Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usanifishaji wa mashine za maabara warahisisha utoaji huduma za afya

Duka la dawa lililopo ndani ya hospitali ya Wilaya ya Manyoni

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wanasema hatua hiyo imeondoa changamoto zilizokuwepo awali, ambapo hospitali na vituo vya afya vilikuwa vinatumia mashine za aina tofauti, hali iliyosababisha ugumu katika usambazaji wa vitendanishi.

Singida. Usanifishaji wa mashine za maabara katika vituo vya afya nchini umeleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma, ukiwemo urahisi wa upatikanaji wa vitendanishi na kuimarisha utendaji wa wataalamu wa maabara.

Wataalamu wa afya wanasema hatua hiyo imeondoa changamoto zilizokuwepo awali, ambapo hospitali na vituo vya afya vilikuwa vinatumia mashine za aina tofauti, hali iliyosababisha ugumu katika usambazaji wa vitendanishi (reagents) na wakati mwingine kuchelewesha huduma kwa wagonjwa.

Hayo yamebainishwa jana Alhamisi, Aprili 23, 2026, wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika Hospitali ya Wilaya Manyoni, mkoani Singida, iliyolenga kuangazia maboresho na utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD).

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manyoni, Dk Bwire Robert amesema kuwa uamuzi wa Serikali kuleta mashine zinazofanana katika vituo vya afya umeleta mabadiliko chanya, hasa katika upatikanaji wa vitendanishi.

Amesema hapo awali kila hospitali ilikuwa na mashine tofauti, jambo lililofanya kuwa vigumu kwa MSD kuhakikisha upatikanaji wa vitendanishi kwa wakati katika maeneo yote.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manyoni, Dk Bwire Robert akizungumza na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

“Kwa sasa tuna mashine zinazofanana nchi nzima. Hapo nyuma ilikuwa changamoto kubwa kuhakikisha kila hospitali inapata vitendanishi kwa wakati. Mashine zinapotofautiana, inakuwa vigumu sana kusambaza vifaa vinavyotakiwa,” amesema Dk Bwire.

Ameongeza kuwa ujio wa mashine hizo umeongeza ufanisi wa huduma za maabara na kupunguza ucheleweshaji wa majibu ya vipimo kwa wagonjwa.

Kwa mujibu wa Dk Bwire, asilimia 99 ya bidhaa za afya katika Halmashauri ya Manyoni hupatikana kupitia MSD, huku asilimia moja pekee ikitoka kwa washirika wa maendeleo.

Ametolea mfano Hospitali ya Wilaya Manyoni, akisema imeboreshwa kwa vifaa vya kisasa ikiwemo mashine ya ultrasound yenye uwezo wa kufanya vipimo mbalimbali, pamoja na kipimo cha moyo (ECHO), jambo linalosaidia kuboresha uchunguzi wa magonjwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya MSD Dodoma, Mwanashehe Jumaa, amesema hapo awali taasisi hiyo ilikumbana na changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji ya vitendanishi kutokana na uwepo wa mashine za aina mbalimbali.

“Zamani tulikuwa tunanunua mashine tofauti tofauti. Kila mashine ilikuwa na mahitaji yake ya vitendanishi, na mara nyingi wazalishaji walitaka vitendanishi vinunuliwe kwao pekee. Hii ilileta ugumu mkubwa katika usambazaji,” amesema.

Amesema Serikali ilipoanza kununua mashine zinazofanana kwa ngazi zote za vituo vya afya kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa imewezesha MSD kusambaza vitendanishi kwa urahisi na kwa wakati.

Meneja wa Mawasiliano wa MSD, Etty Kusiluka, ameeleza kuwa taasisi hiyo inasambaza bidhaa za afya katika vituo zaidi ya 8,600 nchini, ambapo ugawaji hufanyika mara sita kwa mwaka kupitia kamati za afya.

Amesema usanifishaji wa mashine hizo umeimarisha mfumo wa ugavi wa vitendanishi na kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.

Mbali na maboresho ya maabara, Hospitali ya Wilaya Manyoni pia imepiga hatua katika utoaji wa huduma kwa watoto njiti (neonatal care), hatua iliyosaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Dk Bwire amesema kabla ya uwepo wa kitengo maalumu cha watoto njiti, watoto wengi waliozaliwa na uzito mdogo wa gramu 500 hadi 700 walikuwa wanapoteza maisha kutokana na ukosefu wa vifaa tiba.

“Zamani ilikuwa changamoto kubwa kumhudumia mtoto wa uzito mdogo. Lakini sasa tuna vifaa vya kisasa vinavyowezesha kuwahudumia watoto hao na wengi wao wanaishi na kukua,” amesema.

Ameongeza kuwa hivi sasa hata mtoto anayezaliwa kabla ya wakati, akiwa na umri wa miezi sita ya ujauzito, anaweza kuhudumiwa na kuishi kutokana na uwepo wa vifaa bora na wataalamu.

Kwa mujibu wake, maboresho hayo yamesababisha kupungua kwa vifo vya watoto njiti kutoka wastani wa vifo 12 kwa mwaka hadi kifo kimoja tu.

Aidha, uwepo wa vifaa vya kisasa kama mashine za kusaidia kupumua umechangia pia kuokoa maisha ya wajawazito na wagonjwa wengine wenye hali mbaya.

Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Manyoni wameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa hospitalini hapo, wakisema zimekuwa msaada mkubwa kwao.

Mkazi wa Kijiji cha Saswa, Fatuma Ramadhani, amesema uzoefu wake mzuri wa kujifungua mwaka 2023 ulimfanya kurejea tena hospitalini hapo kwa ajili ya huduma hiyo.

“Naleta kumbukumbu nzuri sana ya hapa hospitali. Nilijifungua mtoto mwenye kilo 4.5, hali iliyokuwa ngumu kidogo, lakini madaktari walimhudumia vizuri hadi akawa salama,” amesema.

Amesema imani yake kwa huduma za hospitali hiyo imeongezeka na ndiyo sababu ameichagua tena kwa ajili ya kujifungua.

Kwa upande wake, Maziku Abel amesema baba yake anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu hospitalini hapo, tofauti na awali walipotegemea dawa za kienyeji bila mafanikio.

“Madaktari walimpima na kugundua ana malaria. Sasa anaendelea na matibabu na hali yake inaimarika. Tunawashukuru sana kwa huduma nzuri,” amesema.

Kauli za wananchi hao zinaonyesha kuongezeka kwa imani ya jamii kwa huduma rasmi za afya, huku maboresho ya miundombinu, vifaa na usimamizi yakichangia kwa kiasi kikubwa kuinua sekta ya afya katika maeneo ya vijijini.

Hospitali ya Wilaya Manyoni inaendelea kuwa tegemeo kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo jirani, ikitoa huduma mbalimbali zikiwemo za uzazi, wagonjwa wa nje na matibabu ya magonjwa ya kawaida kama malaria.