Kula vyakula hivi wakati wa mfungo kudhibiti unene
Dar es Salaam. Kufunga saumu ni moja ya nguzo tano za Uislamu. Muislamu yeyote mwenye afya njema, akili timamu anatakiwa kushiriki katika saumu kwa kujizuia kula chakula chochote katika kinywa chake, kwa muda wote wa mchana kutwa.
Hata hivyo, wakati waumini wa dini ya Kiislamu wakiingia katika kumi la pili la mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wadau wa afya na lishe wanasisitiza ulaji unaofaa kwa afya ya mwili na akili, huku wakionya matumizi ya sukari na mafuta kwa wingi wakati wa utayarishaji wa futari.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, ulaji wa mafuta na sukari kwa wingi, husababisha mtu kunenepa kupita kiasi na hivyo kuhatarisha afya yake, huku wakishauri namna nzuri ya ulaji unaofaa kipindi hiki cha Ramadhan.
Wanataja mpangilio wa makundi sita ya mlo kamili, ndiyo yanayotakiwa kwa mtu aliyefunga.
Kutokana na umuhimu wa jambo hilo, Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na wataalamu wa lishe kuhusu mambo ya kuzingatia kwa watu waliofunga mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
Mambo ya kuzingatia
Mtafiti na Ofisa Lishe Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC), Gelagister Gwarasa anasema aliyefunga anatakiwa kuzingatia makundi sita ya mlo kamili pamoja kutokuzidisha vyakula vyenye wanga mwilini.
“Mwezi huu wa Ramadhan, waliofunga wanatakiwa kula mlo kamili kutoka katika mchanganyiko wa makundi tofauti tofauti, isipokuwa visizidi vyakula vyenye wanga mwingi na sukari,” anasema.
Anabainisha kuwa wanatakiwa kula vyakula vyenye wanga kiasi, matunda yawepo, mbogamboga ziwepo, lakini zipikwe na mafuta kidogo.
“Watu wakipika futari wasiweke sukari ya kuongeza katika kila chakula kwa sababu sukari inayopatikana katika vyakula vya nafaka, mihogo, viazi, ndizi mbichi na vyakula vya mizizi inatosha, hivyo hakuna sababu ya watu kuongeza sukari katika mlo,” anasema Gwarasa na kuongeza;
“Ulaji huo hautakiwi kwa sababu tunakuwa tunakula sukari nyingi, kuliko mahitaji ya mwili na matokeo yake watu wananenepa sana kwa sababu wanakula vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta,” anasema.
Makundi sita ya mlo kamili
Gwarasa anasema mlo kamili ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote sita ya vyakula na una virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora.
Anasema mlo huo unapoliwa kwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili, huupatia mwili virutubisho vyote muhimu.
Anataja kundi la kwanza ni asili ya nyama, kundi la pili ni la vyakula vya jamii ya kunde na mbegu za mafuta na kundi la tatu ni la mbogamboga.
Kundi la nne ni nafaka, ndizi mbichi, viazi pamoja na mazao ya mizizi, wakati kundi la tano ni matunda na kundi la sita likiwa ni la vyakula mafuta.
“Zamani katika kundi la mafuta tulikuwa tunasema linajumuisha mafuta, sukari na asali, lakini kwa sasa kundi la sukari na asali halipo, bali kuna kundi la mafuta pekee,” anasema Gwarasa.
Anafafanua kuwa sukari na asali vimeondolewa katika makundi hayo sita ya mlo kamili kwa sababu inapatikana katika kundi la kwanza ambalo ni nafaka, ndizi mbichi, viazi na vyakula vya mizizi, mfano ming’oko na mihogo.
“Sukari ikimeng’enywa, asali ikimeng’enywa tunapata glucose, lakini hii glucose tukila vyakula vya kundi la kwanza ambalo ni nafaka, ndizi mbichi, viazi pamoja na mizizi vikimeng’enywa tunakuja kupata glucose.
“Sasa imekuja kuonekana kuwa watu tunakula sukari nyingi, kwa hiyo mahitaji ya sukari na glucose mwilini kwa siku yanafikiwa kupitia vyakula hivyo vya kundi la kwanza na hivyo hatuhitaji nyongeza ya sukari,” anasema Gwarasa na kuongeza;
“Ndiyo maana wataalamu wengi wa masuala ya lishe na afya wanashauri watu wasitumie sukari kwa wingi kwa sababu inapatikana kwenye kundi la nafaka, ndizi mbichi, viazi na mizizi,” anabainisha.
Anafafanua kuwa ndizi mbichi ipo katika kundi la nafaka, lakini ikiiva inapelekwa kwenye kundi la matunda.
