Wenye VVU walivyo hatarini

Miongoni mwa sababu kubwa inayochangia watu wenye virusi vya Ukimwi (VVU) kuwa wenye hatari ya kupata aina ya pili ya kisukari ni matumizi ya baadhi ya dawa zinazotumika kupunguza makali ya virusi hivyo.  Dawa hizi zinaweza kuleta shida kwenye ufanyaji kazi wa insulin mwilini ambayo husaidia kudhibiti sukari mwilini.

Unene kupita kiasi, pia ni sababu nyingine inayochangia hatari ya kupata aina ya pili ya kisukari kwa watu wenye VVU. Baadhi ya dawa za VVU zinahitaji sana ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi na mafuta, hii inaweza kusababisha ongezeko la uzito.

Unene kupita kiasi unaongeza hatari ya kisukari na matatizo mengine ya kiafya. Hivyo, ni muhimu watu wenye VVU kuchukua hatua za kudhibiti uzito wao kama vile kudumisha lishe bora na kujumuisha mazoea ya kimwili katika maisha yao ya kila siku.

Zifuatazo ni baadhi ya njia za kuzuia kisukari kwa watu wenye VVU. Mosi, lishe yenye afya ni msingi wa kuzuia kisukari. Watu wenye VVU wanahitaji kula vyakula vyenye virutubisho muhimu na kuepuka vyenye sukari nyingi na mafuta mengi. Matumizi ya matunda, mboga nafaka ambazo hazijakobolewa na protini aina ya mbegu kwa wingi ni muhimu kwao.

Pili, mazoezi ni sehemu muhimu ya maisha ya afya na inaweza kusaidia kuzuia kisukari. Watu wenye VVU wanapaswa kujumuisha mazoezi ya mara kwa mara katika ratiba zao. Hata mazoezi madogo kama kutembea, kuruka kamba au yoga yanaweza kuwa na manufaa.

Mazoezi husaidia kudhibiti uzito, kuboresha uzalishaji wa insulini, kuchoma sukari na mafuta mwilini na huimarisha afya ya mwili na akili kwa ujumla.

Tatu, ni muhimu kufuatilia afya ikiwa ni pamoja na  kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa viwango vya sukari mwilini na vipimo vingine vya afya.

Hali hiyo inaweza kusaidia kugundua mapema dalili za kisukari na kuchukua hatua stahiki.

Nne, watu wenye VVU wanapaswa kuzungumza na wataalamu wao wa afya kuhusu dawa wanazochukua na jinsi zinavyoweza kusababisha hatari ya kisukari. Kama inavyofaa, mabadiliko ya dawa yanaweza kufanyika chini ya mwongozo wa mtaalamu wa afya.

Tano, kupunguza msongo wa mawazo ambao unachangia hatari ya kupata kisukari. Unaweza kupunguza hali hiyo kupitia mazoezi ya kupumzika kama vile yoga, au kwa kutafuta msaada wa kisaikolojia. Kudhibiti hali hizi ni sehemu muhimu ya kudumisha afya ya akili na mwili.