Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu ongezeko matumizi dawa za PEP

Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) zinaonyesha kuwa Tanzania hupata takribani maambukizi mapya 60,000 ya VVU kila mwaka.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema, ongezeko la matumizi ya dawa za dharura za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) (Wataalamu wa afya wamesema, ongezeko la matumizi ya dawa za dharura za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) (PEP) nchini, ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu huduma hiyo na ongezeko la watu wanaojiweka kwenye mazingira ya hatari ya kuambukizwa VVU. 

Kauli hiyo imekuja baada ya Ripoti ya Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi ya VVU (2021–2025) kuonyesha idadi ya watu walioripoti kuwa katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo imeongezeka kutoka 1,465 mwaka 2021 hadi 4,128 mwaka 2025.

Katika kipindi hicho, idadi ya waliopatiwa dawa za PEP imeongezeka kutoka 1,457 hadi 3,918.

PEP ni dawa za dharura zinazotolewa kwa mtu aliyekuwa katika mazingira yanayoweza kumweka kwenye hatari ya kuambukizwa VVU, mfano aliyebakwa na zinapaswa kuanza kutumika ndani ya saa 72 baada ya tukio la hatari.

Mtaalamu wa afya kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) jina limehifadhiwa, amesema ongezeko la matumizi ya PEP lina tafsiri mbili kuu.

"Kwanza, linaonyesha wananchi wengi zaidi sasa wanafahamu uwepo wa huduma hii na umuhimu wa kuwahi kituo cha afya baada ya kuingia kwenye mazingira ya hatari,” amesema na kuongeza.

“Zamani watu wengi, hata waliokuwa wamebakwa, walibaki majumbani bila kujua kuwa wanaweza kupata huduma za kinga," amesema.

Amesema tafsiri ya pili ni kwamba idadi ya watu wanaoingia kwenye mazingira hatarishi ya kuambukizwa VVU imeongezeka, hivyo kuongeza mahitaji ya huduma ya PEP.

Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Dk Ernest Winchislaus, amesema takwimu za ongezeko la matumizi ya PEP zinapaswa kutafsiriwa kwa umakini kwa kuwa zinaweza kuonyesha mafanikio ya mfumo wa afya, lakini pia kuibua tahadhari kuhusu mwenendo wa vihatarishi vya maambukizi ya VVU.

Amesema kwa upande mmoja, ongezeko hilo linaonyesha wananchi wengi zaidi wanajua huduma hiyo, wanajua mahali pa kuipata na wanaelewa kuwa inapaswa kuanza kutumika ndani ya saa 72 baada ya tukio la hatari.

"Hata hivyo, takwimu hizi pia zinaweza kuibua maswali kuhusu iwapo kuna ongezeko la ngono zisizo salama, matukio ya ukatili wa kijinsia, ubakaji au ajali za kazini zinazohusisha damu na majimaji ya mwili," amesema.

Dk Winchislaus amesema PEP haipaswi kuonekana kuwa mbadala wa njia nyingine za kujikinga dhidi ya VVU.

"PEP ni hatua ya dharura baada ya mtu kuingia kwenye hatari, si mbadala wa kinga. Kila ongezeko la matumizi yake linapaswa kuambatana na uchambuzi wa kina ili kubaini chanzo cha watu wengi zaidi kuhitaji huduma hiyo," amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ally Mzige amesema pamoja na umuhimu wa PEP, watumiaji wanapaswa kufuata masharti yote ya matumizi ili dawa hizo zifanye kazi ipasavyo.

"Hii ni hatua nzuri katika kuzuia maambukizi ya VVU, lakini watu wanapaswa kujiepusha na vihatarishi vinavyowalazimu kutumia PEP.

Aidha, dawa hizi zinapaswa kutumiwa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya. Kutofuata masharti kunaweza kupunguza ufanisi wake na kumweka mtu katika hatari ya kupata maambukizi," amesema.

Amesema iwapo ongezeko la matumizi ya PEP linachangiwa na kuongezeka kwa ngono zisizo salama, ukatili wa kijinsia au ajali zinazohusisha damu, basi ni ishara kwamba juhudi za kinga zinahitaji kuimarishwa.

Ripoti inavyoonyesha

Uchambuzi wa ripoti unaonyesha tofauti kati ya watu walioripoti kuwa katika hatari ya kuambukizwa VVU na waliopata huduma ya PEP ilikuwa ndogo mwaka 2021.

Pengo hilo liliongezeka mwaka 2022 na 2023 kabla ya kupungua tena mwaka 2024 na 2025, hali inayoashiria kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za PEP kwa wanaozihitaji.

Ripoti hiyo pia inaonyesha wanaume walikuwa wengi zaidi miongoni mwa walioripoti kuwa katika hatari ya kuambukizwa VVU na waliopatiwa PEP ikilinganishwa na wanawake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali hiyo kwa wanaume inahusishwa zaidi na mazingira ya kazi yanayowaweka kwenye hatari ya kuathiriwa na VVU, wakati kwa wanawake sababu kuu ni matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Kwa upande wa wahudumu wa afya waliopatiwa PEP baada ya kuathiriwa na vihatarishi vya VVU kazini, kundi la wahudumu wengine liliongoza kwa visa 1,476, sawa na asilimia 38.1 ya waliopokea huduma hiyo.

Wauguzi na wasaidizi wa wauguzi walikuwa na visa 815 (asilimia 21.1), madaktari na matabibu 757 (asilimia 19.6), wahudumu wa maabara 331 (asilimia 8.6), wanafunzi wa kada za afya asilimia 5.4 na wahitimu wanaopata mafunzo kwa vitendo (interns) asilimia 3.3.


Hali ya maambukizi ya VVU

Takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) zinaonyesha Tanzania hupata takribani maambukizi mapya 60,000 ya VVU kila mwaka.

Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 huchangia zaidi ya theluthi moja (asilimia 33) ya maambukizi hayo, huku wasichana na wanawake vijana wakichangia asilimia 78 ya maambukizi mapya yanayotokea katika kundi hilo.

Wakati huohuo, ripoti maalumu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) iliyotolewa wakati wa mkutano wa 26 wa kimataifa wa Ukimwi uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil, imeonya kuwa dunia inaweza kushuhudia ongezeko jipya la maambukizi ya VVU na vifo vinavyotokana na Ukimwi ikiwa pengo la fedha za mapambano dhidi ya ugonjwa huo halitazibwa kwa haraka.