Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hofu ikipitiliza inaweza kuwa tatizo la afya ya akili

Muktasari:

  • Hofu ni suala la kawaida na linaweza kumkumba mtu yoyote kwa kuwa ni sehemu ya maumbile yetu. Hata hivyo, hofu inapozidi kuna uwezekano wa mhusika kuwa na tatizo la afya ya akili

Binadamu ameumbwa kuwa na hofu kama mbinu mojawapo ya kimwili kujihami na matukio mbalimbali ya kila siku tunayokutana nayo maishani.

Ha ta hivyo, hofu inapopitiliza inaweza kuwa ni tatizo la afya ya akili hivyo kuhitaji uchunguzi, matibabu na ushauri katika huduma za afya.

Tatizo hili hujulikana kitabibu kama Generalised Anxiety Disorder (GAD). Ni tatizo linalotajwa kuwakosesha watu fursa za kimaisha ikiwamo kushindwa usaili wa ajira, mitihani na kujieleza katika hadhara.

Hofu iliyopitiliza huambatana na wasiwasi au woga juu ya maisha ya kila siku na matukio yake bila hata mhusika kuwa na sababu ya msingi.

Mara nyingi watu wenye tatizo hili huwa na tabia ya kuhisi janga kubwa litawatokea karibuni au maafa yatamkumba katika maisha yake au familia yake.

Waathirika hawa wana kawaida ya kutoacha kuwa na hofu isiyo na sababu juu ya familia zao, fedha, afya, ajira, mali, masomo na biashara zao.

Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi na huzuni na hatimaye hofu huitawala akili kiasi cha kuingilia utendaji wake wa kila siku ikiwemo kazi, masomo, kijamii na uhusiano.

Chanzo cha hofu iliyopitiliza

Chanzo halisi cha tatizo hili , lakini yapo baadhi ya mambo yanahusishwa na uwepo kwa tatizo hili ikiwamo nasaba (chembe za urithi), mfumo wa kemikali za ubongo na mazingira.

Baadhi ya ripoti za kiutafiti zinaonyesha kuwa chembe za urithi zina nafasi kubwa ya kumfanya mtu anayetoka katika familia yenye historia ya tatizo hili kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata tatizo hilo.

Tatizo hili pia limehusishwa na kuwepo kwa kiwango kisicho sawa cha baadhi ya kemikali za mfumo wa fahamu katika ubongo, zinazosaidia kusafirisha taarifa katika ubongo kutoka seli moja kwenda nyingine.

Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko katika utendaji kazi wa ubongo na hivyo kusababisha mtu kupatwa na hofu iliyopitiliza.

Mazingira tunayoishi na matukio kama vile ajali mbaya, kuumia kihisia, matukio mabaya yaliyoganda akilini ikiwamo manyanyaso, kufiwa na mtu karibu, talaka, kubadilisha, kuachishwa au kufukuzwa kazi au shule.

Hofu huongezeka ukubwa na kuwa mbaya zaidi, endapo mwathirika akiwa na matatizo makubwa kimaisha, matumizi ya vilevi, tumbaku au kahawa. Haya nayo yanaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hili.

Vile vile watu waliokuwa watumiaji wakubwa wa vitu hivi na kuacha ghafla, wapo katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili.

Mara nyingi tatizo hili huanza kipindi cha utoto au kabla ya umri wa balehe, ingawa pia inaweza kutokea wakati wa utu uzima huku waathirika wakiwa wanawake kuliko wanaume.

Viashiria na dalili za hofu iliyopitiliza

Hofu isiyo na kikomo huathiri zaidi uwezo wa mtu wa kufikiri na hapo baadaye huweza kusababisha matatizo ya kiafya katika mwili ikiwamo shinikizo la juu la damu, kukonda na vidonda vya tumbo.

Hali hii inaweza kuambatana na dalili mbalimbali ikiwamo zinazohusu uwezo wa kufikiri na utendaji kazi wa mwili.

Baadhi ya dalili hizo ni pamoja na hisia ya kuwepo kwa janga wakati wowote, wasiwasi, kujihisi kutaka kukimbia katika hatari, rangi ya ngozi kupauka na kujihisi ngozi kuwaka moto.

Kupata hisia za koo kubana, kufunga au kukabwa na kitu kooni, kupata hali ya kuchanganyikiwa, kujihisi kutengwa na ulimwengu, kupoteza hisia chanya, kutojitambua na kujihisi mtu anayeota.

Dalili nyingine ni kizunguzungu, kuhisi kichwa kuwa chepesi, kupepesuka wanapotembea, kuhisi mvurugano wa hisia, hofu ya kurukwa akili na hofu ya kupoteza uwezo wa kujithibiti mwenyewe.

Kujihisi kitu kinabana kichwani kama vile uliyezungushiwa kamba au mpira, kuhisi baridi au joto sana hata kama hali ya hewa ni kinyume na hisia hiyo.

Kushindwa kujituliza, kuhisi tumbo kubana au kuvurugika, kichefuchefu, kutapika, kujihisi ganzi au vitu kuchomachoma mwilini, woga na kuziba masikio.

Nyingine ni moyo kwenda kasi na kudunda sana, maumivu makali kifuani, shingoni, mabegani, kichwani au usoni, kuhisi kukosa hewa au kupumua kwa shida, kutokwa jasho na kifua kubana.

Pia, kutetemeka kunakoonekana waziwazi au kutetemeka kwa ndani bila mtu mwingine kujua, kuhisi haja ndogo au kubwa mara kwa mara, uchovu kila wakati, kukosa au kupata usingizi nusunusu.

Uchunguzi na matibabu

Iwapo mgonjwa atakuwa na dalili na viashiria vya tatizo hili, daktari atachimba historia ya mgonjwa kwa maswali mbalimbali na baadaye atamfanyia uchunguzi wa kimwili.

Ingawa hakuna kipimo cha kuweza kugundua ugonjwa huu, lakini daktari anaweza kuagiza kufanyika vipimo vingine ili kubaini matatizo mengine ya kiafya.

Iwapo hana tatizo lolote la kiafya katika mwili, daktari atampeleka kwa wataalamu wa afya ya akili kwa matibabu na ushauri zaidi.

Matibabu ya tatizo hili kwa kawaida hujumuisha matumizi ya dawa pamoja na tiba isiyohitaji dawa, ikiwamo tiba ya kujitambua inayojulikana kitabibu kama Cognitive-behavioral therapy (CBT).

Hofu iliyopitiliza haina kinga ya moja kwa moja, bali kuna baadhi ya mambo ambayo husaidia kupunguza makali ya viashiria na dalili za tatizo hili.

Mgonjwa aepuke au kupunguza matumizi ya vyakula au vinywaji kama vile kahawa, chai, Kola au chokoleti na dawa zozote zenye vitu vinavyoamsha tatizo hili.

Mgonjwa afanye mazoezi mepesi ya mwili ikiwamo kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli, kuogelea na kucheza mziki au ngoma za asili angalau nusu saa kwa siku.

Mgonjwa aepuke kurundika mawazo yasiyotatulika kichwani badala yake awe muwazi kwa ndugu, jamaa, rafiki wa karibu au kutafuta msaada kwa washauri na watoa nasaha.

Ajifunze mbinu za kudhibiti msongo wa mawazo kwa kufanya mazoezi laini kama yoga, masaji, kucheza miziki laini, kujifunza kupiga vyombo vya muziki na kutembelea sehemu za kuvutia.

Hofu iliyokithiri inaweza kuwa ni tatizo la kiakili lisilohitaji dawa, endapo una viashiria na dalili nilizotaja.