Hospitali ya ‘Kokilaben Dhirubhai Ambani’ kunoa wataalamu nchini
Dar es Salaam. Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Rais Samia Suluhu Hassan afanye ziara ya kikazi nchini India, Hospitali ya matibabu bingwa nchini humo ya Kokilaben Dhirubhai Ambani inatarajia kufungua tawi lake nchini Oktoba 28, 2023.
Tawi hilo ambalo pia litakuwa ni Kituo cha ushirikiano wa hospitali hiyo jijini Dar es Salaam linatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu maalum nchini na Afrika Mashariki kwa jumla na kuhakikisha utolewaji wa huduma za afya unakuwa wa haraka na rahisi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 24, 2023 na Mkurugenzi, Huduma za Afya wa kituo hicho, David Dickson, na kuongeza kuwa; Mgeni rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
“Tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu lakini pia Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hii, Dk. Santosh Shetty anatarajia kuhudhuria.
“Kituo hiki kitakuwa kitovu cha kurahisisha mafunzo ya madaktari, programu za kubadilishana, na kushirikiana maarifa kati ya wataalamu wa matibabu wa Kitanzania na India. Timu zenye uzoefu kutoka Hospitali ya Kokilaben zitakuwa tayari kutoa mafunzo na kusaidia wataalamu wa matibabu wa Kitanzania,”amesema Dickson.
Wakati ushirikiano kati ya Tanzania na India ukileta matunda hayo pia Oktoba 12, 2023 Waziri Ummy alisema ushirikiano na hospitali kubwa za nchi ya India utaendelea ili wataalamu wa Tanzania wapate ujuzi mpya utakaosaidia ikiwamo utengezaji wa dawa.
“Tukianza uzalishaji wa dawa nchini sasa tutakuwa na uwezo wa kudhibiti bei ya dawa baada ya kuachana na uingizaji dawa kwa asilimia 80 kutoka nje hivi sasa na 60 zinatoka nchini India,”amesema Waziri Ummy.
Kauli ya Waziri Ummy inaendana na mpango wa Hospitali ya matibabu bingwa nchini humo ya Kokilaben Dhirubhai Ambani wa kuwaongezea ujuzi wa kitabibu madaktari wa Kitanzani.
“Hatua hii ya ushirikiano inakusudiwa kubadilisha huduma za afya nchini Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki, kutuweka katika hatua ya kuanzisha kitovu ambapo madaktari na wauguzi wa Kitanzania watajifunza elimu ya matibabu kwa teknolojia ya kisasa na viwango vya kimataifa, ili kukidhi mahitaji ya jamii katika huduma za afya.
“Hivyo, kuondoa haja ya matibabu ya gharama kubwa nje ya nchi na kupunguza mzigo wa kifedha kwa serikali, hivyo kufanya kuwa wazo la kubadilisha huduma za afya kwa manufaa ya Watanzania wote,”amesema na Kuongeza Dickson.