Choo kigumu baada ya kujifungua, suluhisho lake
Muktasari:
- Makala inazungumzia changamoto ya choo kigumu kwa wanawake baada ya kujifungua, ikieleza kuwa inasababishwa na mabadiliko ya homoni, kukua kwa mfuko wa uzazi, na matumizi ya dawa za madini ya chuma.
Dar es Salaam. Changamoto zinazoweza kutokea baada ya mama kujifungua, ni tatizo la kupata choo kigumu. Tatizo hili linaweza kuathiri hali ya faraja na afya yake lakini pia hali ya mtoto.
Aidha, hali hii ya kupata choo kigumu inaweza kuathiri afya ya akili ya mama baada ya kujifungua lakini pia kuongeza maumivu kwa wale waliojifungua kwa njia ya upasuaji na hata ya kawaida.
Wakati anapata choo hicho kigumu, bado anatakiwa kuendelea kula mlo kamili kwa kuzingatia lishe ili mtoto apate virutubisho vyote muhimu katika ukuaji wake.
Hivyo kuna umuhimu wa kumsaidia mama huyu kuwa na unafuu katika kipindi hicho.
Inaelezwa kuwa wanawake wengi wanaweza kuwa na maswali kuhusu aina za vyakula wanavyopaswa kula ili kuandaa maziwa wakati wa kunyonyesha, lakini pia njia gani sahihi ya kuhakikisha wanaepuka tatizo la kupata choo kigumu baada ya kujifungua.
Hata hivyo, Mwananchi limezungunza na baadhi ya mashuhuda waliokumbwa na kadhia ya choo kigumu na wamesimulia hatua walizozichukua kulikabili tatizo hilo.
Caren Joseph (36) mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam anasema tatizo lake lilianza akiwa na ujauzito wa miezi minane, lakini hakujua chanzo chake.
“Nilianza kupata choo kigumu wakati wa ujauzito, japo sikuona kama ni tatizo linalosababishwa na ujauzito, hivyo nikawa makini kutumia vyakula laini kama mtori na matunda bado tatizo halikuisha,” anasimulia mama huyo.
Anasema tatizo hilo alienda nalo mpaka alipojifungua kwa upasuaji na kutokana na maumivu ya mshono, alipata shida kila alipokuwa anataka kwenda haja kubwa.
Anasema alikuwa anapata maumivu makali hivyo aliamua kwenda hospitali kupata suluhu ya tatizo hilo.
Caren anasema baada ya kumweleza daktari kuhusu adha aliyopitia, alimpa ushauri, dawa na vyakula alivyotakiwa kula sambamba na vinywaji ili kumaliza kabisa tatizo.
Shuhuda mwingine ni Irene Malya (30) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, amesema katika safari yake ya ujauzito alikutana pia na tatizo hilo kabla ya kujifungua na alipoenda kwa daktari aliambiwa ni tatizo linalosababishwa na kutofanya mazoezi mara kwa mara.
“Daktari alisema kutofanya mazoezi kunasababisha chakula kujirundika na kushindwa kumeng’enywa vizuri, lakini kula chakula kigumu pia ni chanzo,” anasema na kuongeza kuwa baada ya kuzingatia alivyoelekezwa na daktari tatizo liliisha,” amesema Irene.
Chanzo cha tatizo
Mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Paul Masua anataja visababishi vya tatizo la choo kigumu baada ya kujifungua ni pamoja na mabadiliko ya homoni, kukua kwa mfuko wa uzazi na tatu uwepo wa mtoto kwenye mfuko wa uzazi.
Anasema uwepo wa mtoto kwenye mfuko wa uzazi husababisha utumbo kukandamizwa na matokeo yake ni kupungua kwa spidi na utendaji kazi wa kumeng’enya chakula ndani ya utumbo na kubwa zaidi, ni homoni ya projestini nayo ni moja ya chanzo cha utumbo kupoteza ustadi wake kipindi cha ujauzito.
“Uwepo wa homoni hii kwa mjamzito ndiyo hasa husababisha uchovu na huwa chanzo cha choo kigumu kutoka akiwa na ujauzito na baada ya kujifungua,” amesema.
Amesema vyanzo hivyo ndivyo husababisha hali hiyo na tatizo hili hudumu kwa siku 40 mpaka miezi sita.
Hata hivyo, anasema ili kuondokana na tatizo hilo, mama aliyejifungua anapaswa kula vyakula vyenye matunda na mboga za majani kwa wingi sambamba na maji lita mbili kila siku.
Amesema hiyo ni kutokana na vidonda anavyokua navyo mama huyo kwa sababu vitu hivyo havitoshi kumuondolea tatizo.
“Mjamzito anapata vidonda wakati wa kujifungua kutokana na wengine kufanyiwa upasuaji na wengine kuongezewa njia kwa wanaojifungua kawaida, hivyo vitu hivi si rahisi kumaliza tatizo,” anasema Dk Masua.
Anasema njia nyingine za kumaliza tatizo hilo kwa wale wenye vidonda ambavyo vitasumbuka wakati wa haja endapo itashindikana kutibika kwa njia za matunda na maji, anapaswa kupewa vidonge.
“Tatizo hili likiwa kubwa inabidi mgonjwa tumpatie dawa za kulainisha choo, hii ni baada ya mama kushauriwa zaidi lakini dawa hizi pia zinaposhindikana, tunampa dawa ya mwisho ambayo ni ya kuharisha.”
Dk Masua anasema kipindi hicho baada ya kujifungua mama anapaswa kufanya mazoezi laini angalau nusu saa kwa siku, ambayo nayo ni tiba, lakini pia kupata muda mzuri wa kupumzika, lakini pia kipindi cha ujazito ayafanye hayo ili kuepukana na haya pindi anapojifungua.
Hata hivyo, matumizi ya dawa za kuongeza madini ya chuma kwa wamama wajawazito na kwa mtu yeyote yule yanatajwa kuwa chanzo kikubwa cha kupata choo kigumu.
Zingatia
Wataalamu wa afya wanasisitiza katika kipindi cha ujauzito, ili kuepuka tatizo la choo kigumu unapaswa kufuata mapendekezo ya lishe yenyenyuzinyuzi nyingi, kunywa maji ya kutosha lakini pia kufanya mazoezi yale unayotakiwa kutokana na hali yako.
Matumizi ya vyakula vya mafuta kwa mama mjamzito yanaweza kuboresha afya yake ya utumbo na kupunguza matatizo yanayohusiana na choo kigumu na ikiwa matatizo haya yanashindikana kushughulikiwa kupitia hatua hizi, ni muhimu kuwasiliana na daktari ili kupata msaada wa kimatibabu.