Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto

Wamama wakinyonyesha watoto.Utafiti wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), umebainisha  kwamba kuwapa kinamama dawa za ARV wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na wakati wa kunyonyesha, hupunguza hatari ya kuwaambukiza watoto wao VVU. Picha na Maktaba

Muktasari:

WHO INAPENDEKEZA:

1.    Wajawazito wapimwe VVU
2.    Kama wameathirika waanze kutumia ARV
3.    Wakiwa wanatumia  ARV, wanaweza kunyonyesha
4.    Wanyonyeshe mtoto maziwa pekee kwa miezi sita.
5.    Baada ya miezi sita mtoto apewe mlo laini
6.    Baada ya mwaka mmoja, waache kunyonyesha
7.    Mtoto aliyeachishwa apatiwe vyakula bora
9.    Maziwa ya ng’ombe pia ni muhimu
10.    Maziwa ya mama ni muhimu kumjenga mtoto kimwili na kiakili

Wataalamu wa sayansi ya afya na lishe ya binadamu duniani kote, wanakubali kuwa maziwa ya mama ni muhimu kwa afya ya mwili na maendeleo ya akili ya mtoto Maziwa ya mama yana viinilishe muhimu vinavyomsaidia mtoto kukabiliana kwa ufanisi mkubwa  maambukizi ya vimelea vinavyosababisha magonjwa. Watoto wanaonyonya maziwa ya mama pia hupunguza hatari ya kupata maradhi ya pumu na magonjwa ya ngozi yatokanayo na mzio.

Tafiti zilizofanyika sehemu mbalimbali duniani, zinabainisha kuwa maradhi ya njia ya hewa, kuharisha, maambukizo ya masikio na homa ya uti wa mgongo, hayawashambulii mara kwa mara watoto wanaonyonyeshwa vizuri maziwa ya mama zao katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya umri wao.

Tafiti zinaongeza kusema kuwa hata pale watoto hao wanapougua maradhi hayo, hali yao huwa si mbaya  ikilinganishwa na wale wasionyonya.

Ndani ya maziwa ya mama hasa yale ya mwanzo, kuna kingamwili ijulikanayo kama secretory immunoglobulin A (IgA). Kingamwili hii huimarisha ngozi laini inayofunika njia ya hewa puani, kooni na katika njia ya mfumo wa chakula na kutoa ulinzi madhubuti dhidi ya vimelea hatari vinavyoshambulia mwili wa mtoto kupitia njia hizo.

Kwa sababu hiyo pia watoto wanaonyonya hupunguza uwezekano wa kupata saratani zinazowashambulia watoto hasa zile zinazisababishwa na virusi.

Maziwa ya mama yana joto linalopatana sawia na tumbo la mtoto. Hivyo hayawezi kuleta madhara kama vile michubuko kwenye ngozi laini inayofunika njia ya chakula. Watoto wanaonyonya maziwa ya mama pia hawakabiliwi mara kwa mara na hali ya kukosa choo, kutapika ovyo  na maumivu ya tumbo.

Mbali na kumpatia mtoto faida za kiafya, unyonyeshaji pia una faida kwa mama, familia na taifa kwa jumla. Wanawake wanaonyonyesha hupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti na mifuko ya mayai. Unyonyeshaji pia ni njia ya asili ya kumlisha mtoto mlo kamili bila kutumia gharama.

Wataalamu wa afya ya uzazi nao wanabainisha kuwa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kiasi cha kutosha kila siku, ni njia ya asili ya kupanga uzazi.

Wakati wa kunyonyesha mwili huzalisha kiasi cha kutosha cha kichocheo kiitwacho ‘oxytocin’ ambacho husaidia mfuko wa uzazi kurudia hali yake ya kawaida kwa haraka na kupunguza kiasi cha damu kinachopotea baada ya kujifungua. Wanawake wanaonyonyesha na kufanya mazoezi, mifuko yao ya kizazi hurejea katika hali yake ya awali ndani ya wiki sita ikilinganishwa na wenzao wasionyonyesha ambao inawachukua takribani wiki 10 baada ya kujifungua. 

Faida nyingine anayoipata mama anayenyonyesha ni kuimarika kwa mifupa yake. Wataalamu wa afya ya mama na mtoto wanabainisha kuwa katika kipindi cha kunyonyesha, tumbo la mama husharabu (hufyonza) madini ya kalisiamu kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na faida zote hizo za kimamama kunyonyesha, upo wakati ambapo wanawake wengine hulazimika kutowanyonyesha watoto wao kutokana na imani potofu kuhusu unyonyeshaji, kukosa nafasi kutokana na ajira katika sekta rasmi au kutokana na sababu za kitabibu.

Wanawake wengi hasa vijana wanafikiri kuwa kunyonyesha kunafanya matiti yao yaanguke na kupoteza mvuto. Na wengine hushindwa kunyonyesha kwa vile huona aibu kufanya hivyo mbele za watu kwa hofu ya watu kuona matiti yao hasa watoto wanapohitaji kunyonya wawapo katika kadamnasi au katika mikusanyiko ya kijamii.

Wanawake wengine huwa na hisia kuwa maziwa ya kopo ni bora zaidi kuliko maziwa ya mama na wengine hufikiri kuwa kuwanywesha watoto maziwa ya kopo ni ustaarabu na maendeleo. Na wanawake wengine hufikiri kuwa hawana maziwa ya kutosha, lakini sayansi inaonyesha kuwa kila mama ana maziwa ya kutosha hasa pale anapokuwa na afya njema ya kisaikolojia.

Miongoni mwa sababu za kitabibu zinazofanya wanawake wengi wasinyonyeshe ni matumizi ya baadhi ya dawa na maradhi anayougua mtoto au mama. Wanawake wengi wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ni mfano mzuri wa kinamama wanaolazimika kutokuwanyonyesha watoto wao kwa sababu za kitabibu.

Unyonyeshaji kwa kinamama wenye virusi vya VVU

Hata hivyo, tafiti za afya ya jamii za hivi karibuni zinabainisha kuwa, ni salama kwa mama mwathirika wa virusi vya ukimwi (VVU) anayetumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) kumnyonyesha mtoto wake kwa muda wa mwaka mmoja.

Tafiti zinabainisha kuwa ni salama  kumnyonyesha mtoto waziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 12.

Inasisitizwa kuwa unyonyeshaji huo ni lazima uende sambamba pamoja na matumizi sahihi ya dawa za ARV, hali ambayo inapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mtoto kupata maambukizi ya VVU kwa njia ya kunyonya.

Novemba  2009, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa taarifa iliyotokana na ushahidi wa tafiti mbalimbali, zilipendekeza kuwa kinamama wenye maambukizi wanaonyonyesha wanaweza kuendelea kufanya hivyo hadi watoto wao wasiokuwa na maambukizi ya VVU, wanapofikisha miezi 12 huku wao na watoto wao wakiendelea kutumia dawa za ARV. 

Pale mtoto anapobainika kuwa ana maambukizi baada ya miezi 12, inashauriwa aendelee kunyonya hadi afikishe miaka miwili.

Utafiti ulioongozwa na WHO ambao ulipewa jina la ‘Kesho Bora’ ulibainisha kwamba kuwapa kinamama dawa za ARV wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na wakati wa kunyonyesha, hupunguza hatari ya kuwaambukiza watoto wao.