Sababu tatizo la pingili za mgongo
Muktasari:
- Unakaa kwenye kiti kwa muda gani? Ukaaji wa muda mrefu kwenye kiti unaweza kusababisha hatari ya kujikuta ukipata maumivu ya mgongo.
Unakaa kwenye kiti kwa muda gani? Ukaaji wa muda mrefu kwenye kiti unaweza kusababisha hatari ya kujikuta ukipata maumivu ya mgongo.
Wataalamu wa afya wanasema uti wa mgongo una pingili 33 na katikati ya pingili moja na nyingine kuna kipande cha diski kinachosaidia pingili moja na nyingine zisisagane, hivyo kila unapoinama, kukaa au kuchuchumaa kwa muda mrefu husababisha mgandamizo mkali unaohatarisha uimara wa diski.
Maumivu ya mgongo, wakati mwingine hutokea katika miguu, kiuno kutokana na pingili kupinda; zile pingili zinakandamiza neva za fahamu, pia unaweza kupata maumivu ya uti wa mgongo baina ya pingili kwa kuwa kuna sehemu ambayo ni laini.
Madhara mengine ni miguu kuhisi kama inawaka moto na hata ukitumia dawa za kupunguza maumivu mara nyingi huwa hayaishi.
Watu walio katika hatari ya kupata maumivu ya mgongo ni wale wanaobeba mizigo mizito (makuli) kuanzia uzito wa tani nne hadi nane kwa muda wa saa nane kwa siku, katika kipindi cha miaka minane na kuendelea, mtu huyu anaweza kupata matatizo ya uti wa mgongo wa binadamu.
Kundi lingine ni watu wanaofanya kazi kwa mkao wa kujikunja (Awkward Posture).
‘Awkward Posture’ inawahusu wale watu wanaochomelea chuma ndani ya meli au ndani ya mabomba makubwa, mara nyingi mafundi hawa wanakuwa wamechuchumaa au wameinama huku wanachomelea.
Kundi la tatu ni la watu wanaohamisha bidhaa au mzigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine huku wakiwa wameinama.
Ugonjwa huo unatajwa kuwa ni zaidi ya asilimia 75 hadi 80 ya magonjwa yote duniani.
Daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo, mishipa ya fahamu wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Laurent Lemery anasema wanapokea watu wenye tatizo la maumivu ya mgongo wenye umri kuanzia miaka 35 na kuendelea.
“Kwa siku tunapokea kuanzia wagonjwa 25 wenye umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea, malalamiko yanafanana, atakwambia anaumwa mgongo, mwingine ukiangalia diski zimetoka anatakiwa kufanyiwa upasuaji na wengine misuli imekaza,” anasema.
Dk Lemery anasema wagonjwa hao wamekuwa wakipata maumivu ya mgongo yanayoanzia kiunoni hadi kwenye nyonga pamoja na ganzi kwenye miguu.
Anasema kinachosababisha watu kupata changamoto hiyo ni mfumo wa maisha, alikitolea mfano vijana wanaosoma wakiwa wamekaa kuanzia asubuhi hadi jioni huku wengine wakitumia muda wao kuperuzi simu na luninga bila kufanya mazoezi.
Anasema miaka ya nyuma shuleni kulikuwa na vipindi maalumu vya michezo, lakini siku hizi watoto wanasoma kuanzia Jumatatu hadi Jjumaa na hawakimbii mchakachaka au kwenda kushiriki michezo mbalimbali, jambo ambalo linachangia kupata changamoto hiyo.
“Zamani shuleni wanafunzi walikuwa wakifanya mazoezi hata ule muda wa mapumziko utakuta watoto wanacheza mpira wa rede, kukimbizana na kucheza mpira wa miguu na wanalima kwenye mashamba ya shule, lakini siku hizi haya hayapo, ndiyo maana utakuta mtu ana miaka 35 ana matatizo ya mgongo (pingili),” anasema Dk Lemery.
Pia anasema aina ya ukaaji pamoja na viti vinachangia tatizo hilo, alitolea mfano kuna viti vya chini sana vinasababisha mgandamizo wa diski.
“Tunapaswa kutumia viti ambavyo ni salama kwa migongo yetu, ili kuepukana na tatizo hilo,” anasema.
Anasema kitaalamu dakika za kukaa zinategemeana na uzito, umri na afya ya mtu na kwamba makadirio ni kati ya dakika 45 hadi saa nne.
Ushauri na ushahidi
Dk Lemery anashauri mifumo iangaliwe upya itakayoweza kuwasaidia watoto wanapokuwa shuleni wafanye michezo, ikiwemo kukimbia mchakamchaka, rede na kulima bustani, hali itakayosaidia kuimarisha misuli inayoshikilia uti wa mgongo pamoja na mifupa.
Anasema misuli inapokuwa haina kazi inasinyaa, inakuwa haina nguvu, hivyo kinachotokea diski inaelemewa na uzito wa mwili na matokeo yake mtu kupata matatizo hayo.
