Chaumma yazindua operesheni ya 'Tujenge Pamoja' kuwafikia Watanzania
Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila akizungumza na Vyombo vya Habari.
Muktasari:
- Gharama za uendeshaji wa operesheni nzima, ambayo kwa awamu ya kwanza itatumia bajeti ya Sh186 milioni, zitategemea michango kutoka kwa wanachama wa chama hicho, wadau wa demokrasia pamoja na wapenda mageuzi.
Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimezindua operesheni mpya ya 'Tujenge Pamoja', itakayozunguka mikoa yote nchini kwa lengo la kukusanya rasilimali za kifedha za kuendesha chama, kufanya maboresho ya Katiba ya chama hicho na kuibua changamoto zinazowakabili wananchi.
Operesheni hiyo, itakayoongozwa na viongozi wa juu wa chama kupitia mikutano ya ndani, inatarajiwa kuanza Julai 25, 2026.
Ni utekelezaji wa maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika siku 21 zilizopita, ambacho, pamoja na mambo mengine, kilipitisha mpango mkakati wa uendeshaji wa chama kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Gharama za uendeshaji wa operesheni nzima, ambayo kwa awamu ya kwanza itatumia bajeti ya Sh186 milioni, zinatarajiwa kutegemea michango kutoka kwa wanachama wa chama hicho, wadau wa demokrasia pamoja na wapenda mageuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam, leo Jumanne Julai 21, 2026, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila, amesema operesheni hiyo itaanza kwa awamu ya kwanza mkoani Tabora Julai 25.
"Baada ya Tabora tutakwenda Katavi, Kigoma, Kagera, Mwanza, Simiyu, Singida, Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Pemba na kumalizia Unguja katika awamu ya kwanza," amesema Kigaila.
Amesema baada ya kukamilisha ziara katika mikoa hiyo, pamoja na baadhi ya majimbo, chama kitapanga ratiba ya kuanza awamu ya pili kulingana na kiwango cha rasilimali fedha kitakachokuwa kimekusanywa.
Amesema bajeti ya awamu ya kwanza ni Sh186 milioni, ingawa matarajio yao ni kwamba baada ya kuweka mpango huo hadharani, wanachama, wadau wa demokrasia na wapenda mageuzi watachangia chama hicho.
Kigaila amesema kaulimbiu ya operesheni hiyo, 'Tujenge Pamoja #NiSisi', inalenga kuhimiza ushirikiano wa Watanzania wote katika kujenga taifa.
"Tunaamini changamoto nyingi zinatokana na ubinafsi, hususan wa chama tawala, na mtazamo wa kuwaona wengine kama wageni. Tunaamini nchi inaweza kupata mwelekeo mzuri ikiwa tutajenga pamoja. Hata katika suala la Katiba mpya, ni lazima tukae pamoja na kujenga maridhiano," amesema.
Amesema chama hicho kimeamua kuachana na siasa za ubaguzi na kuamini kuwa Watanzania wote wanapaswa kushiriki katika kujenga mustakabali wa taifa.
"Hakuna mtu mwenye haki ya kipekee ya kumiliki Tanzania. Tatizo la ubinafsi halipo tu ndani ya chama tawala, bali hata katika baadhi ya vyama vya upinzani vinavyoamini vina umiliki wa ukweli na haki.
"Sisi tunasema Tanzania ni mali ya Watanzania wote, wenye vyama na wasiokuwa na vyama," amesema.
Kuhusu Katiba mpya, Kigaila amesema chama kimejipanga kuelimisha wananchi kuhusu ibara zinazohitaji kufanyiwa marekebisho.
"Tuna ramani ya Katiba inayoonesha ibara zenye changamoto na mapendekezo ya maboresho. Tutaanza pale tulipoishia kwa kuzingatia Katiba iliyopo pamoja na maoni ya Tume ya Jaji Joseph Warioba," amesema.
Namna ya kugharamia operesheni
Kigaila amesema operesheni hiyo itagharamiwa na wanachama wa chama pamoja na wadau wa mageuzi.
Amesema chanzo cha kwanza cha mapato kitakuwa ada za wanachama na michango ya usajili, huku viongozi wa chama wakitarajiwa kutoa michango yao.
"Tumekubaliana wabunge wetu wachangie, na tayari wameahidi kufanya hivyo. Leo tunaanza rasmi harambee ya kuchangisha fedha na tutaanza kuweka mkeka wa uchangiaji," amesema.
Amesema viongozi wakuu watano wa chama, wajumbe wa Kamati Kuu, Sekretarieti, viongozi wa mikoa 31 pamoja na viongozi wa majimbo 72 pia watachangia kufanikisha operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa Kigaila, michango yote itawekwa katika akaunti rasmi za chama na taarifa zake zitachapishwa kupitia kurasa za Chaumma Makao Makuu (Chaumma HQ).
"Tumeamua kwenda kwa umma kwa uwazi ili wanachama na wadau wajue namna ya kuchangia. Hatutaki fedha zikusanywe mikononi mwa watu kwa njia isiyo rasmi. Tutatoa taarifa wazi kuhusu kiasi kitakachokusanywa na namna kitakavyotumika," amesema.
Amesema mkakati wa kukusanya michango haujaigwa kutoka chama chochote cha siasa.
"Hakuna chama chenye hati miliki ya kuchangisha fedha. Kila chama kina haki ya kufanya hivyo, mradi kieleze malengo ya michango hiyo," amesema.
Amesema operesheni itaendelea hata kama kiwango cha michango kitakuwa kidogo kuliko matarajio.
Mikutano ya ndani
Akizungumzia zuio la mikutano ya hadhara, Kigaila amesema chama kinatambua changamoto za kisheria zilizopo, hivyo kimeamua kutumia mikutano ya ndani kuwafikia wananchi.
"Tutafanya vikao vya ndani ili wanachama watoe maoni kuhusu maboresho ya Katiba ya chama, wajadili changamoto za maisha wanazokumbana nazo na masuala mengine ya maendeleo ya taifa. Hatutafanya mikutano ya hadhara kwa sasa," amesema.
Amesema chama kitaendelea kufanya shughuli zake za kisiasa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
"Chaumma kina mpango kazi wa mwaka huu ambao lazima utekelezwe. Tukiruhusiwa mikutano ya hadhara tutaifanya, lakini kwa sasa hatuwezi kusimamisha shughuli zetu za kisiasa," amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema, amesema chama kimejipanga kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa yaliyopo.
"Hakuna kosa kubwa la kisiasa kama kusubiri mshindani wako akufungulie mlango. Asipofungua hadi mwaka 2030 utafanyaje? Tutatumia njia zote halali kuhakikisha tunawafikia Watanzania," amesema Mrema.