Kituo cha afya, gari la wagonjwa vyaimarisha huduma Madaba

Baada ya miaka mingi ya kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hivi karibuni wananchi wa Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma wamepata kituo cha afya.

Licha ya ujenzi wa kituo hicho kilichozinduliwa na Rais John Magufuli alipofanya ziara mikoa ya kusini, wananchi hao wamepata gari la wagonjwa litakalorahisisha usafiri pindi kukiwa na dharura.

Wakazi wa halmashauri hiyo wamesema kituo hicho kitasaidia kuwapunguzia gharama. Mmoja wa wananchi hao, Violeth Mwenda anasema hali ilikuwa mbaya siku za nyuma lakini mabadiliko yatakuwepo sasa.

“Hatukuwa na huduma ya upasuaji ambayo iliwalazimu wajawazito wenye matatizo kusafiri zaidi ya kilomita 100 kwenda Songea, Dar es Salaam au Mbeya. Kilikuwa kipindi kigumu na cha mateso,” anasema Violeth.

Anasema ni faraja sasa huduma hizo kuanza kutolewa katika halmashauri hiyo kwani wataokoa fedha na muda waliolazimika kuutumia kusafiri siku za nyuma.

Mwananchi mwingine wilayani humo, Martha Daniel anasema kuna wakati ndugu au jamaa zao walipoteza maisha kwa kukosa matibabu lakini adha hiyo sasa imepata jawabu.

“Kwa kweli tumeonyeshwa njia. Baada ya kutatua kero hii naamini mwakani tutapata maji. Nayo ni kero inayotuhangaisha,” anasema Martha.

Kwenye ziara yake, Rais Magufuri alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili Watanzania watibiwe kwa wakati hivyo kuimarisha siha zao na kuzalisha zaidi.

Rais alisema ujenzi wa kituo hicho Madaba ni moja kati ya vituo 362 vinavyojengwa nchi nzima na kuwataka watendaji wa Serikali kusimamia fedha za miradi ili kufanikisha malengo yaliyopo.

Alisema ujenzi na uboreshaji wa zahanati, vituo vya afya na hospitali inaendelea maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya nje itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Licha ya kuboresha miundombinu, alisema itaendelea kuajiri watumishi ili watoe huduma za uhakika kwenye vituo hivyo.

Naibu waziri wa Tamisemi, Japhet Kandege anasema kituo hicho kimejengwa kwa Sh665 milioni ambazo kati yake Sh220 milioni zimetumika kununua vifaa na Sh445 milioni kwenye ujenzi .

Kufanikish aujenzi huo, anasemaSh400 milioni zimetoka mfuko wa afya na Sh7.2 milioni zimechangwa na wananchi kukamilisha wodi ya wazazi, chumba cha kuhifadhi maiti, kichomea taka, chumba cha upasuaji pamoja na nyumba ya watumishi.

“Tamisemi imeweka malengo ya kukarabati vituo vya afya 535 ifikapo mwaka 2020,” amesema.

Kwa upande wake , Waziri wa Afya, Ummy Mwalim amesema bajeti ya dawa kwa Mkoa wa Ruvuma imeongezeka kutoka Sh845 milioni hadi Sh3 bilioni ndani ya miaka mitatu iliyopita na kuwataka wananchi kuvitumia vituo vinavyoendelea kujengwa kwa matibabu na chanjo ili kupunguza vifo vinavyozuilika.

“Bajeti hiyo kwa Halmashauri ya Madaba imeongezeka kutoka Sh19.9 milioni hadi Sh95.5 milioni. Hii imesaidia kuongeza idadi ya wanaotibiwa hospitalini,” anasema Ummy.

Ujenzi wa vituo hivyo umesaidia kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungulia hospitalini kwani hivi sasa, wajawazito 82 katika kila 100 wanaenda hospitalini na kwa Madaba ni wanawake 93. Suala hilo limewezesha watoto 91 katika kila 100 kupata chanjo ya pepopunda na kifadulo.

Licha ya afya ya mama na mtoto, juhudi za kukabiliana na maradhi tofauti zimeongezeka na kutoa matokeo chanya. Mwaka 2016 watu 261 walifariki kutokana na malaria mkoani Ruvuma idadi ambayo imepungua mpaka vifo 72 ndani ya miaka mitatu.

Maambukizi ya Ukimwi pia yamepungua kutoka asilimia saba hadi asilimia 5.5 ndani ya kipindi hicho huku idadi ya wanaotumia dawa ikiongezeka.