Amapiano inavyobeba promo ya kazi na bata Bongo

Tungo nyingi za wasanii wakubwa Bongo kwenye miondoko ya amapiano, zinaaminisha pombe ndio dawa sahihi ya msongo wa mawazo unaotokana na kuumizwa kimahusiano na mara chache kimaisha.
Baadhi ya wasanii wameliambia gazeti hili kuwa amapiano ni muziki unaochezwa zaidi sehemu za starehe kama baa na ndio sababu tungo zake nyingi zinagusia pombe, huku wengine wakisema ujumbe ni tatizo katika mitindo ya muziki Bongo na sio amapiano pekee.
Ikumbukwe muziki wa amapiano ulianza mwaka 2012 huko Gauteng, Afrika Kusini ila kumekuwa na mjadala ni wapi hasa asili ya muziki huo nchini humo, wapo wanaodai ulianzia katika vitongoji vya Johannesburg - Soweto na kisha kusambaa Afrika.
Mwimbaji wa Konde Music, Harmonize aliwahi kuwataka wasanii kupunguza nyimbo za pombe, jambo lililochochea ugomvi mkubwa kati yake na Rayvanny ambaye wakati huo alikuwa ametangaza ujio wa wimbo wake ‘Muongeze’ unaohusu pombe pia.
"Wasanii punguzeni nyimbo za pombe, msidhani hii nchi kila mtu ni mlevi, hata tunaokunywa siku ya Jumatatu hatunywi, tukizisikia nyimbo za pombe kama tunatonesha kidonda," alieleza Harmonize.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), matumizi mabaya ya pombe husababisha vifo milioni 3 kila mwaka, ikiwa ni asilimia 5.3 ya vifo vyote ulimwenguni kote, huku yakisababisha magonjwa zaidi ya 200.
Licha ya madhila na tahadhari kadhaa kutolewa na wataalamu kuhusu matumizi mabaya ya pombe, nyimbo za kutukuza pombe zinazidi kujichukulia umaarufu nchini. Hizi ni baadhi ya nyimbo chache tu za Bongofleva zenye mahadhi ya amapiano zinazozungumzia kinywaji hicho pendwa.
1. Marioo - Beer Tamu (2021)
Tunaweza kusema ndio amapiano ya kwanza Bongo iliyobeba ujumbe mkubwa kuhusu pombe na kupendwa na wengi. Marioo aliwashirikisha Tyler ICU, Visca na Abba ukiwa ni wimbo wake wa pili wenye mahadhi hayo kufanya vizuri baada ya ‘Mama Amina’.
Humo ndani Marioo hayupo tayari kuvurugwa kichwa na mpenzi wake wala kazini kwake wakati bia zipo, kwa nini akunje sura azeeke mapema wakati bia zipo, asikwambie mtu, bia tamu...
Wimbo huo ulishinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Wimbo Bora wa Mwaka.
2. Rayvanny - Sisi & Yaya (2023)
Hivi karibuni Rayvanny ameachia nyimbo mbili za amapiano, ‘Sisi’ na ‘Yaya’ ambazo zote zinasifia pombe na starehe. Kwenye ‘Sisi’ akimshirikisha DJ Joozey Rayvanny anasema; "Raha kulewa mbele za maadui zao, raha kulewa mbele za ma-ex wako."
Kwenye wimbo ‘Yaya’ aliwashirikisha Diamond Platnumz na Jux, ameeleza namna asivyokosa mkwanja wa kunywa hata iweje. "Najua nina madeni na matatizo ya kodi, ila pesa ya pombe na shisha sikosi... Wee Zombie jaza tena zikiisha, mwaga tano tano zidisha...
Hiyo ni baada ya Desemba 2022 Rayvanny na msanii aliyemsaini katika rekodi lebo yake, Next Level Music (NLM), Mac Voice kuachia wimbo, ‘Muongeze’ ambao nao unahamasisha unywaji pombe, huku wakitaja hadi chapa kubwa za pombe duniani.
3. Lava Lava - Tuna Kikao (2023)
Baada ya kuachia wimbo wake, ‘Tajiri’ ambapo ameelezea jinsi alivyokuwa anamsaka tajiri ili wakalewe, Lava Lava akaona haitoshi, akarudi studio kwa S2kizzy na kurekodi wimbo mwingine, ‘Tuna Kikao’ ambao kwa asilimia 100 unazungumzia pombe tu.
"Sisi ni walevi tunakesha baa, tunatumia hela mpaka juu lianze ng'aa." Lava Lava katika wimbo huo amemshirikisha Diamond Platnumz ukiwa ni wa tatu kufanya pamoja baada ya ‘Far Away’ na ‘Bado Sana’.
Staa huyo wa WCB Wasafi anaendelea kusema mambo ya muhimu kama kujenga nyumba watafanya mwakani, ila sasa cha kwanza ni heshima mezani, na kama pombe huziwezi meza yao haikufai, na wakishalewa jambo linalofuata ni kuhonga tu!
4. Phina - Do Salale (2023)
Mshindi huyu wa Bongo Star Search (BSS) 2018 katika wimbo wake mpya ‘Do Salale’ anasema baada ya kuachana na mpenzi wake anatamani kunywa pombe kuondoa mawazo ila wasiwasi wake ni kwamba akishalewa atajikuta matatani zaidi. Ni maneno ya mshindi huyo wa tuzo nne za TMA.
