Unayopaswa kufahamu kuhusu sukari mwilini

Muktasari:

Sukari ina umuhimu mwilini, lakini haipaswi kuliwa bila mpangilio, ili kuepuka madhara yanayotokana na matumizi holela.

Sukari ina umuhimu mwilini, lakini haipaswi kuliwa bila mpangilio, ili kuepuka madhara yanayotokana na matumizi holela.

Pia ni muhimu kuzingatia ubora na kiwango kinachohitajika mwilini, kwani kuna sukari yenye madhara mwilini na mojawapo ni sukari nyeupe.

Sukari inatumika kama kiungo kwenye uji, chai au wakati wa kutengeneza juisi nyumbani. Pia sukari hutumika wakati wa kutengeneza vinywaji viwandani kama soda, juisi na bia.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanashauri hakuna ulazima kwa binadamu kutumia sukari kwa kuwa vyakula anavyokula vinazalisha kiasi kikubwa cha sukari mwilini.

Pombe kama bia zina kiwango kikubwa cha sukari hivyo husababisha udhibiti wa sukari mwilini kuwa mgumu, lakini pombe kali ni hatari pia kwa kuwa husababisha athari kwa viungo vya mwili kama figo na ini ambavyo pia huathiriwa na ugonjwa wa kisukari.

Katika mahojiano maalumu na Jarida la Afya, wataalamu wamesema binadamu anatakiwa kula vijiko vitano vya sukari kwa siku ambavyo vingi huzalishwa kupitia chakula.

Imeelezwa kuwa baadhi ya vyakula vina sukari iliyozidi, mfano soda yenye ujazo wa mil 350 ina sukari vijiko 10.

Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Theresia Thomas anasema kazi ya sukari ni kuupa nguvu mwili, kazi ambayo inafanywa na vyakula vingi ambavyo huliwa na binadamu.

“Sukari ya kutengenezwa viwandani si kitu cha muhimu kwa binadamu kwa sababu vyakula vingi vinampatia sukari moja kwa moja.

“Vyakula vya wanga vikivunjwavunjwa vinatoa sukari na ikizidi inahifadhiwa kama mafuta mwilini na tunashauri mtu anayeweza kuacha matumizi ya sukari ni vizuri, kwani sio kama chumvi ambayo yenyewe ina madini muhimu yanayohitajika mwilini na haina mbadala,” anasema.

Anayataja baadhi ya madhara ya sukari ni kusababisha meno kuoza na kuongeza sukari ya ziada mwilini.

“Tunapata nguvu kupitia chakula kama ugali, viazi, mihogo, ubwabwa. Sasa unapokula kimojawapo hapo na chai yenye sukari nyingi unakosea, kwani vyote vinaleta kirutubisho kimoja, kumbuka sukari hugeuka mafuta na ikizidi inafanya usugu wa kichocheo cha insulin na mwisho mtu anapata kisukari,” anasema.


Sukari huunguza mwili

Kadri mtu anavyokula vyakula vyenye sukari kwa wingi au vinavyozalisha nguvu kwa wingi, viungo vyake huchomwa taratibu.

Mwenyekiti wa chama cha wagonjwa wa kisukari nchini, Profesa Andrew Swai anasema ni lazima sukari ipatikane mwilini, ili ubongo, maini, figo, mapafu vifanye kazi, lakini akaonya vikizidi huleta madhara.

Profesa Swai ambaye pia ni Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya magonjwa yasiyoambukiza anasema, “Kitaalamu sukari inatakiwa kuja kidogokidogo kadiri inavyohitajika, mfano ukichoma nyama ukazidisha moto nyama inaungua, ndivyo hata mwilini nguvu na hewa vikizidi ile nguvu ya ziada huchoma mwili, ndiyo maana wenye kisukari hupofuka macho, hupata hitilafu kwenye mishipa ya fahamu, figo, mishipa ya damu.”

Anasema mwili hauna uwezo wa kuizuia sukari ikishakutana na hewa lazima itengeneze nguvu.

“Ikiwa hii nguvu haihitajiki kutumika itakuchoma, ukianza kula vyakula hivyo utotoni ukifika miaka 30 umeshapata kisukari,” anasema.

Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Valeria Millinga anasema sukari nyingi ikifyonzwa kwenye damu kusababisha kuharibu na kuziba mishipa ya damu na pia kusababisha kiharusi au stroke.

“Ulaji wa sukari nyingi husababisha kongosho kutoa homoni nyingi ya Insulini kwa ajili ya kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu na endapo kongosho inazidiwa kwa kufanya kazi ya ziada huchoka haraka na kuua seli (beta cells) na kushindwa kudhibiti kiwango cha wingi wa sukari kwenye damu na hivyo kusababisha mtu kupata kisukari,” anasema.


Chanzo cha saratani

Profesa Swai anashauri watu kula matunda halisi bila kuyasaga, ili tumbo lipate zile nyuzinyuzi, kwani yanaposagwa ukinywa ile sukari yake inakwenda moja kwa moja mwilini.

“Vyakula vya wanga vikiingia mwilini vinameng’enywa na kuwa sukari, kwenye mahindi kuna maganda, tunapoyakoboa tunaharibu, maganda yanatusaidia kupata choo. Tukikoboa sana vyakula huzalisha zaidi sukari na ndiyo sababu ya saratani,” anasema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Crispin Kahesa anasema sukari imeonekana ndiyo chanzo kikubwa cha unene uliokithiri.

Anasema ulaji wa vitu vyenye sukari humfanya mtu awe mnene kupita kiasi, hali inayomuweka hatarini kupata saratani.

“Sukari huchangia kuhifadhi mafuta mwilini na kuleta unene uliokithiri ambao ni vitu vinavyochangia saratani nyingi zinazojitokeza sasa hivi ambazo ni zile zinazotokana na mtindo mbaya wa maisha, ikiwemo ulaji mbaya wa chakula,” anasema Dk Kahesa.


Sukari ya viwandani, nyumbani

Profesa Swai anasema sukari inayotumika majumbani imeshachakatwa na kusafishwa kwa ajili ya matumizi, tofauti na ile ya viwandani ambayo hutayarishwa maalumu kwa ajili ya kutumika katika kuzalishia bidhaa mbalimbali, ikiwemo vinywaji, vyakula na dawa.

“Sukari zote zina athari sawasawa, isipokuwa ile iliyochakatwa kiwandani na kutengenezwa kitu kingine huwa na nguvu zaidi ikilinganishwa na ile ya majumbani kutokana na kuongezwa baadhi ya kemikali.

“Sukari ya viandani ukiitumia moja kwa moja ina athari zaidi, ijapokuwa hata ya nyumbani athari zipo,” anasema.


Kuepuka kisukari

Wataalamu wanasema mtu anapokula vyakula vinavyoongeza sukari kwa wingi mwilini ni lazima ahakikishe anafanya mazoezi.

“Unapofanya mazoezi mafuta yanajichoma yenyewe mwilini na unabaki ukiwa na yale yanayohitajika kwa wakati huo. Usipofanya hivyo mafuta yatabaki mwilini na kuleta athari,” anasema Profesa Swai.

Anasema bila umakini sehemu ya kongosho, ini, mapafu huanza huathirika, hivyo ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi.

Tafiti

Utafiti uliofanywa na shirika la kimataifa la kutetea maslahi ya wazee HelpAge, umeonyesha wazee wenye zaidi ya miaka 50 ndio wanaoathirika zaidi, hasa wale wanaoishi vijijijini kwa kuwa hawana uhakika wa vipimo wala matibabu.

Utafiti ulionyesha asilimia 87 hawajawahi kupimwa sukari kwenye damu na wala hawana uwezekano wa kufikiwa kwa vipimo, uhakika wa kipato na hawana afya nzuri.

“Utafiti umebaini wazee wanaishi maeneo ya vijijini ambako hakuna huduma za afya ikiwemo upimaji na uhakika wa matibabu, wazee vijijini na wale wasio na elimu upimaji wa magonjwa kama kisukari ni hafifu kwao.

“Asilimia 92.8 ya wazee vijijini hawakuwahi kupimwa kisukari, asilimia 68.8 ya waishio mijini hawakuwahi kupimwa kabisa magonjwa hayo,” ulieleza utafiti huo.


Matibabu

Wataalamu wanasema mtu anapopata kisukari huwa na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu kuliko kawaida na wengi hupata kisukari aina ya pili ambayo ndiyo aina inayowapata takriban asilimia 90 hadi 95 za wagonjwa wote.

Olivia Mushi (61) ameishi na ugonjwa wa kisukari kwa takribani miaka 26 sasa, anaiomba Serikali iangalie namna itakavyotatua suala la baadhi ya dawa kutopatikana kwa wagonjwa wenye bima na gharama za dawa husika.

“Serikali itusaidie kwenye bima ya afya, unakuta bima haiwezi kukupatia sindano kama frees pain ambayo moja ni Sh40,000 ijapokuwa kawaida ni Sh15,000. Unakuta sindano haipo kwenye bima na kwa mwezi ninatakiwa kununua dozi tano. Ninachoma asubuhi na usiku, mchana ni kula vidonge,” anasema.

Anashauri suala hilo lipewe kipaumbele, kwani hata katika tiba za mazoezi hazijawekwa katika orodha ya huduma zinazotumiwa na bima za afya, ikiwemo vipimo vya MRI na CT Scan.