Vituo vya afya vinavyobadilisha maisha ya wananchi
Muktasari:
- Hadithi ya Bezi inaakisi hali halisi ya mabadiliko yanayoendelea kwenye sekta ya afya nchini, ambapo ongezeko la zahanati, vituo vya afya na hospitali limeanza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma.
Mwanza. “Wajawazito walikufa kwa sababu ya kukosa huduma…mtu anaumwa uchungu usiku anakosa mtu wa kumpeleka kwenye huduma za afya, analazimika kujifungulia huku kisiwani. Mwishowe hali ikiwa siyo yenyewe anakata roho.”
Ni sehemu ya simulizi ya uchungu ya John James, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bezi, uliopo kisiwani katika Kata ya Kayenze mkoani Mwanza, akikumbuka maisha kabla ya ujenzi wa zahanati haujaanza kisiwani humo.
Anasema kwa muda mrefu wakazi wa eneo hilo walikumbwa na changamoto kubwa ya umbali na gharama za kufuata matibabu, huku wakilazimika kukodi mitumbwi kwa Sh150,000 kufuata huduma nchi kavu.
“Sisi tunakaa kisiwani, mjamzito alitakiwa aondoke asubuhi kwenda kliniki na kurudi jioni. Gharama za huko nchi kavu zilikuwa kubwa, wengine walishindwa kabisa kuhudhuria kliniki ikabidi kujifungua bila uangalizi,” anasema na kuongeza kuwa baadhi ya wagonjwa walikuwa wakifia njiani au ziwani kabla ya kufika kupata huduma,”anaeleza.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ilitenga Sh206 milioni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Bezi, ambapo Sh103 milioni ni kwa ajili ya jengo la zahanati na Sh103 milioni kwa ajili ya nyumba ya watumishi wa afya.
Mradi huo ulianza Februari mwaka 2025 kwa ushirikiano na wananchi, ambao walijitokeza kwa nguvu kushiriki ujenzi.
“Wananchi waliupokea mradi kwa hali ya juu… kufikia Juni kazi kubwa ilikuwa imefanyika kwa zaidi ya asilimia 90 kutokana na nguvu ya wananchi,” anasema James.
Anaongeza kuwa kazi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika kupitia bajeti ya halmashauri katika mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi, 2026, huku matarajio yakiwa ni kuona huduma zikianza kutolewa ndani ya mwaka huu.
Zahanati ya Bezi na takwimu za vituo
Hadithi ya Bezi inaakisi hali halisi ya mabadiliko yanayoendelea kwenye sekta ya afya nchini, ambapo ongezeko la zahanati, vituo vya afya na hospitali limeanza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 10,153 mwaka 2021/22 hadi 13,683 kufikia Machi 2026, sawa na ongezeko la vituo 3,530. Zahanati zimeongezeka kutoka 7,189 hadi 8,706 huku hospitali zikiongezeka kutoka 404 hadi 475 mwaka 2026.
Akizungumza bungeni Mei 11, 2026 wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mchengerwa alisema sekta ya afya nchini imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha awamu ya Sita, yaliyoongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba, upatikanaji wa dawa pamoja na huduma za kibingwa na za dharura nchini.
Anasema Serikali imeongeza majengo mapya katika hospitali mbalimbali zikiwemo Hospitali ya Muhimbili, KCMC, BMH, Bugando, Mirembe, pamoja na Kibong'oto huku ikiwa imejenga hospitali mpya 10 za rufaa za mikoa, kukarabati hospitali kongwe 50, kukamilisha maboma 980 ya zahanati na kujenga vituo vya afya 390.
Aliongeza kuwa, katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, Serikali imeongeza wodi za watoto wachanga kutoka 80 hadi 438 pamoja na vituo vya upasuaji wa dharura kutoka 445 hadi 630 ambayo ni mafanikio yaliyochangia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.
“Katika huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa, Serikali imenunua na kusimika vifaa tiba vyenye thamani ya Sh241.6 bilioni,"alisema na kusisitiza: “Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa urahisi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu… ndiyo maana tunaendelea kujenga na kuboresha vituo vya kutolea huduma nchi nzima.”
Ahadi ya Rais Samia
Akifungua Bunge la 13 Novemba 14, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alisema huduma za kibingwa zitaongezwa kwenye hospitali za rufaa na mikoa ili kupunguza gharama za wananchi kufuata huduma mbali.
"Tutaongeza huduma za kibingwa za afya kwenye hospitali zetu za rufaa za mikoa na hospitali za rufaa za kanda, ili tuwapunguzie gharama wananchi kutafuta huduma za rufaa nje ya mikoa yao. Tunataka, badala ya kuwa na watu kuzifuata huduma, huduma ziwafuate watu,"alisema Rais Samia
Faraja kwa wajawazito
Wananchi wengi hivi sasa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hawalazimiki kusafiri umbali mrefu kufuata huduma, hali iliyokuwa ikihatarisha maisha hasa kwa wajawazito.
Mkazi wa Makambako, Njombe, Maria Nyalusi, anasema tofauti ni kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kutokana na usumbufu wa kufuata mbali huduma za uzazi, wanawake wengi walijifungulia nyumbani.
“Serikali yetu sasa hivi imeboresha huduma za afya…zamani miaka ya 1990 ilikuwa ni shida. Kwa mfano, sisi kwetu Makambako ilikuwa ukiumwa uchungu basi ujipange kutafuta usafiri kwenda mbali maeneo ya Mlengula au Kibema,’’ anaeleza.
