Sababu ugonjwa wa mifupa kuwasumbua zaidi wanawake

Dodoma. Chakula kilicholala, yaani kiporo ni miongoni mwa vyakula ambavyo haviepukiki katika familia nyingi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosa muda wa kukitayarisha unaotokana na shughuli za kila siku.

Wapo wengine wanashindwa kukadiria kiasi kinachotosheleza kwa siku husika na wengine hupenda kula baadhi ya vyakula siku moja baada ya kupikwa wakieleza kuwa vinaongezeka utamu.

Watu wengi wanaopenda kula viporo hawajalishi kuwa ni kundi gani la vyakula, huku wengi wakivitunza katika majokofu ili kuzuia kuchacha.

Bila kufahamu madhara yake, baadhi wamekuwa wakiwalisha watoto wadogo na wakati mwingine bila kuzingatia mlo kamili kwa ajili ya afya, hali inayochangia kupata utapiamlo unaosababisha udumavu.

Hali ya watoto kupata utapiamlo imeshuhudiwa katika mikoa ambayo imejaa utajiri wa vyakula kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Rukwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya awali ya viashiria vya uzazi na mtoto na malaria ya mwaka 2022 iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Februari mwaka huu, inaonyesha Mkoa wa Iringa unaongoza kwa udumavu kwa asilimia 59.9, ukifuatiwa na Njombe asilimia 50.4 na Rukwa kwa asilimia 49.8

Wataalamu wa afya na lishe wanazitaja sababu zinazowafanya kupata utapiamlo kwa watoto wanaolishwa viporo kuwa ni aina ya vyakula wanavyolishwa kutohusisha makundi yote yanayohitajika katika ukuaji wa mtoto.

Sababu nyingine ni vyakula vilivyopikwa na kukaa muda mrefu kuwa na tabia ya kupoteza baadhi ya virutubisho, mmeng’enyo wa mtoto kuwa na uwezo mdogo, hivyo mwili kushindwa kufyonza virutubisho vyote na kinga ya mwili kuwa ndogo.

Mkazi wa Rukwa, Magdalena Malema ni mmoja wa wazazi waliojiuliza maswali baada ya watoto wake kupata utapiamlo wakati nyumbani kwake kuna chakula cha kutosha.

Baada ya kuelimishwa, alibaini moja ya sababu za mtoto wake kupata utapiamlo ni ulaji wa viporo uliopitiliza.

“Wakati mwingine nilikuwa napika wali usiku au asubuhi nauacha wakati nakwenda shambani kwa ajili ya mtoto wangu kula pale anapojisikia njaa,” anasema.

Anasema alijifungua mtoto akiwa na uzito wa kilo 2.7, lakini uzito wake uliongezeka taratibu hadi kufikia kilo nane wakati akiwa na miaka miwili na zilikuwa haziongezeki, licha ya umri wake kukua.

Anasema licha ya kumpatia dawa za minyoo, bado alikuwa hana hamu ya kula na aliposhauriwa kumpa dawa za kuongeza hamu ya kula alikataa.

Hata hivyo, baada ya kutembelewa na maofisa afya na lishe kupitia mradi wa USAD Lishe Endelevu, alianza kuzingatia lishe katika familia yake na taratibu afya ya mtoto wake ilianza kubadilika.

“Nikipika uji nachanganya na karoti, wakati mwingine mayai apate protini. Hali ilianza kubadilika na kuwa na afya njema, hadi watoto wenzake wakaanza kumwita bonge,” anasema.Kwa nini wanapata utapiamlo?

Ofisa Lishe Mwandamizi, Wilbert Mngeni anasema sababu za karibu zinazochangia utapiamlo kwa watoto ni kukosa chakula au magonjwa yanayosababisha kukosa hamu ya kula, kuharisha na kutapika.

“Mtoto akila kiporo halafu kikamletea ugonjwa, akaumwa kutapika na kuharisha moja kwa moja mtoto huyo hupata utapiamlo. Mtoto akiugua magonjwa hayo anapoteza virutubishi vingi, lakini pia anapoteza hamu ya kula,” anasema.

Anasema uhifadhi wa vyakula baada ya kupikwa unasababisha baadhi ya virutubisho muhimu kama madini na vitamin vilivyomo kwenye chakula husika kupotea.

Mgeni anasema viporo vingine kwa jinsi vinavyohifadhiwa vinaweza kubadilika ladha na harufu na hivyo kumfanya mtoto kushindwa kula vizuri. Anasema watu wengi wanawapa watoto viporo bila hata kuvipasha moto ili kuua bakteria waliomo kwenye chakula husika.

“Wataalamu wa lishe hatushauri watoto wapewe viporo. Sio kizuri kwa watoto kwa sababu pia kinga zao za mwili bado zinakuwa chini. Tunashauri watoto wale chakula kilichopikwa muda huo huo,” anasema Mgeni.

Kwa watu wazima wanaopenda kula viporo, anasema wanashauri kuhakikisha wanavipasha kikamilifu ili kuhakikisha kuwa bakteria waliomo wanakufa.

Pia anasema ni vema kuhakikisha kinahifadhiwa mahali salama na safi pasipo wadudu, wakiwemo mende, inzi na panya kuweka vimelea vya magonjwa katika vyakula hivyo.

“Chakula kihifadhiwe mahali pazuri na kuhakikisha kabla hujakila unakipasha moto na hivyo kupunguza madhara ya kuchafuliwa na hawa wadudu,” anasema.

Mgeni anasema kitaalamu chakula kikiwekwa katika friji ambayo haina ubaridi wakati wote vimelea vya magonjwa vinakua kwa kasi kubwa.

Kutokana na hilo, anasema ndio maana ubaridi unaotumika kuhifadhia vyakula katika mafriji unatakiwa uwe umefanana wakati wote unapohifadhi ili kuepuka vimelea vya magonjwa kutokukua kwa kasi.


Makundi haya viporo si salama

Mtaalamu wa Lishe, Theresia Thomas anaungana na wataalamu wengine wa lishe kwa kutoshauri watoto kupewa viporo kwa sababu vinaweza kuwaletea madhara ya kiafya na kusababisha kuwa na utapiamlo.

Anasema kisayansi chakula kilichopoa ukipasha moto, bakteria waliomo katika chakula hicho wanakuwa wakali zaidi na ndiyo maana inashauriwa kupasha kwa joto kali kwa muda mrefu.

Theresia anasema watoto na wagonjwa wanatakiwa kula chakula kilichopikwa ndani ya saa mbili ili kuwaepusha kupata madhara yanayotokana na vyakula.


Ushauri wa madaktari

Daktari wa binadamu, Hariel Kimaro anasema kiporo si chakula salama kwenye afya ya binadamu kwa sababu kinazalisha wadudu ambao sio wazuri kiafya.

Anasema mtu anapokula kiporo ambacho ni baridi, ni tatizo kwa kuwa vyakula vya mafuta vikilala vinatengeneza mafuta machafu zaidi ambayo yanaweza kuweka utando katika mishipa ya damu.

Anasema hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa kama shinikizo la damu na magonjwa ya moyo kwa mtu huyo ambaye mishipa yake ya damu mafuta machafu yameweka utando.

“Ukitaka kukila ukipashe kwa moto mkali kuyeyusha mafuta hayo na pia kuua wadudu wanaoingia katika chakula kutoka kwenye hewa,” anasema.

Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Albert Chota anawashauri watu kupika chakula kinachotosheleza kwa mlo mmoja ili kuepuka madhara yanayotokana na viporo.