Sababu za kuongea usingizini

Wataalamu wa afya wanasema kulala ni kitendo cha kuuruhusu ubongo kupumzika kufanya kazi kwa sababu mtu anapokuwa katika shughuli zake za kila siku, huusisha ubongo.

Mbali na watu wazima, hata watoto ambao hawajaanza kufanya kazi, wanapokuwa wanacheza huusisha ubongo, hivyo wanapolala huupumzisha.

Kwa kawaida, ubongo ukifanya kazi ndani ya muda fulani unakuwa umechoka na unatakiwa kupumzika ili baadaye uweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ndani ya saa 24 za siku, ubongo huwa unafanya kazi kwa saa 16, huku saa nane zilizobaki za kulala ndio hupumzika.

Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali za afya, kulala kuna vipindi vyake ambavyo ni mtu kulala fofofo na kawaida na huwa na maana.

Daktari bingwa wa neva katika Hospitalli ya Agakhan Philip Adebayo anasema matendo ya usingizini hutokea ndani ya theluthi ya kwanza ya usingizi, wakati ubongo upo hatua ya usingizi inayoitwa (Non REM).

Anasema mtu husisimka isivyo kawaida katika hatua hiyo ya usingizi hivyo hufanya vitendo bila kufahamu.

“Hii ni kawaida kwa watoto hadi ujana wao (kuongea wakati wamelala), lakini wakati mwingine inaweza kutokea kwa watu wazima,”anasema Dk Adebayo.

Anataja sababu za matendo mbalimbali yanayoendelea mtu akiwa usingizini ikiwamo kuongea kuwa ni matatizo ya kurithi, hivyo inaweza kuwa chanzo chake kutoka kwa wazazi na kurithisha watoto wao.

Sababu nyingine zinazochangia kuongea, kutembea na kufanya vitu vingine wakati wakiwa usingizini anasema ni kutumia vitu vya kuzuia usingizi, ugonjwa wa miguu isiyotulia, matumizi mabaya ya dawa na pombe.

“Kutokana na tatizo hilo mgonjwa anaweza kutumia dawa ya Melatonin kwa msaada zaidi lakini haitibu tatizo moja kwa moja,”anasema Dk Adebayo.

Anasema kwa watoto neva zinakuwa hazijakomaa vizuri hivyo wakati wa usingizi udhibiti wa misuli unakuwa hafifu hivyo mtu huweza kutembea.

“Hii haina uhusiano na kuota ndoto mbaya maana kuna wakati mtu akiota ndoto anakumbuka lakini hii ya kuongea na kutembea usingizini mtu hakumbuki kitu chochote,”anasema Dk Adebayo.

 Kwa mujibu wa madaktari wa afya, mtu kutembea akiwa usingizini au kukaa, hii inamfanya kuwa katika hali mbili tofauti ya usingizini na kuwa macho ambayo ni hatari.

Inaelezwa kuwa, mara nyingi mtu akiwa usingizini huongea vitu visivyoeleweka, hivyo huonekana kama amechanganyikiwa, kesho yake ukimuuliza alikuwa anaongea nini hakumbuki kitu chochote.

Hamza Kilali, mkazi wa Tabata anasema tabia ya mtu kuongea na kutembea akiwa usingizini amekuwa nayo tangu utoto wake na hata alipokuwa anaelezwa anatembea usiku alikuwa anabisha kwa kuwa hakumbuki chochote.

“Mama yangu ananisimulia kuwa aliwahi kunikuta nahangaika kufungua mlango kwenda nje na alipojaribu kunirudisha nikawa nakataa na kubishana huku nalia na hawajui sababu ya mimi kuwa hivyo,”anasema Kilali.

Hata hivyo, anasema siku hizi ameacha tabia ya kutembea lakini bado anaongea usiku na kusababisha mkewe kukerwa na hiyo tabia kwa kuwa imekuwa ni kawaida na hata wakati mwingine kuongea yale aliyofanya mchana.

Mumin Jabir, mkazi wa Ilala anasema mtoto wake wa miaka minne huwa na tabia ya kunyanyuka kitandani huku akiwa amelala.

“Yaani anakuwa amefumba macho kabisa, halafu anataka kushuka kitandani basi mimi huwa namuamsha kisha namuuliza unataka nini, lakini huwa na usingizi analala tena.”