Chanjo, uchunguzi wa homa ya ini kutolewa bure Muhimbili
Muktasari:
- Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa watu wengi huishi na maambukizi ya homa ya ini B au C kwa miaka mingi bila dalili, hali inayosababisha wengi kufika hospitalini wakiwa tayari wamepata madhara makubwa, ikiwemo ini kusinyaa (cirrhosis) au saratani ya ini.
Dar es Salaam. Wananchi watapata fursa ya kupata chanjo ya homa ya ini, kupimwa, kuchunguzwa na kuanza matibabu bila malipo katika kambi maalumu itakayofanyika Julai 28, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani.
Kambi hiyo imeandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na kampuni ya dawa ya Mega We Care na itafanyika katika kliniki ya Muhimbili Sokoine Drive Medical Centre (MNH-SDMC), iliyopo mkabala na reli ya SGR jijini Dar es Salaam.
Lengo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu homa ya ini, kuhamasisha uchunguzi wa mapema, kutoa kinga kupitia chanjo kwa wanaostahili na kuhakikisha wanaobainika kuwa na maambukizi wanaunganishwa na huduma za matibabu.
Homa ya ini imeendelea kuwa moja ya magonjwa yanayochangia vifo duniani kutokana na wagonjwa wengi kutogundulika mapema. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa watu wengi huishi na maambukizi ya homa ya ini B au C kwa miaka mingi bila dalili, hali inayosababisha wengi kufika hospitalini wakiwa tayari wamepata madhara makubwa, ikiwemo ini kusinyaa (cirrhosis) au saratani ya ini.
Mbali na uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa huo, changamoto nyingine ni idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupima, gharama za baadhi ya vipimo vya kina na unyanyapaa unaowafanya baadhi ya watu kuchelewa kutafuta huduma.
Katika maandalizi ya kambi hiyo, kampuni ya Mega We Care imechangia dawa na mahitaji mengine ya kitabibu yatakayotumika katika utoaji wa huduma, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Akizungumza leo, Julai 25, 2026, kuhusu ushiriki wa kampuni hiyo, Ofisa Habari wa Mega We Care, Mengi Ntasimba, amesema wanatambua umuhimu wa kuwekeza katika kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa.
"Ushiriki wetu ni sehemu ya kurudisha kwa jamii. Tunaamini wananchi wengi watanufaika kwa kupata elimu, uchunguzi na huduma zinazoweza kuokoa maisha," amesema.
Kwa upande wake, Hospitali ya Taifa Muhimbili imesema kambi hiyo itatoa huduma mbalimbali zikiwemo elimu ya afya, uchunguzi wa homa ya ini, chanjo kwa wanaostahili, ushauri wa kitaalamu pamoja na kuanzishiwa matibabu kwa watakaobainika kuwa na maambukizi.
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa homa ya ini B inaweza kuzuilika kwa chanjo, huku matibabu ya kisasa yakisaidia kudhibiti ugonjwa huo na kupunguza hatari ya kupata madhara makubwa endapo maambukizi yatagundulika mapema.
Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani hufanyika kila Julai 28 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, kuhamasisha kinga, uchunguzi wa mapema na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za matibabu kwa wakati.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mamilioni ya watu duniani wanaishi na maambukizi sugu ya homa ya ini B na C, huku wengi wao wakiwa hawajui hali zao. Hali hiyo imeifanya homa ya ini kuwa miongoni mwa sababu zinazoongoza kwa vifo vinavyotokana na magonjwa ya ini, jambo linalosisitiza umuhimu wa kuimarisha uchunguzi wa mapema, chanjo na upatikanaji wa matibabu.