Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wengi waliopima afya Sabasaba wakutwa na shinikizo la damu

Muktasari:

  • Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Thabit Ramadhan, amesema mafanikio hayo yanaonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupima afya na kupata elimu kuhusu magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza.

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 1,200 wamejitokeza kupima afya zao kwenye banda la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), jambo linaloonesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kupima afya.

Taasisi hiyo imefikia asilimia 75 ya lengo lake la kutoa huduma kwa watu 1,600, wengi wa waliotembelea banda hilo walipima magonjwa ya moyo huku wengine wakichanjwa chanjo ya homa ya ini.

Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 14, 2026, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dk Thabit Ramadhan, amesema mafanikio hayo yanaonesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupima afya na kupata elimu kuhusu magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza.

“Tumefanikiwa kukaribia lengo letu kwa kuwahudumia wananchi zaidi ya 1,200. Hii ni zaidi ya asilimia 75 ya malengo tuliyojiwekea ya kuwafikia wananchi kati ya 1,000 na 1,600,” amesema Dk Ramadhan.

Amesema kati ya wananchi hao, 510 walifika kwa lengo la kufahamu hali ya afya zao kupitia vipimo mbalimbali, huku asilimia 47 wakibainika kuwa na shinikizo la damu, jambo linaloonesha ukubwa wa tatizo hilo katika jamii.

Kwa mujibu wa Dk Ramadhan, zaidi ya asilimia 58 ya wananchi waliotembelea banda la JKCI walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo, ikiwamo kipimo cha picha ya moyo (Echocardiography), umeme wa moyo (ECG), kipimo cha mapigo ya moyo wakati wa mazoezi (Stress Test), pamoja na kupatiwa ushauri na matibabu kulingana na mahitaji yao.

Aidha, amesema zaidi ya wananchi 50 walipatiwa huduma za kupimwa na kuchanjwa chanjo ya homa ya ini.

Akizungumzia kampeni ya ‘Toa ni moyo’, Dk Thabit amesema inalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo.

Amesema Serikali, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, hugharamia matibabu ya zaidi ya watoto 300 wenye matatizo ya moyo kila mwaka, lakini mahitaji bado ni makubwa.

“Zaidi ya watoto 20,000 huzaliwa kila mwaka na matatizo ya moyo. Hata kama tunatibu zaidi ya watoto 300 kila mwaka, bado idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo,” amesema.

Ameeleza kuwa gharama kubwa za matibabu ndiyo changamoto kuu inayosababisha watoto wengi kushindwa kupata huduma kwa wakati. Hivyo, ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia kampeni ya ‘Toa ni moyo’ ili kuokoa maisha ya watoto hao.

Mbali na huduma za uchunguzi na matibabu katika maonyesho hayo, JKCI pia ilitoa elimu kuhusu mtindo bora wa maisha na lishe inayosaidia kuzuia magonjwa yasiyoambukiza.

Dk Ramadhan amesema zaidi ya wananchi 150 walipatiwa elimu ya afya kuhusu umuhimu wa lishe bora, mazoezi na kuzingatia mtindo mzuri wa maisha ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la JKCI, Asha Jumanne, mkazi wa Kigamboni, amesema huduma zinazotolewa na taasisi hiyo zimemsaidia kugundua kuwa ana shinikizo la damu, jambo ambalo hakuwa akilifahamu awali.

“Nimekuja kwa ajili ya kupata ushauri wa afya, lakini baada ya kupimwa nimegundulika kuwa na shinikizo la damu. Nashukuru huduma hizi zimetolewa bure kwa sababu zimenisaidia kujua hali yangu mapema, na sasa nitafuata ushauri wa madaktari,” amesema.

Kwa upande wake, mkazi wa Ubungo, Hamisi Jackson, ameipongeza JKCI kwa kuendelea kutoa elimu na huduma za uchunguzi kwa wananchi, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya watu wanaofika hospitalini wakiwa tayari wamepata madhara makubwa ya magonjwa ya moyo.

“Elimu wanayoitoa ni muhimu sana. Watu wengi hawapimi afya zao hadi wanapougua. Kampeni kama hizi zinapaswa kufanyika mara kwa mara, hata katika ngazi za wilaya na mikoa, ili wananchi wengi wanufaike,” amesema.