Uzalishaji mbegu kiume wazidi kupungua-Utafiti

Dar es Salaam. Idadi ya mbegu za kiume duniani kote inapungua kwa kasi ya kiwango cha asilimia 50 katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, utafiti mpya umebaini.

Utafiti huo umeonyesha kwa mwaka 2018 mwanaume alitoa mbegu milioni 33 hadi milioni 46 katika kila mililita ya shahawa, kiwango ambacho pia kimetajwa kupungua kwa asilimia 50 kwa sasa ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 1973, ambapo alizalisha mbegu milioni 101.1 kwa mililita.

Wakati ripoti hiyo ikichapishwa katika jarida la Human Reproduction Update Novemba 15, hapa nchini kumekuwa na ongezeko la wanaume wanaopata changamoto hiyo kutokana na mtindo wa maisha na ongezeko la joto kwa mujibu wa daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili.

Mkuu wa Kitengo cha magonjwa na kinamama na uzazi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Nathanael Mtinangi alisema changamoto hiyo nchini inaonekana pia, kwa sababu asilimia 50 ya wagumba wanaogundulika ni wanaume.

Alitaja miongoni mwa mambo yanayogundulika kwa wanaume kuwa ni kutokuwa kabisa na mbegu, kuwa nazo zenye ubora hafifu na zisizo na mbio, mbegu chache zinazorudi kinyumenyume au kufanya tendo mara kwa mara na hivyo kuathiri uzalishaji mbegu bora.

“Tunachokigundua kwao anaweza kuwa hana mbegu kabisa kulingana na maumbile yake alivyozaliwa, ama ana mbegu zinatengenezwa lakini zinafika mahali zinakutana na kipingamizi, mwanaume ama hatengenezi mbegu au anatengeneza chache,” alisema.


Utafiti

Utafiti huo, ulioongozwa na mtaalam wa uchunguzi wa magonjwa kutoka nchini Israeli, Hagai Levine, unahusisha utafiti wa mwaka 2017 ambao ulikuwa umechunguzwa kwa kujumuisha maeneo ya Amerika Kaskazini, Ulaya, Australia na New Zealand pekee.

Unajumuisha takwimu kutoka kwa wanaume zaidi ya 57,000 waliokusanywa katika tafiti zaidi ya 223 katika nchi 53 na kuufanya kuwa uchunguzi mkubwa zaidi kuwahi kufanywa juu ya mada hiyo.

Kati ya mwaka 1973 hadi 2018, mkusanyiko wa mbegu za kiume kwa wanaume ambao hawajulikani kuwa wagumba ulipungua kwa zaidi ya asilimia 51, kutoka kwa mbegu milioni 101.2 hadi milioni 49 kwa milimita ya shahawa.

Utafiti huo unaungwa mkono na daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kwa wanaume, Steven Kaali, aliyesema hiyo ina maana kuwa mbegu zinapozidi kupungua hata uzalishaji pia unapungua.

“Mbegu za kiume zikiwa chache uzalishaji wake unakua mdogo, zikiwa nyingi uwezekano wa kuzalisha unakua mkubwa, ijapokuwa kuna matatizo mengine ambayo yatasababisha mbegu kushindwa kulifikia yai na kutungisha mimba,” alisema Dk Kaali huku akitaja mtindo wa maisha kuwa sababu kuu.