Nguvu ya limao kwa afya ya wenye kisukari

Muktasari:

Kwa kuwa limao ina kiasi kingi cha vitamini C, husaidia kutibu na kutuliza matatizo ya muda mrefu kwenye mfumo wa upumuaji.

Baadhi ya watu wanaamini ugonjwa wa kisukari ni wa kitajiri na una masharti na makatazo mengi, hivyo kuwafanya wagonjwa wawe waoga kula au kutumia aina fulani ya vyakula, vinywaji au viungo kama malimao.

Malimao mbali na kuwa kiungo katika mboga na mambo mengine, linatumika kama dawa na husaidia kuongeza kinga ya mwili, kusafisha tumbo pamoja na kusafisha damu.

Wataalamu wa tiba asili wanasema limao lina uwezo mkubwa wa kusaidia na kuondoa mchanga katika figo, kupunguza kukamaa kwa mishipa (strokes) na kupunguza joto la mwili. Kama kinywaji ambacho huondoa uchovu mwilini.

Wagonjwa wengi wa kisukari wanapata shida ya kukosa choo, hivyo juisi ya limao husaidia kutibu matatizo yahusianayo na tumbo kushindwa kumeng’enya chakula na kufunga choo. Ongeza matone machache ya limao kwenye chakula chako au kwenye kifungua kinywa na itakusaidia katika kumeng’enya chakula.

Wanaopata homa za mara kwa mara hasa nyakati za asubuhi, matumizi ya limao kwenye maji ya kunywa inasaidia kuweka mwili sawa. Pia hutibu mafua au baridi.

Unene uliopitiliza ni moja ya sababu ya kupata kisukari aina ya pili. Limao husaidia kunyonya mafuta mwilini na hupunguza uzito. Pia wenye matatizo kwenye mfumo wa upumuaji kama pumu, juisi ya limao husaidia kutuliza matatizo hayo.

Kwa kuwa limao ina kiasi kingi cha vitamini C, husaidia kutibu na kutuliza matatizo ya muda mrefu kwenye mfumo wa upumuaji.

Ugonjwa wa kisukari kwa kiasi kikubwa huharibu afya ya kinywa na meno, hivyo matumizi ya limao au jusi yake huongeza afya ya meno. Ikiwa juisi halisi ya limao ikinyunyiziwa juu ya jino linalouma inasaidia kuondoa maumivu. Kusugua (masaji) juisi ya limau juu ya fizi za meno kunaweza kusaidia watu wenye matatizo ya kutokwa damu kwenye fizi huku ikiondoa harufu mbaya katika fizi na mdomo kwa ujumla.

Kwa wenye matatizo ya shinikizo la damu, moyo wanaweza kutumia limao au juisi ya limao kuna msaada mkubwa. Mara nyingi limao imetumika kwa watu wenye mfadhaiko wa akili na majonzi. Faida tajwa za limao au juisi ya limao zisimfanye mgonjwa wa kisukari aache kutumia dawa zake.

Mwandishi Lucy Johnbosco ni mshauri wa wagonjwa wa kisukari