Maambukizi mapya ya VVU duniani yashuka kwa asilimia 65
Muktasari:
- Ripoti hiyo ya awali iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Ukimwi (UNAIDS) inaonyesha takribani watu milioni tano duniani bado hawajui kuwa wanaishi na VVU, hali inayotajwa kuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kudhibiti maambukizi mapya.
Dar es Salaam. Idadi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) duniani imepungua kwa asilimia 65 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, huku watu wanaoishi na maambukizi hayo wakifikia milioni 40.9 mwaka 2025, takwimu mpya za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Ukimwi (UNAIDS) zinaonyesha.
Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya UNAIDS iliyotolewa katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu VVU na Ukimwi Juni 12, 2026, watu milioni 1.2 walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2025, ikilinganishwa na watu milioni 3.5 walioambukizwa mwaka 1995, mwaka ambao ulirekodi kiwango cha juu zaidi cha maambukizi mapya duniani.
Ripoti hiyo inaonyesha licha ya mafanikio hayo, watu 570,000 walifariki dunia kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi mwaka 2025, sawa na mtu mmoja kufariki kila dakika kutokana na sababu zinazohusiana na VVU.
“Kati ya watu milioni 40.9 wanaoishi na VVU duniani, milioni 39.7 ni watu wazima wenye umri wa miaka 15 na zaidi, huku watoto milioni 1.3 wenye umri wa miaka 0 hadi 14 wakiendelea kuishi na maambukizi hayo. Wanawake na wasichana wanawakilisha asilimia 51 ya watu wote wanaoishi na VVU duniani,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo alipotafutwa kutaka kufahamu nafasi ya Tanzania katika ripoti hiyo, Ofisa Mahusiano wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NASHCoP), Shoko Subira amesema:“Kwa sasa ripoti hii si ya mwisho ilitolewa kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya juu iliyofanyika hivi karibuni haijasainiwa. Itakuwa na marekebisho baadaye Julai na ripoti kamili itatolewa Novemba mwaka huu.”
Kwa upande wa matibabu, imeonyesha watu milioni 32.1 walikuwa wanapata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs) kufikia mwisho wa mwaka 2025, ikilinganishwa na milioni 7.7 mwaka 2010. Hii ina maana kuwa asilimia 78 ya watu wote wanaoishi na VVU duniani walikuwa wanapata matibabu.
Ripoti hiyo pia inaonyesha wanawake wanaongoza kwa upatikanaji wa huduma za matibabu, ambapo asilimia 84 ya wanawake wanaoishi na VVU walikuwa wanapata ARVs mwaka 2025, dhidi ya asilimia 74 ya wanaume.
Kwa wanawake wajawazito wanaoishi na VVU, asilimia 87 walipata dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hatua hiyo imechangia kupungua kwa maambukizi mapya kwa watoto kwa asilimia 69 tangu mwaka 2010, kutoka watoto 300,000 hadi 94,000 mwaka 2025.
Katika kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95, UNAIDS imeeleza kuwa asilimia 88 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wanajua hali zao mwaka 2025. Kati yao, asilimia 89 walikuwa wanapata matibabu na asilimia 95 ya waliokuwa kwenye matibabu walikuwa wamefikia kiwango cha kudhibiti virusi mwilini.
Hata hivyo, changamoto bado zinaendelea kuwepo. Takribani watu milioni tano duniani bado hawajui kuwa wanaishi na VVU, hali inayotajwa kuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kudhibiti maambukizi mapya.
Ripoti hiyo imebainisha makundi maalumu yanaendelea katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU kutokana na unyanyapaa, ubaguzi na vikwazo vya kisheria vinavyowazuia kupata huduma za afya. Watu wanaojidunga dawa za kulevya wako katika hatari mara 34 zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko watu wengine wazima, huku wafanyakazi wa ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao na wanawake waliobadili jinsia wakiwa katika hatari mara 17 hadi 18 zaidi.
Wakati huohuo, Tanzania Kwa mujibu wa takwimu hizo (THIS 2022/23) kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka miongoni mwa watu wazima wenye umri wa miaka 15 na zaidi kilikuwa asilimia 0.18, sawa na takribani watu 60,000 kila mwaka. Kiwango hicho kilikuwa asilimia 0.24 kwa wanawake na asilimia 0.11 kwa wanaume.
Kiwango cha maambukizi ya VVU katika jamii miongoni mwa watu wazima nchini Tanzania kilikuwa asilimia 4.4, sawa na takribani watu wazima 1,548,000 wanaoishi na VVU. Maambukizi yalikuwa juu zaidi kwa wanawake (asilimia 5.6) kuliko kwa wanaume (asilimia 3.0).