Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Mambo sita yanayoathiri ubora wa mbegu za kiume

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wametaja mambo sita ambayo mwanamume anapaswa kuwa makini nayo, ili kutoathiri ubora wa mbegu zake za kiume.

Ili binadamu akamilike, mwanamume anatakiwa kutoa chembeuzi ‘chromosome’ 23 na mwanamke chembeuzi 23 na kukamilisha Asidi Kiinideoksiribo ‘DNA’ 46.

DNA hizi hubeba vinasaba au jeni, yaani sehemu ambazo zinaamua tabia za kiumbe husika kama vile mwonekano, jinsia na yale yote kilichopokea kutoka kwa wazazi wake.

Lakini wasiwasi mkubwa hivi sasa ni kutokana na kushuka kwa kiwango na ubora wa mbegu za kiume, kutokana na tafiti zaidi ya 200 zilizofanyika duniani ukifikia nusu.

Mwanamume anaweza kuzaliwa vizuri akapata matatizo yakaathiri mbegu zake au akazaliwa tayari ana shida katika mbegu zake, ingawaje wanaopata matatizo baadaye idadi yao inatajwa kuongezeka.

Hili limetajwa kusababishwa na mambo mengi, hasa vyakula na mtindo wa maisha, athari zimejitokeza kwenye kiasi cha mbegu za uzazi anazotoa mwanamume, ubora wake na uwezo wake kuogelea katika majimaji ukeni kulifikia yai.

Mkuu wa kitengo cha upandikizaji mimba (IVF) Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Matilda Ngarina anataja mambo ya kufuata na kuepukwa ili mwanamume awe na mbegu zilizo bora.

Dk Ngarina anasema mwanamume lazima ajue vitu vingapi vinaweza kuharibu ubora, akitaja wapo ambao huzaliwa wakiwa tayari na changamoto ya mbegu, ikiwemo shida za homoni, mfumo na wengine kupata athari baadaye na kuharibu ubora wa mbegu zinazozalishwa.

“Inategemea unakula nini, unakunywa nini, unafanya kazi gani na tabia ya ngono zembe pia nayo inaathiri ubora wa mbegu.

“Ukifanya ngono zembe ukawa na maambukizi inaathiri ubora wa mbegu, ukinywa pombe nyingi, sigara, kukaa muda mrefu sehemu yenye joto inaathiri ubora wa mbegu,” anasema.

Anataja kutokula vyakula vyenye ubora, ikiwemo mboga za majani, matunda na protini kwa wingi kuwa ni tabia ambazo huathiri ubora wa mbegu pamoja na kuharibika kwa mishipa ya kupitishia mbegu kutokana na joto kali pia inachangia.

Mambo sita yanayoathiri ubora wa mbegu za kiume

Mbegu bora ni ipi?

Dk Ngarina, ambaye ni bingwa wa magonjwa ya kike na uzazi, anasema ubora ndio unaoamua urahisi au uwezekano wa mwanamke kupata ujauzito au kutengeneza watoto, kwahiyo ubora wa mbegu ni kitu muhimu.

Anasema ili mbegu ziweze kuonekana bora, huangaliwa katika vitu vinne, ikiwemo idadi ya mbegu anazozitoa mwanamume.

“Katika mshindo mmoja mwanamume anatakiwa kutoa mbegu zaidi ya milioni 30, kwa hiyo kuwa chini ya hapo inategemea, mwingine ana sifuri kabisa, mwingine anakuwa na milioni moja, milioni tano na mwingine zaidi ya milioni 30,” anasema.

Dk Ngarina anataja kitu kingine ni ubora wa zile mbegu anazozitoa. “Ile manii inavyomwagwa ina vitu vingi, huwa tunaangalia kwenye hadubini tunaona tabia za mbegu husika, tunaangalia na kuona jinsi zinavyotembea kwenda kutafuta yai, kawaida mbegu bora ukiiweka pale inaogelea kwa kasi kwenda mbele.

“Ina kichwa, shingo na mkia, ni kama mjusi alivyo, huwa inaenda inatembea kwenda kutafuta yai kwa kasi, utaona inajigonga inashtuka inasonga mbele. Mbegu ambayo si bora unaikuta inachezacheza palepale imeenda kulia, kushoto mara inarudi ilikotoka inazunguka pale pale.

“Tunaona vizuri zaidi kwenye hadubini, utakuta nyingine iko palepale siyo bora, inatembea palepale haijui inatakiwa kwenda wapi. Asiyebora mwingine utakuta ikimwagwa ipo palepale haina safari yoyote inatulia tuli.”

