Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mirembe yataja maeneo kuongeza nguvu kudhibiti matatizo ya afya ya akili

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Upatikanaji wa Huduma ya Afya ya Akili Wakati wa Majanga na Dharura,” ikilenga kuhamasisha jamii na taasisi za afya kuwekeza zaidi katika huduma za afya ya akili.

Manyara. Ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia, ulevi uliokithiri na matumizi ya dawa za kulevya ni miongoni mwa sababu zinazoufanya mkoa wa Manyara kuwa na ongezeko la watu wenye matatizo ya afya ya akili.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Paul Lawala wakati wa maadhimisho ya Siku ya afya ya akili ambapo timu ya watalaamu wa hospitali hiyo waliweka kambi wilayani Babati mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Dk Lawala takwimu za kitengo cha tafiti na mafunzo cha hospitali Mirembe zinaonyesha kuwa mkoa wa Manyara unaongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa uraibu wanaopokelewa katika vituo vya afya.

Dk Lawala amesema maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika mkoani Manyara kutokana na historia ya majanga yaliyotokea hivi karibuni katika wilaya ya Hanang, ambayo yaliacha athari kubwa kwa afya ya akili ya wakazi wake.

“Tumechagua kufanya maadhimisho haya mkoani Manyara kwa sababu mkoa huu umekumbwa na matukio kadhaa ya majanga na dharura, ikiwemo maafa ya Hanang. Athari kama hizi huacha majeraha makubwa ya kiakili, hivyo tunahakikisha jamii inapata elimu, huduma na msaada wa kitaalamu wa afya ya akili,” amesema Dk Lawala.

Amesema lengo la kuweka kambi ya matibabu Babati ni kutokana na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia, ulevi uliokithiri na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wananchi wa mkoa huo, hali inayochangia ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili wanaohitaji huduma maalumu.

Dk Lawala amesema timu iliyofika Manyara inajumuisha madaktari bingwa wabobezi wa afya ya akili, wanasaikolojia, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa ustawi wa jamii na tiba kazi, ambao watakuwa Babati kwa siku tatu kutoa huduma bure za matibabu, ushauri nasihi na mafunzo kwa watoa huduma kutoka sekta mbalimbali.

“Makundi yatakayopokea mafunzo ni pamoja na watoa huduma wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, askari polisi, na watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Tunataka kila mtoa huduma awe na uelewa wa namna ya kutoa msaada wa awali wa afya ya akili, hasa wakati wa majanga,” alisema.

Aidha, Dk. Lawala aliiomba Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Mirembe katika kuimarisha huduma za afya ya akili nchini.

“Tunaomba serikali iendelee kushirikiana nasi katika kutoa elimu na mafunzo kwa jamii. Gharama kubwa za matibabu ya magonjwa ya akili zimekuwa kikwazo kikubwa kwa Watanzania wengi kupata huduma hizi. Tunashauri serikali kurasimisha kifungu maalum cha bima ya afya kwa matibabu ya akili ili Watanzania wote waweze kupata huduma hizi muhimu bila ubaguzi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameipongeza Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kwa kuandaa kambi hiyo muhimu ya huduma na elimu ya afya ya akili.

Sendiga amesema maadhimisho hayo yamekuja wakati muafaka, hasa baada ya mkoa huo kukumbwa na maafa ya Hanang ambayo yaliathiri kwa kiasi kikubwa afya ya kiakili ya wakazi.


“Kaulimbiu ya mwaka huu inagusisha moja kwa moja maisha yetu kama Watanzania. Baada ya maafa ya Hanang, wananchi wengi walipoteza wapendwa, makazi na mali, hali iliyoathiri afya yao ya akili. Hivyo, ujio wa Hospitali ya Mirembe ni faraja kwa wananchi wa Manyara,” amesema.

Sendiga amesema tatizo la afya ya akili linazidi kuongezeka kutokana na changamoto za kijamii, kiuchumi na ukatili wa kijinsia huku akieleza kuwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya wanaume.

 “Zamani tulizoea kuona wanawake wakiwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, lakini sasa hali imebadilika. Wanaume nao wameanza kuwa wahanga, na tayari kuna chama cha wanaume wanaopitia ukatili kutoka kwa wenza wao. Hii inaonyesha umuhimu wa elimu ya afya ya akili kwa jamii nzima bila kujali jinsia,” amesema

Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Mirembe katika kuhakikisha huduma za afya ya akili zinaboreshwa mkoani Manyara, akisisitiza kwamba ujio huo hautabaki kuwa wa mara moja pekee.

“Kwa niaba ya serikali, ninaahidi kuwa huu si ujio wa mwisho. Tutahakikisha watoa huduma wote wa afya mkoani Manyara wanapata mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Mirembe. Tunataka kila hospitali, kila kituo cha afya kiwe na mtaalamu anayeweza kutoa huduma ya awali ya afya ya akili,” alisema.

Maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa rasmi wa kambi ya matibabu na mafunzo ya afya ya akili yatakayodumu kwa siku tatu wilayani Babati.

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu, ushauri nasihi na elimu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili bila malipo.

Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani hufanyika kila mwaka Oktoba 10 duniani kote, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya akili na kuchochea hatua za kitaifa na kimataifa za kuboresha huduma, sera na uelewa wa jamii kuhusu changamoto zinazohusiana na afya ya akili.