Balozi Mchumo ateuliwa mkurugenzi mkuu shirika la kimataifa

Muktasari:

  • Kutokana na historia na utumishi wake uliotukuka, Balozi Mchumo ameteuliwa kuongoza shirika la kimataifa linalohamasisha kilimo na matumizi endelevu ya mianzi. Tanzania ni miongoni mwa nchi 45 wanachama wa shirika hilo.

Aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Balozi Ali Mchumo ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la INBAR lenye makao makuu nchini China.

Kwa uteuzi huo, Balozi Mchumo ataliongoza shirika hilo lenye nchi wanachama 45 kwa miaka mitatu. Kwa mujibu wa taarifa ya INBAR, shirika linalohamasisha utunzaji wa mazingira, Balozi Mchumo ataanza kutekeleza majukumu yake kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.

“INBAR ina furaha kumkaribisha Balozi Ali Mchumo kuwa mkurugenzi mkuu wake wa tano. Balozi Mchumo anatoka Tanzania, nchi inayolima mianzi na moja ya waanzilishi wa shirika hili. Kwa uzoefu alionao tunaamini atasaidia kufanikisha malengo ya shirika,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ili kuwahudumia nchi wanachama walioinzisha mwaka 1997 Tanzania uikiwamo, INBAR ina ofisi za kikanda India, Ghana, Ethiopia na Ecuador.

Akimkaribisha China, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki amesema Mchumo anayo nafasi kubwa ya kulirejesha zao la mianzi kwenye umaarufu.

“Uteuzi wa Balozi Mchumo ni heshima kubwa kwa Afrika. Hii ni mara ya kwanza kwa Mwafrika kuchukua nafasi hiyo tangu taasisi hiyo ianzishwe. Tunaamini ubovevu wa Balozi Mchumo, INBAR itapata mafanikio makubwa chini ya uongozi wake. Ubalozi utashirikiana naye kwa karibu tukiwa kama wawakilishi wa nchi yetu katika taasisi ya INBAR,” alisema Mbelwa.

Mbelwa anaamini kupitia taasisi hiyo, Tanzania itaendelea kunufaika na teknolojia ya kuwezesha matumizi ya mianzi kupambana na umasikini.

Balozi Mchumo ni mwanasiasa mkongwe ambaye amehudumu kwenye nafasi mbalimbali nchini. Akiwa amezaliwa mwaka 1945 amehudumua kwenye nafasi tofauti kuanzia ubunge hadi uwaziri kabla ya kuwa balozi katika mataifa tofauti Afrika, Ulaya na Amerika. Ameshika nyadhfa tofauti pia kwenye mashirika ya kimataifa, kama la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), la biashara (WTO) na maendeleo ya biashara (UNCTAD) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kabla ya uteuzi huo, Balozi alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Bidhaa (CFC) wenye makao makuu jijini Amsterdam, Uholanzi.

Kati ya mwaka 2013 na 2015 alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF).