Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BIASHARA LEO : Saccos zishughulikie changamoto zilizopo kuboresha huduma zake

Hassani Mnyone

Muktasari:

  • Udumavu huu unatokana changamoto zinazovikabili Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) hivyo kutowanufaisha wanachama wake kwa kiwango kilichotarajiwa.
  • Ili kuyafikia malengo ya kuzinufaisha jamii za wananchi wanaokubaliana na mfumo huu, ipo haja kwa taasisi hizi ndogo za fedha kuchukua hatua stahiki kushughulikia changamoto hizo kwa wakati.

Licha ya umuhimu wake wa kuwakomboa wananchi kiuchumi, Saccos nyingi nchini zilizodumaa kwa kukosa mipango endelevu ari ya ushindani na taasisi za fedha.

Udumavu huu unatokana changamoto zinazovikabili Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) hivyo kutowanufaisha wanachama wake kwa kiwango kilichotarajiwa.

Ili kuyafikia malengo ya kuzinufaisha jamii za wananchi wanaokubaliana na mfumo huu, ipo haja kwa taasisi hizi ndogo za fedha kuchukua hatua stahiki kushughulikia changamoto hizo kwa wakati.

Kutokuwa na ubunifu kwenye bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi hizi ni miongoni mwa changamoto zinazorotesha ufanisi wake. Huduma za kuweka na kukopa zilizopo ni za kizamani zisizoendana na mahitaji ya wateja au spidi ya mabadiliko ya sayansi ya teknolojia.

Huduma hizi hazifanyiwi uboreshaji hivyo kuzifanya ziendelee kuwa duni kukidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Kutokuwa na wataalamu wa asasi ndogo za fedha ni changamoto nyingine inayohitaji kufanyiwa kazi. Ukosefu wa rasilimali watu wenye sifa na vigezo stahiki unadumaza Saccos nchini.

Taasisi hizi zinakosa wataalamu wa uongozi wa ushirika na asasi ndogo za fedha jambo linalozifanya zishindwe kukua vizuri na kuboresha huduma kutokana na kukosa ubunifu na ugunduzi kuanzia utawala, bidhaa na kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Kutegemea zaidi fedha kutoka nje kwa ajili ya kujiendesha kunadhohofisha nguvu ya taasisi kujitegemea katika utoaji huduma. Benki za biashara zimekuwa zikifaidika na nafasi hii kwa kutoa mikopo mikubwa kwa vyama hivi na kuibua migogoro mingi ambayo kwa kiasi kikubwa imevifanya vyama vyingi kuyumba.

Saccos zinahitaji kujijengea uwezo wa kifedha kwa kuandaa na kuweka mikakati ya kibiashara ambayo itasimama na kutoa dira ya kuwezesha vyama kufika mbali.

Vyama hivi vinapaswa kuepuka sasa badala yake vibuni miradi na huduma nyingi ili kujiwekea mizizi imara ya kibiashara. Kupokea na kutumia fedha kutoka nje siyo tatizo ila viongozi kubweteka kiasi cha kukosa dira ya kujiendesha.

Saccos hazitakiwi kuachwa nyuma na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Hii ni changamoto inayotakiwa kutafutiwa majibu ya haraka kutokana na vyama vingi kukosa mifumo ya kieletroniki inayohifadhi kumbukumbu za biashara kama vile miamala na taarifa muhimu za taasisi.

Taasisi nyingi zinatumia mafaili kutunza taarifa zao hivyo kuchelewesha huduma pale zinapohitajika. Kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa intaneti na umeme, hakuna haja ya kutotumia teknolojia kufanikisha shughuli za Saccos.

Vyama hivi pia vinahitaji mipango endelevu ya biashara ili kuwa na dira. Vyama vinahitaji kuwekeza kwenye utafiti utakaosaidia kubaini njia sahihi ya kuandaa mpango utakaoleza yanayoweza kufanyika kwenye masoko, ushindani, uongozi, mitaji na kunufaisha taasisi.

Ni jambo lililowazi kuwa taasisi za ushirika hazina mipango ya muda mrefu kibiashara hivyo kuhitaji wataalamu wa kutoa mwelekeo sahihi ili kufika mbali kiutendaji.

Taasisi hizi pia zinatakiwa kuacha kuendelea kutumia sera na sheria zilizopitwa na wakati kwenye utoaji wa huduma kwani haziakisi mabadiliko ya uchumi wa kisasa.