Dk Ngarina anasema wanavyoangalia ubora wa mbegu ili watoe majibu kwamba ni bora, hutakiwa zaidi ya asilimia 60 ziwe na safari zinazoeleweka.

Anataja changamoto nyingine wanayokutana nayo ni mbegu isiyo ya kawaida, “mwingine mbegu zipo nyingi lakini kila unayoiangalia mara haina kichwa, haina miguu, ina kichwa. Kuna namna kichwa kinatakiwa kuwa, shingo iweje, mkia uwe namna gani na mbegu iwe na urefu gani, ufupi na size ipi.”


Changamoto

Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari imeanza kutoa huduma ya upandikizaji mimba kwa kundi la kwanza la wenza wanaohitaji huduma hiyo, baada ya kufunguliwa kwa kitengo hicho hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, bado hawajafanya utafiti kubaini tabia za mbegu zisizo bora kwa wanaume wengi zina changamoto ipi kati ya hizo alizoainisha hapo juu, ikiwemo mwendo, maumbile na idadi.

Ila anasema mara nyingi wenye shida ya mbegu, hukumbana na changamoto hizo zilizoainishwa.

“Wengine ni chache, wengine hawana kabisa mbegu, yaani akimwaga pale unakuta hakuna mbegu kabisa, wengine wanamwaga unakuta zote ziko hapo hazina safari kabisa, wengine wanamwaga lakini hazina viwiliwili,” anasema.

Hata hivyo, Dk Ngarina anasema lishe ndiyo inaamua ubora wa mbegu, vyakula ambavyo vipo hasa maeneo ya mijini wengi wanaona uvivu au siyo hadhi kula ugali wa mtama ule ambao haujakobolewa, vile vyakula asili ni bora zaidi.

Anasema vyakula visivyo bora vinaathiri sana ubora wa mbegu, hasa vile vyenye mafuta mengi vilivyopita kwenye viwanda kwa asilimia kubwa vinaharibu ubora wa mbegu.

“Maeneo ya vijijini hawana shida sana kwa kuwa wao hawali vyakula vibaya, wanakula lishe nzuri ile inayotakiwa, hasa kama jamii ni wakulima na wafugaji wazuri,” anasema.

Akizungumzia uhusiano wa mbegu na DNA, Dk Ngarina anasema mbegu hubeba DNA au chembeuzi 23 zote ambazo mtu anahitaji katika mwili wake ili aweze kuwa binadamu kamili na inapokwenda hukutana na yai la kike lililobeba chembeuzi 23, ili binadamu atokee inahitajika chembeuzi 46.

“Nusu uhai anaitia baba na nusu anatoa mama, kwa hiyo bila kuwa na mbegu huwezi kukamilisha uhai wowote,” anasisitiza.


IVF Muhimbili

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, Muhimbili kwa sasa wapo kwenye mkakati, wameanza kundi la kwanza la wagonjwa kwa kuwa upandikizaji hauwezi kufanyika kwa mmoja.

“Lazima mwenza wake aje na kama nilivyosema nusu inatoka kwa baba na nusu kwa mama, hatutaweza kuendelea na anayekuja peke yake.”

Anasema wanafanya hivyo ili kujua pia shida iko wapi. “Mara nyingi mwanamke anaweza akaja peke yake kwa maana mara nyingi wanawake ndiyo huwa tunaona hatuzai, ukishamwelewesha mwanamume anakuja kwa shingo upande.

“Tunafanya uchunguzi na wakati wote huwa tunahangaika na kinamama, kumbe shida ipo kwa baba na mara nyingi tunagundua ni tatizo linalotibika kwa dawa pekee, anapata mtoto kwa njia ya kawaida.”

Anasema katika uhalisia wanaume kote duniani hawapendi kuonekana wana shida ya uzazi.

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, kwa wanaume anaohitaji kujua tabia za mbegu zao wanapata nafasi kufanyiwa vipimo. “Yeyote anayekuja kufanya kipimo anapata majibu, upo hapa tunakwambia mbegu zako zote zinatembeea kutafuta yai hazina shida, mwingine tunamwambia pole hakuna mbegu kabisa.

“Wanakuja wengi huwataki kusema kwa nini wanapima mbegu zao, lakini unamsoma kwamba amegundua kuna shida anaomba kupima mbegu zake, tunawapima na kuwapatia majibu yao.”