Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kifaa cha kupima UTI nyumbani chaanza kutumika Tanzania, chaibua mjadala

Muktasari:

  • Ingawa takwimu za kitaifa kuhusu kiwango cha maambukizi ya UTI ni chache, zile za kidunia zilizochapishwa katika jarida la Front Public Health mwaka 2022, zinaonyesha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo viliongezeka mara 2.4 katika kipindi cha miaka 29.



Dar es Salaam. Wananchi wanaohitaji kufanya uchunguzi wa awali wa maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) huenda wakapunguza safari za kwenda hospitali na vituo vya afya kufuatia kuanzishwa kwa kifaa maalumu cha kupima ugonjwa huo nyumbani.

Kifaa hicho kinachojulikana kama Checkfor UTI Test, kimeanza kupatikana katika soko la Tanzania kwa lengo la kusaidia utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo unaoathiri mamilioni ya watu duniani.

Akizungumza Dar es Salaam leo Alhamisi, Julai 2, 2026, mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Eshton Nkala amesema kifaa hicho kinatoa fursa kwa watu kupata taarifa za awali kuhusu uwezekano wa kuwa na maambukizi ya UTI, bila kulazimika kwenda hospitali kwa hatua ya mwanzo.

Ingawa takwimu za kitaifa kuhusu kiwango cha maambukizi ya UTI ni chache, zile za kidunia zilizochapishwa katika Jarida la Front Public Health mwaka 2022, zinaonyesha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo viliongezeka mara 2.4 katika kipindi cha miaka 29.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha, watu 4,052,972 walipata maambukizi ya UTI kati ya Julai 2025 hadi Machi 2026.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2019 kulikuwa na matukio milioni 404.61 ya UTI duniani huku watu 236,790 wakifariki kutokana na ugonjwa huo. Watu 520,200 walipata madhara mbalimbali ya kiafya, ikiwemo ulemavu.

Dk Nkala amesema mara nyingi maambukizi ya njia ya mkojo huanza kwa dalili zinazoweza kuonekana kuwa ndogo, ikiwemo kukojoa mara kwa mara, maumivu au hali ya kuungua wakati wa kukojoa, maumivu ya tumbo la chini pamoja na mabadiliko ya rangi au harufu ya mkojo.

Amesema changamoto kubwa katika kudhibiti UTI ni watu kuchelewa kutambua dalili na pia kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

“Wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema ni muhimu katika kupunguza hatari ya maambukizi kuwa makali zaidi, kujirudia mara kwa mara au kusababisha matatizo mengine ya kiafya,” amesema.

Amekielezea kifaa hicho kuwa hakichukui nafasi ya daktari au hospitali, bali ni nyenzo ya kusaidia mtu kuchukua hatua mapema anapoona dalili au anapokuwa na wasiwasi kuhusu afya yake.

“Matokeo ya awali yanaweza kumsaidia mtu kufanya uamuzi sahihi wa kwenda hospitali kupata ushauri wa kitaalamu, kufanyiwa vipimo zaidi na kupata matibabu stahiki,” amesema daktari huyo.

Amesema kifaa hicho kinatengenezwa nchini na kampuni ya Canadian Biotech na kinapatikana kupitia JD Pharmacy, Bariki Pharmacy na Cugra General Supplier.

“Dalili hazipaswi kupuuzwa. Uchunguzi wa mapema na matibabu kwa wakati ni muhimu katika kulinda afya,” amesisitiza.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa afya wametoa tahadhari kuhusu matumizi ya vifaa vya kujipima nyumbani bila usimamizi wa wataalamu.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige amesema hawezi kupendekeza matumizi ya kifaa hicho kama mbadala wa uchunguzi wa hospitalini kwa sababu matokeo yake yanaweza kutafsiriwa vibaya na kusababisha wananchi kufanya uamuzi usio sahihi kuhusu afya zao.

Amesema vipimo vya UTI vina masharti mbalimbali ya kitaalamu, yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kutoa hitimisho.

"Mwanamke aliyeko kwenye hedhi hawezi kupimwa mkojo kwa usahihi kwa sababu damu inaweza kuathiri matokeo. Lazima asubiri amalize hedhi ndipo afanyiwe kipimo," amesema Dk Mzige.

Amesema vipimo vya haraka vinaweza kutoa dalili za awali, lakini haviwezi kubaini aina ya bakteria wanaosababisha maambukizi wala dawa inayoweza kuwaua.

"Kipimo kinachokubalika kuthibitisha UTI ni culture, ambapo mkojo huoteshwa maabara kwa saa 48 hadi 72 ili kubaini bakteria waliopo na dawa zinazoweza kufanya kazi dhidi yao. Hicho ndicho kipimo kinachotoa majibu sahihi zaidi," amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mzige, uchunguzi huo unafanyika katika hospitali za rufaa, hospitali za mikoa na baadhi ya hospitali binafsi zenye maabara maalumu za microbiolojia.

Lakini pia ameonya dhidi ya matumizi holela ya dawa za antibiotiki bila uthibitisho wa maabara, akisema hali hiyo inaweza kusababisha usugu wa dawa na hata kuathiri figo kwa baadhi ya wagonjwa.

"Wapo wagonjwa wanaotibiwa mara kwa mara kwa kudhani wana UTI sugu au malaria sugu bila kufanyiwa uchunguzi wa kina. Matokeo yake wanaendelea kutumia dawa zisizofaa na wakati mwingine hupata madhara makubwa," amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Alex Msoka amesema kwa sasa hakuna mfumo rasmi uliopitishwa unaoruhusu wananchi kujipima UTI nyumbani kama mbadala wa uchunguzi wa hospitalini.

Amesema vipimo vya haraka vya mkojo vimekuwa vikitumika kwenye vituo vya afya na hospitali, lakini vinafanywa chini ya usimamizi wa wataalamu na matokeo yake huthibitishwa kwa vipimo vya ziada pale inapobidi.

"Vipimo vya haraka vina nafasi yake katika uchunguzi wa awali, lakini uwezo wake wa kutoa majibu sahihi hauwezi kulinganishwa na uchunguzi wa maabara unaohusisha culture," amesema.

Dk Msoka amesema hata baada ya mtu kupata majibu yanayoashiria uwepo wa maambukizi, bado mhusika anatakiwa kumuona daktari ili afanyiwe tathmini ya kitaalamu kabla ya kuanza kutumia dawa.

Ameongeza kuwa kama kifaa kitauzwa bila mfumo unaoeleweka wa ushauri na ufuatiliaji wa kitaalamu, kinaweza kusababisha wananchi kujitibu wenyewe na kuchelewa kupata matibabu sahihi.

"Vipimo vya kujipima nyumbani vinaweza kuwa teknolojia nzuri, lakini lazima viende sambamba na elimu sahihi kwa watumiaji na mfumo wa kuwapeleka wagonjwa hospitalini kwa uchunguzi wa kina pale inapohitajika," alisema.

Wataalamu hao wanasisitiza kuwa, licha ya maendeleo ya teknolojia katika uchunguzi wa magonjwa, wananchi wanapaswa kuzingatia kuwa matokeo ya vipimo vya nyumbani ni ya awali na hayapaswi kutumika kama msingi wa kuanza kutumia dawa bila ushauri wa daktari.