Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 20 ya Mtei akihudumu wodi ya wagonjwa wa akili

Muktasari:

  • Mtei alianza kazi ya uuguzi mwaka 2007 akiwa muuguzi msaidizi na hajawahi kuhamia eneo jingine tangu hapo.

Dar es Salaam. Miaka 20 ya kufanya kazi katika wodi ya wagonjwa wa afya ya akili si jambo dogo. Wengi huiogopa sehemu hii kwa harufu ya dawa, milango inayofungwa kwa kufuli, na sauti za wagonjwa wanaozungumza peke yao au wanaoomba msaada.

Hii ni hali ya kawaida kwa wauguzi wanaohudumu katika mazingira haya, lakini kwa Peter Mtei, sehemu hii ni nyumbani, na wagonjwa ni kama familia yake ya pili.

Mtei alianza kazi ya uuguzi mwaka 2007 akiwa muuguzi msaidizi na hajawahi kuhamia eneo jingine tangu hapo.

Anasema alipata hamasa ya kufanya kazi kwenye wodi ya afya ya akili alipofanya ziara ya kimasomo katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ambapo aliguswa na hali ya wagonjwa waliokuwa hawapewi kipaumbele na jamii.

Anakumbuka kuwa mwanzoni alikutana na changamoto nyingi ambazo hakuzitarajia alipokuwa chuoni. Kwa muda alihisi woga, hadi kufikia hatua ya kuogopa kwenda kazini, lakini elimu aliyokuwa nayo ilimsaidia kukabiliana na hali hiyo na hatimaye akaizoea kazi hiyo.

Aliendelea kujisomea na kupata shahada katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), na kupanda ngazi hadi kuwa Ofisa Muuguzi Mwandamizi na sasa ni Meneja wa Jengo la Afya na Magonjwa ya Akili.

Miaka 20 ya uuguzi wodi ya wagonjwa wa akili

Katika kipindi chote cha kazi yake, Mtei anakumbuka matukio mengi, yakiwemo ya wauguzi kuumia wanapowahudumia wagonjwa, hasa wakati wa kuwapa dawa.

“Katika ile hali ya purukushani kumsaidia mgonjwa na kumpa dawa, wapo wauguzi wanaumia mkono, kidole au wanateguka mkono,’’ anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa wauguzi hupatiwa mafunzo ya jinsi ya kujilinda wanaposhughulika na wagonjwa, ikiwemo kutowaruhusu wagonjwa kukaa nyuma yao.

Anasema jukumu lao kubwa ni kuhakikisha mgonjwa anapata huduma pindi anapoingia wodini. Hushirikiana na ndugu wa mgonjwa kumdhibiti awali, na dawa ya mwanzo hutolewa kwa njia ya mshipa.

‘’Endapo mgonjwa ni hatarishi, hufungwa kwa kamba maalumu zisizomuumiza ili aweze kulala kwa uangalizi. Baadaye huendelea na dozi za matibabu, na kama hali yake itaendelea kuwa shwari, hupelekwa wodi nyingine kwa uangalizi wa kawaida,’’ anaeleza.

Mtei anasema wapo wagonjwa wanaotibiwa katika chumba maalumu cha uangalizi mkali (ICU) kwa saa 24 kabla ya kuhamishiwa wodi kubwa kulingana na hali yao.

Ndugu huruhusiwa kuwaona wagonjwa wao wakiwa nje, hasa kama bado ni hatarishi, lakini baadaye hupewa nafasi ya kushiriki nao kwa karibu zaidi wanapoanza kuonyesha mabadiliko.

Anasimulia tukio la kipekee la mwaka 2014, alipopewa mgonjwa kijana mwenye umri wa miaka 16 aliyekuwa na sonona kali kwa zaidi ya miezi minne. Mgonjwa huyo alikuwa kimya kabisa, lakini siku moja alitabasamu wakati akimhudumia.

Tukio hilo lilimpa matumaini makubwa. Baadaye kijana huyo alipona, akarudi shule, akahitimu kidato cha sita na baadaye chuo kikuu. Siku ya mahafali yake, alimwalika na mbele ya umati akamshukuru kwa kumpa tumaini kupitia tabasamu lake.

Tukio hilo lilimfundisha kuwa wakati mwingine huduma ndogo, kama tabasamu, inaweza kuwa daraja la maisha kwa mtu mwingine.

Kwa sasa, Mtei anajivunia kuwaona wagonjwa wengi aliowahudumia wakiwa wamepona na kusonga mbele katika maisha yao. Wapo waliorejea kazini, shuleni au vyuoni na wanafanya vizuri.

Anasema kazi hiyo imemfundisha kuwa changamoto ya afya ya akili inaweza kumpata mtu yeyote, bila kujali nafasi yake katika jamii.

’Nimegundua hii changamoto inaweza kumpata mtu yeyote, mdau yeyote na sababu ni nyingi imekua kama shule kwangu, najivunia sijawahi kujilaumu kufanya kazi eneo hili,’’ anasema.

Changamoto

Anakiri kuwa kazi hiyo ina changamoto nyingi. Wakati mwingine, wauguzi hujikuta wakihudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja, hali inayoweza kusababisha kuumia au kutukanwa. Hata hivyo, wengi wao huchukulia kuwa ni sehemu ya kazi yao.

‘’Kuna ndugu wanaoleta wagonjwa hospitalini kisha kuwatelekeza. Wapo pia wanaochelewesha matibabu kwa kuamini kuwa wagonjwa wamelogwa au wana matatizo ya kichawi,’’ anaeleza na kusisitiza ushirikiano kati ya wauguzi na ndugu wa wagonjwa.

Anasema matibabu huenda kwa kasi endapo mgonjwa atawasilishwa mapema. Wakati mwingine, ndugu hushindwa kutoa ridhaa ya matibabu, wakiamini mgonjwa atatulia. Wengine anasema hukataa kuruhusu matumizi ya dawa za hospitali wakiamini zaidi tiba mbadala, jambo ambalo huhatarisha afya ya mgonjwa.

Licha ya changamoto hizo, Mtei anaamini kuwa mafunzo endelevu kwa wauguzi wa afya ya akili ni muhimu, na ni vyema  Tanzania ikajifunza kutoka kwa mataifa mengine,  ili kuboresha huduma na kupunguza madhara yanayoweza kuwakumba wauguzi.

Anasema kwa miaka 20 aliyoifanya kazini, ameona mabadiliko makubwa. Serikali imefanya juhudi mbalimbali, hasa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo sasa kuna wodi zaidi, vitanda vimeongezeka kutoka 12 hadi 66, na elimu kwa ndugu wa wagonjwa imeimarika.

Pia dawa zinapatikana kwa kiasi kikubwa na wataalamu wanaendelea kuzalishwa, jambo linaloongeza ufanisi wa huduma.

Hata hivyo, anaona idadi ya wagonjwa wa afya ya akili inaendelea kuongezeka, hali inayoonyesha kuwa bado kuna haja ya kuimarisha zaidi huduma, elimu kwa jamii, na ushirikiano wa karibu katika kushughulikia changamoto hizo.