Vyakula muhimu kwa aliyefunga
Walbert Mgeni ni Ofisa Mtafiti Mafunzo na Elimu ya Lishe kutoka TFNC, anasema kuwa vyakula vinavyofaa kwa mtu aliyefunga swaumu ni vile vyenye majimaji kama supu kwa sababu husaidia kufanya umeng’enywaji mzuri.
“Mtu ameshinda na njaa siku nzima, hivyo ili kuamsha vimeng’enyo vinavyosagwa na chakula ni vizuri mfungaji akaanza na vyakula laini,” anasema Mgeni na kuongeza;
“Kwa mtu aliyefunga anatakiwa kula vyakula laini kama supu, kwa sababu unapokunywa supu inarudisha maji mwilini, pia husaidia vimeng’enyo vilivyokaa muda mrefu bila kufanya kazi, kuanza kufanya kazi,” anasema Mgeni.
Kuhusu ulaji wa tende kama kianzio wakati wa kufuturu, Mgeni anasema tende ina sifa ya kuwa na nishati kwa wingi kwa sababu ina sukari, hivyo kwa sababu mfungaji ameshinda na njaa na nishati au nguvu imepungua, anatakiwa kula tende kwa kiasi ili apate nishati.
Pia mtu aliyefunga anashauriwa kunywa maji safi na salama, kwani maji yana umuhimu mkubwa kiafya katika kufanikisha kazi mbalimbali mwilini.
Maji husaidia kuzuia uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa kama vile saratani ya tumbo na kibofu cha mkojo pamoja na mawe kwenye figo, hasa yanaponyweka kwa kiasi kinachotakiwa.
Wakati Mgeni akibainisha hayo, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC, Fatma Mwasora naye anasema kipindi hicho, futari ndiyo hutumika wakati wa kufuturu jioni na daku huliwa usiku wakati wa kufunga.
“Futari ni mlo unaotayarishwa katika kipindi chote cha funga ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan na huliwa kijamii kwa maana ya watu hukusanyika pamoja ili kupata mlo huo, ambao hujulikana kwa jina maarufu la kiarabu kama kufuturu,” anasema Mwasora.
Kwa upande wa daku, maana yake ni chakula kinacholiwa usiku wa manane kwa ajili ya kujiandaa kufunga siku inayofuata.
Hivyo, milo ya futari na daku ni muhimu iwe kamili, kwa sababu uwepo wa virutubishi vya nishati lishe kwenye futari na daku husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini.
“Na kwa upande wa virutubishi vya protini ni muhimu kwa sababu husaidia kuujenga mwili na kuimarisha kinga ya mwili. Vilevile madini na vitamini vinahitajika kwa wingi kwenye futari na daku ili kusaidia kuimarisha kinga ya mwili,” anasema Mwasora.
Mwasora anafafanua kuwa ulaji wa kundi moja la nafaka na mizizi huweza kusababisha athari ya kula aina moja tu ya chakula na kupata virutubishi vya aina moja.
“Pia katika kipindi hiki kama vyakula vya asili ya nyama na jamii ya mikunde havitajumuishwa katika milo ya futari na daku ya kila siku, huweza kusababisha upungufu wa virutubishi vya protini mwilini. Vyakula hivi husaidia kujenga mwili na kuimarisha kinga yake,” anafafanua Mwasora.
Namna ya kudhibiti unene
Gwarasa anasema kwa mwezi huu wa Ramadhani, miongoni mwa njia za kudhibiti unene ni watu kujitahidi kupunguza matumizi ya sukari.
“Unaweza kunywa uji lakini haikulazimishi wewe kutumia sukari nyingi, unaweza pia usiweke sukari kwa sababu ule uji uliopika tayari ni sukari na futari uliyopika tayari ina sukari, kwa hiyo watu wazingatie hayo kwa ajili ya afya bora,” anasema.
Kuhusu matunda mtu anatakiwa kula vipi? Anasema aliyefunga anashauriwa kula matunda yasiyo na sukari sana na kiwango cha matunda anayotakiwa kula kwa siku kisipungue saizi ya chungwa moja.
“Ukubwa wa chungwa moja lilivyo ndio saizi ya matunda ambayo mtu aliyefunga anatakiwa kula kwa siku pamoja na mboga mboga,” anabainisha.
Anasema hata tende, mtu anatakiwa kula kwa kiasi, asile kikombe kizima au mfuko mzima.
Anasisitiza pia, watu wale matango, kachumbari kwa sababu hizo ni mboga, lakini waepuke matunda yenye sukari kama ndizi na badala yake wakipata matunda kama matikiti maji kwa sababu ndani yake yana maji.
“Hivyo niwaombe, mwezi huu wa Ramadhan watu waepuke kula vyakula vya wanga kwa wingi, vyakula vyenye sukari nyingi au mapishi yanayotumia mafuta mengi, ni hatari kwa afya zetu, hivyo tujiepushe navyo,” anasema Gwarasa.