Arusha na mkakati wa kuwa kitovu cha utalii Afrika

Muktasari:

Licha ya changamoto zilizopo, Serikali inatamani kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kwa dhamira ya kukuza mapato yatokanayo na sekta hiyo hasa fedha za kigeni.
Novemba 7-9, wajumbe kutoka Bodi ya Utalii (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) na Tume ya Utalii Zanzibar (ZCT) pamoja na wawakilishi wa kampuni 42, walishiriki kwenye maonyesho ya utalii yaliyofanyika jijini London, Uingereza.

Michango ya wadau ni muhimu kufanikisha lengo la kuwa na sekta ya utalii; imara na yenye ushawishi kwa uchumi wa taifa na wananchi kwa ujumla.
Licha ya changamoto zilizopo, Serikali inatamani kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kwa dhamira ya kukuza mapato yatokanayo na sekta hiyo hasa fedha za kigeni.
Novemba 7-9, wajumbe kutoka Bodi ya Utalii (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) na Tume ya Utalii Zanzibar (ZCT) pamoja na wawakilishi wa kampuni 42, walishiriki kwenye maonyesho ya utalii yaliyofanyika jijini London, Uingereza.
Hii ni moja ya juhudi za kuhakikisha sekta hiyo inakua. Kufufuliwa kwa Shirika la Ndege (ATCL), licha ya mambo mengine, kumedhamiria kuutangaza utalii nje ya mipaka na kuvutia wageni wengi zaidi.
Rais John Magufuli wakati akizungumza na wahariri alisema baada ya muda mfupi ATCL itapata ndege saba ambazo kati yake baadhi zitakuwa zinaenda Ulaya, Marekani na China ili wageni wanaotaka kutembelea vivutio vya nchini wapate fursa ya moja kwa moja bila kupitia nchi nyingine.
Wakati haya yakifanyika, Arusha inaandaliwa kuwa kitovu cha utalii Afrika. Siyo jambo la ajabu, kwa wakazi wa jiji hili kukutana na mamia ya watalii mitaani kila mwaka. Licha ya uwepo wa vivutio vingi nchini lakini watalii wengi huwa wanafika Arusha, siyo kwa bahati mbaya bali kwa ratiba za safari zao, kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti au kupanda Mlima Kilimanjaro.
Zaidi ya watalii, 1,137,182 ambao walifika nchini mwaka jana  na kuliingizia taifa Dola 1.9 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh3.8 trilioni), asilimia 80 walipitia Arusha.
Vivutio hivi vitatu ambavyo vinafikika kwa urahisi kupitia Arusha ni miongoni mwa maeneo ya maajabu saba ya asili barani Afrika ambayo yamo kwenye orodha ya urithi wa duniani.

Kwa kupitia Arusha, watalii wanapata fursa ya kutembelea hifadhi za Tarangire, Manyara na Arusha hivyo umuhimu wa jiji hili kwenye sekta ya utalii ni mkubwa na ndiyo maana haikuwa ajabu Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alipoliita Geneva ya Afrika.

Alifanya hivyo, Agosti 2000, alipofika Arusha kwenye mazungumzo ya kusaka amani ya Burundi na kubaini tulivu jiji hili muhimu kwa Afrika.

Mchango wa sekta ya Utalii

Sekta ya utalii ni miongoni mwa zinazoongoza kwa kutoa ajira nyingi kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha ambako zaidi ya asilimia 40 ya wakazi wake wanautegemea.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii nchini (Tato), Siriri Akko anasema zaidi ya watu zaidi ya 8,000 wamejiriwa kwenye sekta hiyo pamoja na zaidi ya 80,000 ambao hufanyakazi ya kuongeza na kuwasaidia watalii wanaofika nchini.

Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo anasema Arusha ni mji muhimu sana kwa uchumi wa Taifa na kwa Watanzania wote.

