Sh24 bilioni kukabili Ebola, Mpox Afrika Mashariki
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Fedha hizo, zinazotolewa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), zinalenga kuimarisha mifumo ya usalama wa afya ya kikanda, kuongeza uwezo wa maabara, na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na majibu ya dharura dhidi ya milipuko ya magonjwa.
Arusha. Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa Euro 8 milioni (takribani Sh24.2 bilioni) kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kukabiliana na magonjwa ya Ebola na Mpox katika nchi wanachama.
Fedha hizo zinazotolewa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), zinalenga kuimarisha mifumo ya usalama wa afya ya kikanda, kuongeza uwezo wa maabara, na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na majibu ya dharura dhidi ya milipuko ya magonjwa.
Akizungumza jana Juni 13,2026 jijini Arusha wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo ya ushirikiano, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi alisema msaada huo ni ishara ya ushirikiano uliojengwa juu ya uaminifu, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja katika kukabiliana na vitisho vya afya ya umma vinavyoikumba kanda hiyo.
“Tunapokea msaada huu muhimu kutoka Serikali ya Ujerumani ili kuimarisha zaidi juhudi zetu za kupambana na milipuko ya magonjwa na kuboresha utoaji wa huduma za afya katika ukanda wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa sehemu ya fedha hizo itatumika katika awamu mpya ya utekelezaji wa hatua za kuimarisha maandalizi ya milipuko, kuongeza ujuzi wa wataalamu na kuboresha mifumo ya maabara katika nchi za EAC.
“EAC itatekeleza afua maalumu za kuimarisha utambuzi wa haraka wa magonjwa, ufuatiliaji, na uwezo wa kujibu milipuko kwa wakati,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa msaada huo utaendelea kuimarisha maabara za mkononi pamoja na mafunzo kwa wataalam ili kuhakikisha viwango vya huduma vinafanana katika nchi zote wanachama.
Alisema msaada unaoendelea kutoka Ujerumani unaimarisha azma ya EAC ya kujenga mfumo wa afya wa kikanda unaojitegemea na wenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa yanayoibuka na yanayojirudia.
Kwa upande wake, Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Manuel Mueller alisema kusainiwa kwa makubaliano hayo ya euro milioni 8 kunafungua ukurasa mpya katika ushirikiano kati ya EAC na Ujerumani, unaolenga kuimarisha afya, usalama na ustahimilivu katika Afrika Mashariki.
Alisema mradi huo unalenga kuunga mkono malengo ya kimkakati ya Mtandao wa Kikanda wa Maabara za Marejeo za EAC kwa magonjwa ya kuambukiza, sambamba na kuimarisha uwezo wa maabara katika ukanda huo.
Alifafanua EAC itatekeleza mradi huo kwa ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Bernhard Nocht ya Tiba ya Tropiki ya Ujerumani, ambayo imekuwa mshirika muhimu tangu mwanzo wa mradi huo.
“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za EAC katika kukabiliana na magonjwa haya, tukitambua kuwa magonjwa ya milipuko hayana mipaka, na yakipuuzwa yanaweza kuvuka na kuathiri hata mabara mengine,” alisema.