Kitanzi cha wezi wa dawa na watumishi wazembe hiki hapa

Dodoma. Matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya afya ni muhimu kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

Kutokana na umuhimu huo, Tanzania nayo haiko nyuma, kwani hivi karibuni kulizinduliwa kituo cha umahiri katika masuala ya afya ya kidijitali kitakachounganishwa na mfumo utakaochangia kuboresha huduma za afya kwa kuongeza ufuatiliaji wagonjwa kuanzia wanapofika hospitali, huduma wanayopatiwa, kupona au kufa kwa ugonjwa gani.

Mfumo huo pia utawawezesha viongozi wakuu wa sekta hiyo (Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu) kupata taarifa ya mrundikano wa wagonjwa hospitalini na ugonjwa upi umeenea katika hospitali husika.


Kuondoa uzembe kupitia simu

Kituo hicho kitaunganishwa na mfumo utakaowasaidia viongozi wakuu wa wizara kuondoa uzembe sehemu za kutolea huduma za afya kutokana na kuona moja kwa moja kwenye mifumo au simu ya mkononi huduma zinazotolewa katika hospitali mbalimbali nchini.

Akizungumzia mfumo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe anasema utasaidia kuondoa uzembe kwa watoa huduma watakaoonekana moja kwa moja kwenye mfumo kutofanya kazi inavyostahili.

“Mfumo huu utakuwa ukikaa ofisini unaona kitu gani kinaendelea kwenye hospitali fulani, unaona wagonjwa wa nje (OPD) wamekaa muda mrefu, inakufanya uchukue hatua za haraka kumuuliza mkurugenzi husika kuna shida gani mbona wagonjwa wamekaa muda mrefu hawapati huduma?

“Hii ni nzuri, kama kuna uzembe inatusaidia kuchukua hatua na kama kuna upungufu pia itasaidia kuchukua hatua kulingana na tunachokiona kuliko kusubiri waandishi wa habari waseme ndipo na sisi tuchukue hatua,” anasema Shekalaghe.


Udhibiti wizi wa dawa, matumizi holela

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Tehama Wizara ya Afya, Silvanus Ilomo anasema kituo hicho pia kitasaidia kudhibiti wizi na matumizi yasiyo sahihi ya dawa katika vituo vya afya na hospitali nchini.

Anasema hatua hiyo inakuja kwa sababu mfumo huo utasaidia kupeleka taarifa moja kwa moja kwenye kituo kuhusu dawa kiasi gani na aina gani imetolewa na Bohari ya Dawa (MSD) na imeenda katika hospitali gani.

“Tunaandaa mfumo ambao dawa inapotoka kuanzia MSD inaonekana mpaka inapofika kwenye kituo, taarifa zake zote na matumizi, kwamba zilipokelewa dawa kadhaa na sasa ametumia kadhaa na zimebaki kadhaa,” anasema Ilomo.

 Aidha, anasema kutokana na taarifa za mgonjwa kuingizwa katika kumbukumbu zao kuanzia awali, itasaidia kubaini aina ya dawa aliyopewa mgonjwa kulingana na ugonjwa anaoumwa ili kuimarisha ufuatiliaji wa huduma za afya hospitalini.

Ilomo anasema kituo hicho kitafanya kazi kuu ya kuimarisha ufanyaji kazi wa mifumo ya afya kwa kuiunganisha pamoja kwa njia ya Tehama, kubadilishana taarifa na data zitakazopatikana mahali pamoja ili kuepuka kurudia tafiti ambazo zimefanywa na wadau wengine.

Pia kituo kitatumika kukuza teknolojia na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo kuhusu Tehama na kuwasaidia kwenye ufanyaji tafiti, kukuza bunifu na maendeleo ya teknolojia.


Taarifa za tafiti

Kituo hicho kinatumika kuhifadhi taarifa zitakazokusanywa kutoka kwa wafanyakazi wa huduma ya afya kwa jamii ambao wanakusanya taarifa kuhusu huduma na kufanya tafiti katika masuala ya jamii ili kuhifadhi au kuzioanisha na sehemu nyingine.

Ilomo anasema uhifadhi wa data unasaidia kuwa na majibu ya pamoja kuhusu utafiti wa magonjwa katika maeneo na kuhifadhi data zitakazoisaidia mamlaka kuchukua hatua.

 Mfumo huo pia utasaidia kukusanya taarifa zinazofanana kutoka kwa wafanyakazi ambapo awali kulikuwa na ukusanyaji na uhifadhi wa data kupitia mifumo mbalimbali kulingana na eneo husika.

Aidha, anasema kuliko kuanzisha mifumo mipya, wizara imejipanga kuunganisha mifumo iliyopo kwenye taasisi za sekta ya afya ili kufanya kazi kwa pamoja na kusomana.


Gharama za ujenzi

Ujenzi wa kituo hicho uliogharimu Sh500 milioni umetokana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wizara hiyo ina mrundikano wa mifumo ambayo haisomani na kusababisha kupungua kwa ufanisi wa kazi.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango Julai 2022 aliiagiza wizara hiyo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika hospitali zake, hasa magonjwa ya kuambukiza na ya mlipuko.


Wananchi wanasemaje?

Akizungumza na Mwananchi, mdau wa masuala ya afya, Dk Paul Kapalango anasema kituo hicho kitasaidia kuondoa changamoto zinazoikumba sekta ya afya, hususan utendaji kazi mbovu unaolalamikiwa na wagonjwa.

“Nimesikia ujio wa kituo hicho, ni kizuri kwa sababu kitakuwa kidijitali zaidi, hapo kwenye kupata taarifa kwa viongozi wakuu ndio kiu yetu, tunataka kuona hatua za haraka zikichukuliwa, kuna changamoto lukuki kwenye sekta hiyo,” anasema Kapalango.

Naye Amina Ombeni anashauri wahudumu watakaobainika kufanya uzembe kupitia mifumo wachukuliwe hatua haraka, lengo likiwa kuboresha utoaji huduma bora kwa wananchi.