Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taasisi ya kimataifa kusaidia huduma za watoto njiti Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), Dk Godwill Kivuyo,akikabidhiana hati ya makubaliano na Mwakilishi wa Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Afya ya Mtoto Afrika (ICHA) Tanzania,Erik Rowberg

Muktasari:

  • Taasisi ya Afya ya Mtoto Afrika (ICHA), imeingia mkataba wa miaka mitatu na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), uliolenga kuimarisha huduma za watoto wachanga wakiwemo njiti, hatua inayotajwa kuongeza uangalizi kwa watoto hao na kupunguza vifo vyao.

Arusha. Katika kuboresha afua na huduma bora kwa watoto wachanga, wakiwemo njiti, Taasisi ya Afya ya Mtoto Afrika (Icha) imeingia mkataba na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) wa kusaidia kuboresha ufanisi wa utoaji huduma na uangalizi kwa watoto hao.

Ili kupunguza vifo vya watoto wachanga, wakiwemo njiti, Serikali imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu kama wodi za watoto wachanga.

Mkataba huo umesainiwa jijini Arusha leo, Jumanne Novemba 18, 2025 katika hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Akizungumza hospitalini hapo, mwanzilishi wa Icha, Profesa Stephen Swanson amesema mkataba huo wa miaka mitatu umelenga kuendeleza na kupanua huduma hiyo.

Amesema wataendelea kushirikiana na hospitali hiyo na wadau wengine kuhakikisha wanaendeleza ubora katika matibabu ya watoto wachanga wakiwemo njiti ili kuhakikisha wanaokoa maisha yao.

“ALMC inatambulika kwa huduma zake ikiwemo kitengo cha wodi maalumu za uangalizi wa watoto njiti (Nicu). Chini ya makubaliano haya sisi kama taasisi isiyo ya kiserikali tutatoa wataalamu wa watoto, madaktari na wauguzi tutawajengea uwezo,” amesema na kuongeza:

“Tutaboresha miundombinu, kutoa mafunzo ndani na nje ya hospitali pamoja na kuwawezesha kiuchumi lengo likiwa ni kuhakikisha huduma hizi zinatolewa kwa viwango vya juu na kuhakikisha tunaendelea kupunguza vifo vya watoto njiti.”

Amesema wataendelea kushirikiana na hospitali hiyo na wadau wengine kuhakikisha wanaendeleza ubora katika matibabu ya watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto wakiwemo njiti, ili kuhakikisha wanaokoa maisha yao.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya ALMC, Dk Godwill Kivuyo amesema kwa kipindi cha miaka 11 hospitali hiyo imekuwa ikishirikiana na Profesa Swanson ambaye alikuja kama mmishionari kutoka Marekani kutoa huduma kwa watoto njiti.

Amesema mkataba huo utaongeza ufanisi wa taasisi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake na kuendelea kutoa huduma bora kwa watoto njiti.

“Kutokana na maono ya Profesa Swanson kupitia Icha tumeingia nao makubaliano kuwasaidia watoto njiti na wale wenye changamoto za kuzaliwa chini ya mwezi mmoja,” amesema na kuongeza:

“Umuhimu wa mkataba huu ni kuwezesha huduma hii iwe endelevu isikome iendelee kutolewa kwa ubora kwa ajili ya watoto wetu Arusha na Afrika kwa ujumla, tunashukuru wameona taasisi ya kanisa inaweza kufanya nao kazi tunaahidi kuendelea kupunguza vifo vya watoto njiti.”

Mmoja wa wauguzi kutoka wodi ya Nicu, Angel Pallangyo amesema, “Nipo hapa kwa zaidi ya miaka minane, tulianza kwa kupewa elimu namna ya kusaidia familia kwani baadhi ya wazazi hudhani wao ndiyo sababu ya watoto kuzaliwa njiti, tunawaelezea kilichotokea na tunawashirikisha namna ya kuhudumia watoto.”

Muuguzi huyo amesema wamekuwa wakishirikisha wazazi wote wawili au kama yuko mzazi mmoja wamekuwa wakitoa elimu kwa mmoja wa ndugu wa familia husika ili kuelewa namna ya kuhudumia watoto njiti.

“Kupitia hospitali hii, taasisi ya Icha inasaidia familia ambazo hawawezi kulipia, hivyo kupitia mfuko walionao wanasaidia familia ambazo zinashindwa kumudu gharama ikiwemo vifaa tiba na dawa.

“Tumekuwa tukipewa mafunzo ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha utendaji kazi na yanatusaidia kutoa mafunzo kwa akina mama na familia za watoto wachanga wenye changamoto mbalimbali, wakiwamo njiti,” amesema.

Naye Dk Eunice Msuya amesema, “Tunaendelea kutoa elimu kwa wazazi kwani wengine wengi hasa wa vijijini wana dhana potofu kwa sababu wanajifungua watoto njiti, wengine wamekuwa wakidhani wao ndiyo chanzo cha kujifungua watoto njiti, ila tunaendelea kuwapa elimu,” amesema.

Agosti 2023 Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia watoto wachanga na vijana kutoka Wizara ya Afya, Dk Felix Bundala alisema kutokana na maagizo ya Serikali wodi za Nicu nchini ziliongezwa kutoka 14 mwaka 2018 hadi kufikia 250 mwaka 2024 na lengo ni kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.