Manufaa ya kupunguza ulaji sukari kiafya
Ulaji wa sukari umekuwa sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, lakini ni muhimu kuzingatia madhara yake kiafya na umuhimu wa kupunguza kiwango tunachokitumia.
Sukari, hasa ile iliyosindikwa, inaweza kuwa na athari mbaya kwa afya zetu, kama vile kuongezeka kwa hatari ya kupata kisukari, unene kupita kiasi na magonjwa mengine ya moyo.
Sukari huwa na kiwango kikubwa cha kalori ambazo hazina virutubishi vya muhimu kwa miili yetu. Mara nyingi, vyakula vilivyo na sukari nyingi kama vile vinywaji vyenye gesi, pipi na vyakula vingine vyenye asili ya sukari na vya viwandani hutoa kalori nyingi ambazo hazina manufaa kwa mwili wetu.
Hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa uzito na hatari ya kupata aina ya pili ya ugonjwa wa kisukari.
Pili, ulaji wa sukari unaweza kusababisha kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya moyo. Utafiti uliowahi kufanywa mwaka 2013 na taasisi ya American Journal of Clinical Nutrition unaonyesha kuwa watu wanaokula sukari nyingi wana hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya moyo kuliko wale wanaopunguza ulaji wao. Hii ni kwa sababu sukari inaweza kusababisha mabadiliko ya kemikali mwilini, ambayo husababisha kuziba kwa mishipa ya damu na hatimaye kusababisha matatizo ya moyo.
Kupunguza ulaji wa sukari pia kunaweza kuboresha afya ya meno. Bakteria kinywani hupenda kula sukari na hivyo kuunda asidi ambayo inaweza kusababisha kuoza kwa meno na magonjwa ya kinywa.
Kwa kupunguza ulaji wa sukari, tunaweza kudumisha meno yetu na afya nzuri ya kinywa.
Athari kwa vyakula vyenye sukari ni nyingi, inaweza kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari, kusababisha ugonjwa wa moyo, pia inaweza kuathiri viwango vya lehemu au kitaalamu cholesterol.
Mbali na athari hizi za moja kwa moja kwa afya, kupunguza ulaji wa sukari kunaweza kusaidia kuboresha maisha kwa ujumla. Kuwa na lishe bora na kupunguza matumizi ya sukari kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya muda mrefu na hivyo kuboresha afya.
Kupunguza ulaji wa sukari kunaweza kuwa changamoto kwa watu wengi kutokana na utamu wake uliozoeleka na upatikanaji wake rahisi katika vyakula vya kisasa.
Hata hivyo, hatua ndogo ndogo kama vile kuchagua vinywaji visivyotumia sukari au kula matunda badala ya juisi za viwandani, kunaweza kusaidia kupunguza ulaji wa sukari.
Kuepukana na magonjwa ya moyo, matatizo ya figo, kisukari aina ya pili na unene kupita kiasi, pamoja na kuboresha afya ya meno na viwango vya nishati ni lazima kupunguza na kuacha matumizi ya sukari na vyakula pamoja na vinywaji vyenye sukari.