vumbi tunalovuta.

Seleman Mashimba, dereva wa bodaboda anasema katika ratiba yake amejiwekea kila siku kupata kikombe cha maziwa, ili kuweka sawa kifua chake kutokana na kazi anayofanya.

Akizungumza na Mwananchi, Mashimba anasema mara nyingi anatembea kwenye barabara zenye vumbi, hivyo hutumia maziwa kupunguza athari anazoweza kuzipata kwenye kifua chake.

“Utaratibu wangu ni kwamba kila siku jioni lazima ninywe maziwa ya moto kikombe kimoja, kazi ninayofanya ni ngumu, kutwa nzima upo barabarani vumbi lote linakuishia,” anasema Mashimba.

Hili limeelezwa pia na Rehema Seif, anayefanya biashara ya mama lishe, mara moja moja na yeye hutumia maziwa kwa lengo la kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na moto anaovuta wakati wa kupika.

Wakati hao na wengi kati yetu tukiamini hivyo, wataalamu wa afya wanasema hakuna utafiti uliowahi kufanyika na kuthibitisha ufanisi wa njia hiyo na inabaki kuwa dhana ambayo si sahihi.

Akizungumzia hilo, daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Sadick Sizya anasema dhana hiyo imekuwepo kwa muda mrefu kwenye jamii, lakini si sahihi kama ilivyo kwa dhana nyingine potofu.

Anasema hakuna uhusiano wowote wa yanakopita maziwa na mfumo wa hewa ambao ndio unapitisha vumbi na moshi, hivyo unywaji wa maziwa hauna msaada katika kuondoa vumbi.

Mtaalamu huyo alieleza hakuna njia inayoweza kutumika kuondoa vumbi au kupunguza athari zinazoweza kujitokeza baada ya vumbi kuingia kwenye mfumo wa hewa wa binadamu isipokuwa kuzuia vumbi hilo lisiingie.

“Vumbi, moshi, harufu na aina zote za hewa tunazovuta zinapita kwenye mfumo wa hewa, maziwa yanapita kwenye mfumo wa chakula ambao unaanzia kwenye koo hadi tumboni. Kwa hiyo ukiangalia hapo kwa haraka utaona ni mifumo miwili tofauti ambayo haiingiliani.

“Utakuta mtu anaamini vumbi lililoingia kwenye mapafu kwa njia ya hewa, akinywa maziwa yataliondoa au kusafisha mapafu, hizi ni nadharia au tuseme imani ambazo tumezirithi vizazi na vizazi ila hazina ukweli wowote,” anasema Dk Sizya.

Mbali na tofauti za njia zinazopita vumbi na maziwa, mtaalamu huyo anaeleza hata virutubisho vilivyopo kwenye maziwa hakuna kinachofanya kazi ya kupunguza au kuondoa athari za vumbi au moshi kwenye mapafu.

“Maziwa yana protini, maji, madini ya calcium, fat, hivi vitu vyote havina uhusiano na kusafisha mapafu kuondoa vumbi, kitu ambacho mtu anatakiwa kuzingatia anapofanya kazi sehemu ya vumbi avae barakoa zile za N95, zinasaidia kukinga vumbi hata moshi,” anasema.