Gambo anaeleza, wanaonufaika na utalii wa Arusha siyo wakazi wa jiji hilo pekee bali hata Serikali ambayo imekuwa ikipata asilimia 17 kwa mwaka ukiwa ni mchango sekta nzima kwenye Pato la Taifa hivyo kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo au utoaji wa huduma za kijamii kwa nchi nzima

Kutokana na ukweli huo, anasema ni lazima kuwepo na mikakati ya kuhakikisha Arusha inaboreshwa zaidi ili iwe kitovu cha utalii barani Afrika miaka michache ijayo.

Kutokana na unyeti na upana wake, anasema maboresho hayo hayawezi kufanywa na Serikali, mawakala wa utalii au mamlaka za hifadhi pekee bali kunahitajika jitihada za pamoja kutoka kwa wadau wote.

Anaeleza, lengo ni kupokea zaidi ya watalii milioni mbili kwa mwaka ambao watakaa Arusha wakiwa salama huku wakipata huduma zote muhimu bila usumbufu wowote na kulipa kodi zote zinazostahili.

Mipango

Ili kuiwezesha Arusha kuwa kitovu mpango wa kutatua kero pamoja na mikakati maalumu imeandaliwa na uongozi wa mkoa. Ofisa Utalii wa mkoa, Flora Assey anasema yapo mambo 28 ambayo wadau wamekubaliana kuyafanya ili kufanikisha lengo hilo.

“Tumekubaliana kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya jiji na maeneo jirani pamoja na kuwashirikisha wadau juu ya mabadiliko yoyote hasa ya kodi,” anasema.

Mengine yaliyoafikiwa ni kuimarisha vita dhidi ya ujangili, kuanzisha tovuti na kituo cha utalii Arusha bila kusahau kumaliza migogoro ya ardhi zaidi mipaka baina ya hifadhi na wananchi.

Assey anasema hayo yote yamepitishwa na kikao kilichowashirikisha wamiliki wa kampuni na waongozawatalii, watendaji wa hifadhi za taifa, Mamlaka ya Mapato (TRA) na Jeshi la Polisi.

Wengine walioshiriki ni Bodi ya Utalii (TTB), Chama cha Wamiliki wa Hoteli, wanahabari za utalii na wawakilishi wa utalii wa ndani na kitamaduni. “Kila jambo tulilokubaliana kuna taasisi imepewa jukumu la kulisimamia,” anasema.

Maadhimio hayo yamelenga kuboresha utamaduni wa kitalii ili kuongeza siku za wageni kukaa Arusha na kuanzisha matamasha ya filamu na kukabiliana na changamoto ya ongezeko la watu na mifugo maeneo ya hifadhi.

Ili kuongeza makusanyo ya Serikali kutokana na tozo zinazotozwa kwenye sekta hiyo, mkoa huo umejipanga kuondoa usumbufu katika ulipaji suala litakalofanyika sanjari na kuwatabua walipakodi wote na kuwa na alama maalum kwa magari ya utalii.

Licha ya kuimarisha ukusanyaji mapato, mkakati huo unahusisha kupunguza utitiri wa kodi zinazotozwa na Serikali za Mitaa, kuboreshwa maslahi ya waongoza watalii na kuboresha miuondombinu ya sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato), Willy Chambulo anasema mpango huo utahusisha ujenzi wa jengo ambalo taasisi na mamlaka zote za utalii zitakuwa na ofisi ili kupunguza muda wa kufuata huduma maeneo tofauti zilipo ofisi husika.

Kufanikisha hilo, anasema: “Tutakuwa na vikao kila baada ya miezi minne na kufanya tathmini ya ulinzi na usalama hotelini, kurahisisha upatikanaji wa vibali vya wawekezaji na kupunguza upungufu wa ndege za moja kwa moja kutoka Ulaya hadi nchini.”

Katibu Tawala wa mkoa, Richard Kwitega anasema: “Tutapunguza vizuizi na kuboresha ufuatiliaji wa fedha wanazolipa watalii kutoka maeneo yote yanayotambulika. Tutaainisha changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.”

Wadau hao wanaamini endapo masuala yote yatafanyiwa kazi Arusha itavutia zaidi ya watalii milioni mbili kwa mwaka na kutimiza ndoto ya kuwa kitovu cha utalii Afrika.