Humo ndani amelalama..."Natamani nilewe sasa nikilewa pombe nazo zinashuka chini, na mimi sina wa ubani nitafanya nini...
5. Jux - Enjoy (2023)
Ni wimbo wake Jux akimshirikisha Diamond Platnumz ukiwa ni wa pili kufanya pamoja, wanaamini kufurahia maisha kupitia unywaji wa pombe na starehe nyingine, ndio kitu pekee kilichobaki kwao baada ya kuumizwa na mapenzi.
"Napenda nikilewa, napanda juu ya meza, huku natema Kiingereza, tupande juu ya meza... Ya nini niteseke roho, jiunge nami upoze koo." kutoka katika wimbo, Enjoy ambao katika mtandao wa TikTok umefikisha watazamaji zaidi ya bilioni 1.
6. Ibraah - Addiction (2021)
Alimshirikisha Harmonize katika wimbo wake, ‘Addiction’ ambao kwa asilimia 100 wanazungumzia pombe jinsi inavyowasaidia kwenye baadhi ya mambo kama kuondoa msongo wa mawazo na inavyowaletea matatizo.
"Kwanza pombe ni dawa, ikiwa na msongo wa mawazo inakuweka sawa. Pombe sio kahawa, kama huziwezi usizidishe utapagawa...,”anahamasisha na kuonya Ibrah katika wimbo huo.
Wasanii wengine Bongo waliotoa nyimbo za amapiano na kuigusia pombe ni Mac Voice ft. Rayvanny (Pombe), Ril Vin X Billnass (Tit For Tat Remix), G Nako (Hiyo Hapo), Mboso (Moyo), Whozu (Sijui Nikoje), Anjella ft. Harmonize (Toroka), Marioo (Tomorrow) n.k.
Kauli ya wasanii
Mwimbaji wa Konde Music, Ibraah anasema wasanii kuimba pombe katika amapiano ni biashara nzuri inayowalipa.
"Kwa sababu amapiano ni muziki unaochezwa sana sehemu za starahe kama klabu na baa ambazo mara nyingi watu wanakunywa pombe, kwa hiyo nyimbo za namna hiyo wanazipenda kwa kuwa wanaona kama wameimbiwa wao.
"Ila siyo uimbe tu ilimradi amapiano umetaja pombe, hapana iwe bora kwa sababu ni biashara inayoingia sokoni ambako kuna ushindani," anasema Ibraah.
Anataja sababu ya nyimbo zinazohusu pombe kupata mapokezi mazuri ni kwa sababu hazikuwepo kwa wingi sokoni.
Utakumbuka hadi sasa Ibraah ametoa EP moja, Steps (2020) na albamu moja, ‘The King of New School’ (2022), katika orodha ya wasanii wa Tanzania waliopokea fedha nyingi za mirabaha kwa mwaka 2022 alikamata nafasi ya nne akikabidhiwa kitita cha Sh4.5 milioni.
Kwa upande wake Afande Sele ambaye kupitia wimbo wake ‘Darubini Kali’ (2003) alikemea wasanii kusifu ngono na pombe katika nyimbo zao wakati kuna mengi ya kuisemea jamii, anasema amapiano ni muziki mzuri ila ujumbe wa baadhi ya wasanii ndio tatizo.
"Kwenye ujumbe kuna shida bado, na sio katika amapiano tu ni aina zote za muziki Bongo, kama leo hii Hiphop haina ujumbe wowote wanajiimbia wao na sio jamii, pengine uwezo wa kufikiri kwa vijana umepungua," anasema Afande Sele.
Afande Sele anasema tungo nyingi zinaipoteza jamii, hilo linaweza kusababisha muziki wa amapiano kushindwa kuendelea kwa sababu hao wanaowaimbia hivyo leo kuna siku wataona huu ni ujinga na kuachana nao.
"Ila kama watakuwa na ubunifu kama ambavyo baadhi yao wanaonyesha kwamba wanaimba vitu hata kama ni vya kuburudisha havina ukakasi, nadhani wanaweza kufika mbali wakichanganya na vionjo kidogo vya nyumbani," anasema mkali huyo wa rhymes.
Naye Mchizi Mox, aliyevuma na wimbo wake ‘Chupa Nyingine’ (2009) unaohamasisha unywaji pombe, anasema "Pengine Taifa limekuwa na walevi wengi, na kawaida pombe huendana na muziki, hivyo tunaweza kusema walevi wamesogezewa huduma karibu," anasema Mchizi Mox, ambaye ni mmoja wa wasanii wa kundi la Wateule.
Msikie Daktari
Je, pombe inaweza kuwa ni suluhisho la msongo wa mawazo kama wasanii wanavyoeleza katika nyimbo hizi? Dk Joachim Mabula anasema inaweza kuwa suluhisho lakini sio la kudumu.
"Mtu anapokunywa anakuwa amepata pumziko la muda, ila kesho yake pombe inapokuwa imeisha hali yake inarudi palepale, hii ndiyo sababu unakuta mtu mwingine anakunywa kila siku ili kupata hiyo ahueni ya muda mfupi," anasema Dk Mabula.
Anasema msongo wa mawazo unaosababishwa na ukosefu wa fedha, ugumu wa maisha au mahusiano, suluhisho sio pombe, bali kutatua tatizo husika, kukubali matokeo, kuzungumza na wengine, kuwa na ratiba nzuri ya kazi, chakula na usingizi.