Unazijua athari za kuchelewa kuzaa?

Wanawake wengi siku hizi wanachelewa kuzaa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kiafya, kusoma au hadi wajenge nyumba ndiyo waanzishe familia kwa maana ya kupata watoto.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanashauri wanawake kuzaa wakiwa na umri wa miaka 20 hadi 30 ili kuondokana na matatizo kabla na baada ya kujifungua.

Kwa miaka mingi ujumbe huo umekuwa ‘ukipelekwa’ kwa wanawake ili kuwapunguzia athari mbalimbali za kiafya.

Lakini ni mara chache kukuta wanaume wakizungumzia jambo hilo, hata kwa wake zao hali inayosababisha watu waamini kuwa wanaweza kuwa na watoto wakati wowote wanapohitaji na haijalishi umri.

Wanachosema wataalamu wa afya

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ili kujifungua watoto wenye afya njema na waliotimilifu, mwanamke anatakiwa kufanya hivyo akiwa na umri usiozidi miaka 30.

Wanasema ndani ya umri huo, mtoto aliye tumboni anakuwa katika nafasi nzuri ya kukua kwa kupata lishe bora hasa maziwa ya mama ambaye bado atakuwa na damu changa.

Dk Andrew Mombo wa Hospitali ya Bugando jijini Mwanza anasema kupata watoto kwa umri mkubwa kuna athari kama ukosefu wa uzito wa kutosha kwa mtoto.

Pia, anasema kuna uwezekano wa wajawazito kupata maradhi kama vile kisukari.

Dk Mombo anasema mwanamke kuzaa akiwa zaidi ya miaka 50 kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia 30 kwa mtoto kuzaliwa na tatizo la usonji.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Dk Cecilia Protas wa Bugando, akisema kuzaa na umri mkubwa kuna madhara mengi ikiwamo ukuaji dhaifu wa fuvu la kichwa la mtoto akiwa tumboni, sambamba na athari nyingine kwenye moyo.

“Kuna kesi nyingi ambazo zimeripotiwa kuhusiana na watu kuzaa wakiwa na umri mkubwa hasa matatizo ya moyo,miguu na mikono.Hii ni kutokana uchovu wa chembe chembe za damu ambayo imetumika kupata ujauzito,” anasema Dk Cecilia.

Anasema mbali na matatizo ya kiakili, kuna kasoro nyingine kama vile kukua polepole kinyume na ilivyo kwa watoto wengine.

Utafiti uliofanywa na taasisi za afya duniani umeonyesha watu waliopata watoto wakiwa na zaidi ya umri wa miaka 45 watoto wao wana kasoro ikiwamo ulemavu wa kimaumbile.

Dk Thomas Weria kutoka Hospitali ya Wilaya, Rorya mkoani Mara anasema watu wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha kuhusiana na madhara yanayoambatana na uzazi wa uzeeni.

“Kuna baadhi ya mila nchini ambazo hazina uelewa kuhusiana na suala hili, hivyo ni wazi kunahitajika elimu ya kutosha kwa wananchi kujua madhara yake,” anasema Dk Weria.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Dk Weria anasema mamlaka husika zinatakiwa kuweka mikakati kuntu ya kuhakikisha kwamba kila mtaa au kijiji vinakuwa na vituo maalumu kwa ajili ya kutoa ushauri kuhusu afya ya uzazi.

Wananchi wazungumza

Mary Lucas 63, mwalimu mstaafu na mkazi wa Kisesa wilayani Magu, anasema alipata watoto wake wanne akiwa na umri wa kati ya miaka 23 hadi 31 na hawakuwa na matatizo yoyote kiafya.

Mwalimu huyo ambaye ambaye alijifungua kitinda mimba wake, Moris akiwa na miaka 49, anadai alishika ujauzito bila kutarajia.

Kutokana na hali hiyo, anasema alipojifungua mtoto alikuwa hana uzito wa kutosha hali iliyomsababishia akae hospitali kwa muda mrefu kwa ajili ya uangalizi wa mwanaye.

“Kama unavyoona (akionyesha), huyu mwanangu wa mwisho anatakiwa kuniita bibi maana wanalingana na wajukuu wangu. Sikutarajia kupata mtoto nikiwa na umri kama huo,” anasema Mary.

Mzazi huyo anasema licha ya matatizo ya mtoto huyo kuwa na kilo chache, mfumo wake wa ukuaji pia ni tofauti na wale wa kwanza. “Moris anaugua mara kwa mara,” anasema Mary.

Mkazi mwingine wa Bukoba, Kagera, Justus Mugisha 72, anasema baada ya familia yake kuzama katika Ziwa Victoria mwaka 1996 kwenye ajali ya MV Bukoba, ndiyo iliyomsababishia apate watoto wa uzeeni.

“Ni dhahiri kwamba kupata watoto uzeeni kuna madhara makubwa ikilinganishwa na umri wa wastani.

“Baada ya kukosa familia yangu, ilinilazimu kuoa ili kupata watu wakiwamo watoto wa kukaa nao kwa ajili ya kunifariji. Kwa sasa nina watoto wawili (waliozaliwa akiwa na miaka 50 na 52),” anasema Mugisha.

Anasema watoto hao ambao anawazidi kwa zaidi ya miaka hamsini, wana upungufu wa kiafya ikiwamo akili na ukuaji wao ni wa taratibu sana.

Mwanaisha Mohammed (36), anayeishi kwenye ndoa kwa miaka tisa sasa na hajabahatika kupata mtoto, anasema

alikuwa na ndoto ya kuwa na mtoto kabla hajatimiza miaka 30.

Anasema hali imekwenda tofauti na matarajio yake, kwa kuwa ameshavuka miaka 35.

“Kuzaa mapema raha, kwanza unaweza kumlea mtoto vizuri na ukamtimizia mahitaji yake muhimu ikiwamo elimu.

Ila ukishavuka 35; kama mimi sijui inakuaje hapo baadaye akifika elimu ya chuo kikuu.

“Sijapenda kuchelewa kuzaa ila imetokea tu. Nimekwenda hospitali, nimeambiwa sina tatizo. Ila umri umekwenda hata sijui itakuwaje kama nikibahatika kupata ujauzito,” anasema Mohammed.