Dk Lemery anasema kama ukiendelea kupuuza maumivu yanayoendelea kujitokeza kwenye mgongo inaweza kusababisha diski kucheza mahali pake au kusagika, hivyo itabidi ufanyiwe upasuaji.
“Ukiona dalili za maumivu ya mgongo, hasa yanayoanzia kiunoni hadi kwenye nyonga na ganzi kwenye miguu, ushauri wangu uende hospitali ili upewe ushauri,” anasema Dk Lemery.
Dk Lemery alitoa ushauri kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepuka hatari ya kushambuliwa na ugonjwa huo.
Imelda Isaya (28), mmoja wa waathirika anasema pingili zinazopatikana chini eneo la kiuno zinagusana na kusababisha kusagika pamoja na ute ute unaokaa sehemu hiyo umekauka.
Isaya anasema matibabu yake ameambiwa ni kufanyiwa upasuaji ambapo pingili zake zitavutwa na atawekwa plastiki pamoja na chuma.
Anaeleza alianza kupata maumivu makali ya mguu pamoja na kuwa na ganzi, jambo ambalo limemsababishia anapotembea kulazimika kusimama njiani mara kwa mara.
“Hili tatizo lilianza tangu mwaka 2020, maumivu yanaanzia kwenye kiuno kuelekea kwenye goti huku mguu unawaka kama moto, wakati mwingine unakuwa na ganzi. Sikujua nina tatizo kubwa kama hili.
“Mfano ninaposhuka kwenye daladala kuja hapa Hospitali ya Muhimbili ili nielekee kitengo cha MOI nasimama hadi mara 50 wakati huo lazima niiname, ili maumivu yapungue,” anasema Isaya.
Muathirika aliyefanyiwa upasuaji mwaka 2015, Abraham Ibrahim (72) anasema alipata tatizo la pingili na alifanyiwa upasuaji na aliwekewa plastiki, hivyo kwa sasa mguu wake umekuwa mfupi na kulazimika kutumia gongo moja kwa ajili ya kutembelea.
“Madaktari walitushauri tupunguze uzito kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara pamoja na kula aina ya vyakula, vikiwemo mabamia na mabilinganya. Uzito mkubwa unachangia kupata ugonjwa huu. Tunashauriwa kula bamia kwa sababu inasaidia kuongeza uteute kwenye pingili ili zisisuguane,” anasema Ibrahim.
Mgonjwa mwingine anayeishi mkoani Morogoro, Imelda Nesphori (40) anasema tatizo lilianzia kwenye mgongo na mara kwa mara alikuwa akipata maumivu makali na kumsababishia kushindwa kufanya shughuli zake za kumuingizia kipato.
Anasema maumivu hayo yalimtesa kwa miaka mitano na kila alipokwenda hospitali alikuwa akiandikiwa dawa, lakini tatizo lilikuwa linajirudia.
Imelda anasema tatizo hilo lilihamia kwenye mguu wa kulia na maumivu yalikuwa yanaanzia kwenye paja hadi kwenye nyayo na kumsababishia kushindwa kutembea.
“Nikitaka kutembea lazima nikae nipumzike mara kadhaa. Sehemu ya kufika dakika 10 nitasimama kwa kuinama mara saba hadi hadi nafika,” anasema Imelda.
Anasema baada ya tatizo kuwa kubwa alipewa rufaa ya kwenda Muhimbili na alipofanyiwa vipimo ilibainika mfupa wa paja ulikuwa umesagika ndipo alianzishiwa matibabu na mazoezi.
Hatari zaidi kazini
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) inahamasisha utekelezaji wa Sheria Na.5 ya Mwaka 2003 ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa kuendelea kufanya kaguzi za kiusalama na kiafya katika sehemu kazi, ikiwemo ofisi za Serikali, taasisi za umma na kukagua miradi ya kimkakati na kushauri ipasavyo.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani Aprili 28, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema wafanyakazi milioni 1.9 hufariki dunia duniani kote kwa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Makadirio hayo ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na la Afya (WHO) mwaka 2016 yalizingatia vihatarishi 19 mahali pa kazi, ikiwamo kufanya kazi muda mrefu, uchafuzi wa hewa mahali pa kazi, vihatarishi vinavyosababisha magonjwa ya pumu na saratani, vihatarishi vya egonomia, na kelele.
Kihatarishi kikubwa kilikuwa ni kufanya kazi kwa muda mrefu, kilichohusishwa na takriban vifo 750,000, ikifuatiwa na uchafuzi wa hewa mahali pa kazi uliosababisha vifo 450,000.
Kwa upande wa Tanzania, katika kipindi cha miaka mitano (2016 - 2020) taarifa za ajali na magonjwa 6,846 ziliwasilishwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa ajili ya fidia.
Katika ajali na magonjwa hayo asilimia 26.4 zilitokea wakati wafanyakazi wakiwa safarini katika kutekeleza majukumu ya kikazi na asilimia 5.3 ya ajali hizo zilisababisha vifo.