Ushauri unavyoweza kuchangia udumavu wa mtoto

Picha na Mtandao

Katika kumjenga mtoto kiakili na kimwili, wazazi na walezi wamekuwa wakipokea ushauri wa malezi wanaopewa na kujikuta wakienda kinyume na wataalamu wa afya na malezi.

Wengi hupokea ushauri kwenye vikundi, kliniki, marafiki na mitandao ya kijamii kwa kuamini kuwa wanachoongea hao ni sahihi katika kumkuza mtoto.

Upo ushauri sahihi, waliofuata walifanikiwa lakini wengine wamekuwa wakitumia kama sehemu ya kipimo cha malezi ya mtoto kwa kuwaelezea wengine.

Wataalamu wa lishe wanaeleza kuwa asilimia kubwa ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwalisha watoto vyakula visivyo sahihi kwa sababu ya kupokea kila ushauri.

Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa lishe na malezi, Dk Luiza Temu anasema lishe za watoto zinatakiwa kufuatiliwa kwa makini zaidi, kwani ni sehemu ya kumjenga mtoto kiafya, kiakili na kimwili.

Anasema kumekuwa na udumavu kwa sababu wazazi wamekosa elimu iliyobora kuhusu malezi ya mtoto tangu anapofikia umri wa kuanza kula na kujikuta wanapokea kila ushauri kutoka kwa wengine.

"Unakuta mtoto afya inatetereka, ukimuuliza mzazi imekuwaje anasema nilipata ushauri kwa wamama wenzangu,” anasema Dk Luiza.

Anasema kila ukuaji wa mtoto unatokana na malezi aliyopatiwa tangu utotoni, hivyo amewataka wazazi kutowachukulia watoto kama watu wazima wakati bado wanahitaji malezi ya karibu na yaliyo bora.

"Wazazi wengine mtoto akifikisha mwaka mmoja na nusu anakula milo ya kiutu uzima, wakati mwingine anapewa hata visivyo saizi yake, mtoto anaonekana mtu mzima kumbe bado ni mdogo," anasema.

Mbali na hilo, daktari huyo ameonya juu ya madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa kushindwa kuandaa vyema lishe ya mtoto.

"Nafaka zikiwa chafu mtoto ataharisha na ikitokea mahindi au nafaka nyingine yoyote ilikuwa na dawa na ukapika bila kuosha vizuri mtoto anaweza pata matatizo ya ini.

Pia anasema nafaka zisizokauka vizuri iwe karanga, mahindi au yoyote ikivunda kuna sumu ambayo inaitwa Flatoxin inapatikana humo, inaweza pia kuleta tatizo la ini.

“Kama kiwango cha wanga kimezidi sana unampa mtoto nguvu nyingi ambayo haihitaji kwa muda huo. Na kwa mtoto mwenye kisukari ukimpa uji wenye wanga mwingi lazima sukari itapanda."
 

Wazazi wazungumza

Mkazi wa Buguruni, Annastazia Joseph anasema wazazi wamekuwa na tabia ya kupokea ushauri katika malezi ya mtoto, hususan akiwa wa kwanza.

"Ushauri tunapokea kwenye malezi na lishe, hasa tunayoambiwa kliniki aidha mtoto haongezeki kilo au havutii kumbeba na ukiangalia watoto wengine wamenona,” anasema Annastazia.

Annastazia anasema kuna watoto wengine hawapendi kula, hivyo wanajikuta wanakabwa, ikishindikana wanauliza wengine kuhusu ulaji wa watoto na chakula gani kinafaa.

"Mimi mwanangu anapewa unga wa dona na siagi, siamini katika ushauri wa watu kuhusu lishe ya mtoto wangu, naona jinsi watoto wengine wanavyohangaika wakati wa kujisaidia kutokana na michanganyiko," anasema Rajabu Kimweli, mkazi wa Mashine ya Maji.

Anasema hata akikaa na marafiki huuliza kwa waliowatangulia kupata watoto, lakini mwisho kila mmoja anakwenda kufanya anachoona kinafaa kwa mtoto wake.
 

Msaga nafaka

Msaga nafaka Tabata, Msanifu Msafiri anasema chakula sahihi cha kumpatia mtoto anayeanza kula ni moja ya mambo muhimu ambayo huwasumbua wazazi wengi, kwani wapo wanaokwenda kwenye ofisi yake kuomba ushauri vitu vya kuchanganya.

"Kwa kawaida lishe ninayosaga hapa unakuta wamechanganya mahindi, mchele, ulezi, soya, mtama, karanga na dagaa au mahindi, ulezi, soya, mchele, karanga, ngano, ufuta, nikiletewa nasaga nawapa wanaondoka nao," anasema.

Anasema wakati mwingine anawaambia wahusika kupunguza baadhi ya vitu, vinakuwa vingi kuliko vingine na kuweka ugumu kwenye usagaji wa mashine.

Msafiri anasema wazazi wanafanya hivyo kupitia wenzao, mwingine hajui kama aliyempa ushauri amepewa vyakula maalumu, kwa hiyo wanawafikiri ni sehemu ya vyakula vya watoto kwa kuwa tu ameona mtoto wa huyo mtu hafanani na wake.

Anasema wapo wazazi wanawachukulia watoto vyakula kwa mama lishe kutokana na uvivu na kutokujua vyakula hivyo vimeandaliwaje, akitolea mfano wa uji, wengi hawaivishi vizuri.

Hata hivyo, anasema kumekuwa na wafanyabiashara wakiwa wanawashawishi wazazi kununua unga wanaotengeneza bila kujua kama mtoto ana tatizo la kitu gani katika moja ya nafaka anazochanganya.

Rose Adam ni mwandaaji na muuzaji wa unga lishe kwa ajili ya uji wa watoto, anasema mtindo wa maisha umesababisha kuwa na malezi ya tofauti katika ulishaji wa watoto na wamejikuta wakiangalia biashara hiyo baada ya kugundua kuna uhitaji wa hali ya juu.

Anasema uandaaji wa lishe unahitaji uzoefu na ufahamu mzuri wa lishe ya watoto, kwani watu wasipokuwa makini, wanaweza kuhatarisha afya ya mtoto kwa sababu ya kutafuta pesa.