Fanya haya kuepuka changamoto za uzazi

Wanawake wenye kisukari mara nyingi hupata changamoto mbalimbali katika ushikaji wa ujauzito kuliko wanawake ambao hawana ugonjwa huo. Zaidi ya ugonjwa wa kisukari, kuna sababu nyingi zinazohusiana na ugonjwa wa kisukari zinazochangia changamoto hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo ni kuwa na uzito mkubwa na mafuta mengi kwenye kizazi, kupata hedhi isiyo ya kawaida au kukata kabisa kwa hedhi. Baadhi ya wanawake wenye kisukari hupata hedhi isiyo ya kawaida ambayo inaweza kufika katika mzunguko wa siku 35 au zaidi na wengine kutopata kabisa hedhi. Pia kisukari kinaweza kusababisha kukoma hedhi kabla ya umri.

Kwa upande wa wanaume, mbali na kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa, figo na shinikizo la damu, pia wana uwezekano mkubwa wa kuwa tasa. Kisukari kinaathiri uzazi wa kiume kwa njia nyingi, kama ukosefu wa nguvu za kiume, uharibifu wa neva ambayo inaweza kusababisha ugumu katika kusimamisha uume. Pia wana uwezekano mkubwa wa kupata changamoto ya kupungua kwa wingi wa mbegu za kiume na manii.

Kutokana na hali hiyo, ni muhimu mwanamume au mwanamke kuzungumza na daktari mapema, ili kuhakikisha unadhibiti ugonjwa wa kisukari kabla ya kujaribu kupata ujauzito.

Wanawake wenye ugonjwa wa kisukari wana uwezo wa kushika mimba na kwa wanaume pia uwezo wa kumpa ujauzito mwanamke, lakini watafanikiwa hilo ikiwa wataweza kuishi katika misingi thabiti ya ugonjwa wa kisukari.

Ni muhimu kudumisha afya kwa kuzingatia ulaji wa vyakula sahihi pamoja na kufanya mazoezi kama kukimbia, kuogelea, kuendesha baskeli au kufanya yoga. Pia kuzingatia matumizi ya dawa au sindano ni muhimu. Ukifanya haya unaweza kuondokana na changamoto ya uzazi. Ikiwa kuna tatizo lingine mbali na ugonjwa wa kisukari, ni muhimu kumjulisha daktari.


Mwandishi wa makala hii, Lucy Johnbosco ni mshauri wa wagonjwa wa kisukari.