Faraja aliyonayo Maria inajiakisi pia kwa Kulwa Lusega, mkazi wa mkoani Mwanza anayesema: ‘’Nilipoenda kujifungua sikuwa na damu kabisa.Uzuri nilianzia kituo cha afya Buhongwa wakanipa rufaa nikaenda Butimba (Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana). Ujenzi wa miundombinu ya afya, kikiwemo kituo cha afya Buhongwa, umenisaidia kwa sababu ingekuwa mbali lazima ningekufa, lakini namshukuru Rais Samia katusaidia wanawake.’’
Wataalamu wa afya wanasema kuongezeka kwa vituo vya afya, kumesaidia kuongeza idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya chini ya uangalizi wa wataalamu.
Hii imepunguza hatari za vifo vya mama na mtoto, ambazo awali zilichangiwa na kuchelewa kufika hospitali au kujifungulia majumbani bila msaada wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa Jarida la Takwimu za Hali ya Utoaji wa Huduma za Afya nchini kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2024, idadi ya wajawazito waliohudhuria kliniki angalau mara nne au zaidi, imeongezeka kutoka 1,404,631 katika kipindi cha Januari hadi Juni 2023 hadi 1,524,074 mwaka 2024.
Katika huduma za kujifungua, wajawazito waliojifungulia katika vituo vya afya wameongezeka kutoka 1,028,726 hadi 1,091,290, huduma za upasuaji wa dharura kwa wajawazito zimeongezeka kutoka 118,603 hadi 127,345, huku, vyumba vya uangalizi maalum kwa watoto wachanga vikiongezeka kutoka 175 hadi 184
Muuguzi na mkunga, Johari Mlagwa anasema kutokana na maboresho na ongezeko la vifaa tiba na huduma za uzazi, wajawazito wengi wanajifungulia kwenye vituo vya afya hali inayowasaidia kuwa salama wao na watoto wao.
“Wengi wanajifungulia hospitalini…siku hizi masuala ya kujifungulia nyumbani hayapo kwa sababu huduma zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa sana,”anasema.
Tumaini magonjwa mengine
Ongezeko la vituo vya kutolea huduma nchini halijaleta faraja na matumaini kwa wajawazito pekee. Wagonjwa wengi wakiwamo wa figo sasa wana ahueni kwa kuongezeka huduma hospitali kadhaa ikiwamo ya upandikizaji wa figo.
Awali huduma hiyo ilitolewa Hospitali Kuu ya Muhimbili, lakini sasa imeenea katika hospitali kadhaa za rufaa ikiwamo Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma.
Kama haitoshi, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza Aprili mwaka huu, imefanikiwa kwa mara ya kwanza kupandikiza figo tangu kuanza kwa mchakato huo miaka miwili iliyopita.
Even Mauki anaishukuru Serikali, wataalamu pamoja na ndugu yake aliyemchangia figo na kufanikisha kupandikizwa kiungo hicho katika Hospitali ya Bugando, akieleza ana matumaini ya kurejea katika maisha ya kawaida.
Ongezeko la vifaa tiba na huduma za kibingwa
Sambamba na ujenzi wa vituo vya afya, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba vya uchunguzi ili kuwezesha utoaji wa tiba sahihi kulingana na ugonjwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, hadi kufikia Juni 2024 mashine za MRI zimeongezeka kutoka sita mwaka 2022 hadi 13, CT Scan zimeongezeka kutoka 22 hadi 45, Ultra Sound zimeongezeka kutoka 296 hadi 469 na Digital X-ray zimeongezeka kutoka 192 hadi 677. Ongezeko hilo limeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uchunguzi wa magonjwa nchini.
Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2024 pekee, jumla ya wagonjwa 531,861 walipata huduma za uchunguzi kwa kutumia vifaa hivyo, ambapo wagonjwa 28,877 walihudumiwa kwa MRI, 38,778 kwa CT Scan, 227,005 kwa Ultra Sound na 237,201 kwa Digital X-ray.
Gharama kikwazo
Licha ya maendeleo na uwepo wa vifaa tiba hivi ya kisasa, wananchi wanaiomba Serikali iangalie upya gharama za vipimo kwa kutumia mashine hizo.
“Mwanangu alipata ajali ya bodaboda tulipofika Bugando ikatakiwa apimwe CT Scan na tukalazimika kugharamia Sh200,000. Tulijichangisha na kukopa hadi ikapatikana na akatibiwa. Tunaomba Serikali iangalie upya gharama ili sisi wenye hali ya chini pia tupate unafuu tunapohitaji vipimo hivyo,”anasema Asia Salum, mkazi wa jijini Mwanza.
Anashauri kwakuwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye Bima ya Afya kwa wote, ni vyema ikahakikisha vipimo vyote vinaingizwa kwenye bima, ili mwananchi awe na uhakika wa huduma zote.
Si gharama pekee, juhudi hizi za Serikali zinakwaza pia na changamoto kadhaa ikiwamo uharibikaji wa vifaa na mazingira ya utoaji wa huduma katika vituo vingi vya afya, jambo linalofifisha dhamira njema ya kuboresha sekta ya afya nchini.
‘’Ukweli ni kwamba uharibifu wa vifaa na vitendea kazi, rushwa, huduma duni, na mazingira ya hofu kwa watumishi wa afya ambapo hakuna uhuru wa kutoa maoni hasi, si matatizo ya hospitali moja bali ni changamoto zilizoenea katika hospitali nyingi za umma nchini,’’ anasema Waziri Kivuli wa Afya wa chama cha ACT- Wazalendo alipoozungumza na Mwananchi mwishoni mwa mwaka jana.