Prime
Chaumma bado hakujapoa, makatibu…
Muktasari:
- Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinaendelea kukumbwa na mivutano ya ndani baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Salum Mwalimu, sasa mgogoro ukihamia kwa makatibu wa mikoa wanaorushiana tuhuma kuhusu uhalali wa uamuzi huo.
Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinaendelea kukumbwa na misukosuko ya ndani, mgogoro ulioanza kwa kuondolewa kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Salum Mwalimu, ukihama kutoka vikao vya juu vya uongozi hadi kwa makatibu wa mikoa, hali inayoashiria mvutano huo bado unakikumba chama hicho.
Hatua hiyo imekuja baada ya makatibu wa mikoa 20 wa chama hicho kujitokeza hadharani kuunga mkono uamuzi wa Halmashauri Kuu wa Juni 30, 2026 wa kumuondoa Mwalimu madarakani, huku wakitoa onyo kwa viongozi wanaodaiwa kuendeleza masilahi binafsi na kuchochea migogoro ndani ya chama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatatu Julai 13, 2026, makao makuu ya chama hicho, Biafra, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Makatibu wa Mikoa wa Chaumma, Bazili Lema amesema chama kinataka kujenga sura mpya ya siasa za ushindani badala ya za maigizo.
"Chama kinataka kivue taswira ya siasa za maagizo na kujenga chama imara chenye ushindani wa kweli katika siasa," amesema.
Kauli hiyo imekuja wakati ambao bado kuna makundi ndani ya chama yanayopinga namna Mwalimu alivyoondolewa madarakani huku makatibu wa mikoa wa Manyara, Tabora, Morogoro na Njombe wakidai awali kuwa hatua hiyo haikufuata taratibu za katiba ya chama.
Hata hivyo, Bazili amesema viongozi hao walitoa msimamo bila kuwa na taarifa kamili za yaliyojadiliwa na kuamuliwa katika Halmashauri Kuu.
Amesema Katiba ya Chaumma ya mwaka 2012, toleo la 2024, kupitia ibara ya 53 (r), inaipa Halmashauri Kuu mamlaka ya kuthibitisha au kusimamisha uteuzi wa Katibu Mkuu, huku ibara ya 69 ikielekeza namna ya kukaimisha nafasi hiyo pale inapobaki wazi.
Kwa mujibu wa Bazili, baada ya Mwalimu kuondolewa, Halmashauri Kuu ilimteua Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, kuwa Kaimu Katibu Mkuu kwa kuwa Mwalimu anatokea Zanzibar, hivyo hatua hiyo ilikuwa inaendana na masharti ya Katiba ya chama.
Kuanza kwa mgogoro
Mgogoro huo ulianza rasmi Juni 30, 2026 baada ya Halmashauri Kuu ya Chaumma kupiga kura ya kutokuwa na imani na Salum Mwalimu na hivyo kusimamisha uteuzi wake kama Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa tamko la pamoja la makatibu wa mikoa 20, ambao wanawakilisha zaidi ya asilimia 68 ya makatibu wote wa mikoa wa chama hicho, Mwalimu aliondolewa baada ya vikao vya chama kuthibitisha tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili.
Miongoni mwa tuhuma hizo ni madai ya ubadhirifu wa fedha za wadau wa chama, kukibambikia chama deni la takribani Sh197 milioni, kutumia fedha za chama nje ya utaratibu rasmi, kuendesha chama bila kuwashirikisha viongozi wengine na kubadili maamuzi ya vikao halali vya chama kwa matakwa yake binafsi.
Akisoma tamko hilo, Bazili amesema kabla ya uamuzi wa mwisho kufikiwa, Mwalimu alipewa nafasi ya kujieleza katika Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu, ambapo pamoja na kujitetea aliwasilisha nyaraka mbalimbali, zikiwamo zile zinazodai kuwa chama anakidai kiasi cha takribani Sh197 milioni, madai ambayo viongozi hao wanayaita yasiyo na msingi.
