Kwa nini hupaswi kuacha mazoezi haya unapoamka?
Muktasari:
- Watu wengi huanza siku zao bila kuupa mwili maandalizi muhimu, hali inayoweza kuathiri utendaji wao wa siku nzima.
Russia. Kuamka ni mwanzo wa siku mpya unaohitaji mwili na akili kuwa katika hali bora ili kukabiliana na majukumu ya kila siku kwa ufanisi.
Hata hivyo, watu wengi huanza siku zao bila kuupa mwili maandalizi muhimu, hali inayoweza kuathiri utendaji wao wa siku nzima.
Njia rahisi na yenye tija ya kujiandaa ni kufanya mazoezi lainishi ya viungo mara tu unapoamka. Mazoezi haya husaidia kuamsha mifumo mbalimbali ya mwili na kuufanya uwe tayari kwa shughuli za siku.
Kwa kuzingatia kanuni za kisayansi za mazoezi, unyooshaji wa viungo huimarisha mwili, huongeza wepesi wa viungo na kuleta utulivu wa akili.
Kwa kawaida, mazoezi ya kunyoosha viungo hulenga sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo misuli, maungio, ngozi, tendoni, ligamenti na mifupa.
Sehemu hizi zina jukumu muhimu la kusaidia mwili kusogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa urahisi. Ili kupata manufaa kamili, mazoezi haya yanapaswa kufanyika kwa utaratibu maalum, yakianzia miguuni na mikononi, kisha kiwiliwili, na hatimaye kichwa pamoja na shingo. Inashauriwa yafanyike kwa dakika tano hadi kumi kila asubuhi.
Faida ya kwanza ya mazoezi haya ni kuondoa uchovu na kuleta utulivu wa kimwili na kiakili.
Msongo wa misuli unapojikusanya husababisha kukakamaa kwa mwili na hata maumivu. Hali hii inaweza kumfanya mtu ajisikie kama mgonjwa. Mazoezi ya kunyoosha viungo husaidia kupunguza shinikizo hilo na kuufanya mwili uwe mwepesi na tayari kwa siku.
Aidha, mazoezi haya husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini. Misuli inapokuwa huru, damu hutiririka kwa urahisi zaidi, hivyo kusambaza virutubisho muhimu katika sehemu mbalimbali za mwili.
Pia, mazoezi haya huchochea utolewaji wa homoni za furaha (endorphins) zinazosaidia kuboresha hali ya hisia na hata kuchangia usingizi mzuri baadaye.
Faida ya pili ni kusaidia kuweka mkao sahihi wa mwili. Kunyoosha misuli iliyokakamaa, hasa katika maeneo ya mgongo wa chini, kifua na mabega, husaidia kuuweka uti wa mgongo katika mpangilio mzuri.
Hii husaidia kupunguza maumivu na uchovu unaoweza kujitokeza kutokana na mkao mbaya.
Tatu, mazoezi lainishi huongeza wepesi wa mwili. Hali hii huufanya mwili uwe tayari kufanya harakati mbalimbali kama kutembea, kukimbia au hata kuruka bila shida.
Mwili unapokuwa mwepesi, hupunguza hatari ya kupata majeraha wakati wa shughuli za kila siku.
Nne, mazoezi haya huongeza ustahimilivu na uimara wa misuli. Misuli inapofanya kazi vizuri, hutumia sukari mwilini kwa ufanisi zaidi na kusaidia kuchelewesha uchovu. Hivyo, mtu huanza siku akiwa na nguvu na ari zaidi.
Faida ya tano ni kupunguza uwezekano wa majeraha. Mazoezi haya huifanya misuli kupokea damu na virutubisho kwa wingi, hali inayosaidia kuzuia na kuponya haraka majeraha madogo ya misuli yanayotokana na shughuli mbalimbali kama kunyanyua vitu au kufanya kazi za mikono.
Sita, mazoezi haya huongeza hali ya kujiamini na furaha. Kufanya mazoezi asubuhi huleta burudani na kuandaa akili katika hali chanya, jambo linaloweza kuboresha utendaji kazini au shuleni.
Saba, hujenga nidhamu binafsi. Unapozoea kufanya mazoezi haya kila siku, huwa sehemu ya maisha yako. Nidhamu hii hukuwezesha kuendelea kupata faida zake za kiafya kwa muda mrefu.
Kwa kuongeza, matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kuboresha utekelezaji wa mazoezi haya.
Kupitia simu janja, unaweza kupakua programu mbalimbali zinazokuongoza hatua kwa hatua katika kufanya mazoezi sahihi. Kwa ujumla, mazoezi lainishi ya viungo ni rahisi, hayahitaji gharama wala vifaa maalum, na yanaweza kufanyika popote ulipo.
Kwa matokeo bora zaidi, unaweza kuyaambatanisha na muziki ili kuongeza hamasa na kuboresha hali ya akili. Kuanza siku kwa mazoezi haya ni uwekezaji mdogo wenye faida kubwa kwa afya ya mwili na akili.