Aidha, kufuatia tuhuma hizo, Mwalimu aliandika barua kwa Mwenyekiti wa chama hicho, akiomba kupisha uchunguzi dhidi yake na baadaye Halmashauri Kuu ya Chama hicho ikaridhia kutenguliwa kwake.
Wakati Bazili akisema hayo, kwa upande wao, Makatibu wanne wa mikoa ya Njombe, Tabora, Manyara na Morogoro wanaotuhumiwa kukihujumu chama, wao wamesisitiza kuwa msimamo wao si kuunga mkono kuondolewa au kutoondolewa kwa Mwalimu, bali wanataka uchunguzi ufanyike kuhusu tuhuma alizohukumiwa nazo ili hatua stahiki zichukuliwe
Mwananchi limezungumza na Edward Msabaha, Katibu wa Chaumma Mkoa wa Tabora ambaye kwa niaba ya makatibu hao amefafanua kuwa katika kikao chao cha Julai 10, 2026, makatibu hao wanne walitoa tamko la wito wa uchunguzi dhidi ya tuhuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wao.
"Sisi hatuungi mkono kuondolewa na hatumtetei Katibu Mkuu, bali tunataka uchunguzi huru dhidi ya tuhuma zake," amesema.
Amefafanua kuwa, kuondolewa kwa Katibu Mkuu hakukufuata taratibu za chama akibainisha kuwa alipaswa kuondolewa na Baraza Kuu la chama pekee.
"Tuhuma zake zikishathibitishwa awajibishwe kwa mujibu wa sheria kwani kikao kilichomuondoa hakina mamlaka hayo isipokuwa Baraza Kuu la chama pekee," amesema.
Katika maelezo yake, Msabaha ameeleza kutotambua mamlaka ya Bazili kama Mwenyekiti wa Makatibu wa mikoa kama anavyojitambulisha, akisema ni nafasi ya muda aliyopewa katika kikao maalumu na Katibu Mkuu Juni, 2026 ambayo iliishia hapo na si nafasi yake ya kudumu anayotambuliwa nayo ndani ya chama.
Katika hatua inayoonesha fukuto linaendelea kukitesa chama hicho, Bazili katika tamko la makatibu 20 amefafanua hakuna msingi wa madai hayo kwa kuwa vikao vya chama vilifuata taratibu zote za kikatiba na kwamba iwapo Mwalimu hajaridhika na uamuzi huo, katiba ya chama imeweka utaratibu wa kukata rufaa.
Katika hatua nyingine, Bazili amewatuhumu baadhi ya viongozi wanaopinga uamuzi huo kuwa wanatumika na watu wenye masilahi binafsi wanaotumia fedha kuendeleza mgogoro.
Amehoji namna makatibu hao wa mikoa minne walivyokutana jijini Dar es Salaam kutoa tamko la pamoja, akidai chama kina taarifa za watu waliowaratibu na kugharamia mkutano huo.
"Huu ni mchezo wa watu wanaotaka kuibua migogoro ili kudhoofisha harakati za ukombozi. Tunaacha kujadili katiba mpya, ulinzi wa rasilimali za nchi na masuala mengine muhimu, tunajadili nani ameondolewa ofisini," amesema.
Bazili ameongeza kuwa chama hakitakuwa tayari kuvumilia viongozi wanaotanguliza masilahi binafsi au wanaokiweka chama katika mazingira ya migawanyiko.
Amesisitiza lengo la Chaumma kwa sasa ni kurejesha imani ya wanachama, kuimarisha harakati za kisiasa na kuhakikisha chama kinaingia katika ushindani wa kisiasa kikiwa na umoja.
Akifafanua kuhusu nafasi yake, Bazili amesema aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa makatibu wa mikoa wa chama hicho ili kurahisisha uratibu na utendaji wa shughuli za makatibu wa mikoa nchini, akiwa Katibu wa Mkoa wa Kilimanjaro.