BIASHARA LEO : Benki ya Taifa ya Ushirika itasaidia kuimarisha biashara
Muktasari:
- Kuna ulazima wa kuifanya sekta hii na wadau wake kuendana na kasi ya maendeleo kwa kuanzisha ‘Benki ya Taifa ya Ushirika’ itayowapa nafasi wana ushirika kujidai kwa kutumia huduma za kisasa za fedha kutoka kwenye taasisi yao binafsi na kuongeza ushindani kwenye sekta ya fedha nchini inayotawaliwa na benki nyingi za biashara.
Ushirika ni sekta inayoweza kuchangia mapinduzi kwenye sekta fedha, kilimo na uchumi kwa ujumla kutokana na kuhudumia watu wengi kupitia vyama vya kilimo na masoko (Amcos) na vile vya kuweka na kukopa (Saccos).
Kuna ulazima wa kuifanya sekta hii na wadau wake kuendana na kasi ya maendeleo kwa kuanzisha ‘Benki ya Taifa ya Ushirika’ itayowapa nafasi wana ushirika kujidai kwa kutumia huduma za kisasa za fedha kutoka kwenye taasisi yao binafsi na kuongeza ushindani kwenye sekta ya fedha nchini inayotawaliwa na benki nyingi za biashara.
Ili kuipata benki hiyo, kutokana na matakwa ya sheria za Bbenki na taasisi za fedha na zile za Benki Kuu ya Tanzania (BOT), mtaji unaohitajika unaweza kufika Sh15 bilioni ambazo ni kubwa kama tutatumia njia ya kutembeza bakuli ili kupata mtaji huu.
Ni muhimu basi kutengeneza msingi imara kuanzia chini kwenye vyama vya msingi kabla kufika huku juu kwa kutengeneza mfumo mzuri wa benki za ushirika kikanda ambazo hizo ndizo zitakuwa njia ya kusaidia kukuza mtaji huu unaohitaji kuweka akaunti Benki Kuu.
Ipo Benki ya Ushirika Kilimanjaro na Kagera hivyo zinatakiwa ziongezeke nyingine kutoka Kanda ya Kusini mfano mkoani Mtwara, Kati hasa pale Dodoma na maeneo mengine kama Mbeya kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Tukiwa na benki za kanda walau sita itasaidia kupatikana kwa mtaji mkubwa kwa haraka na kuwezesha kutengeneza taasisi inayomilikiwa na wananchi wa kawaida iliyoundwa kwa mfumo unaonekana na unaoeleweka, na wenye nguvu.
Benki hii itakuwa na uwezo wa kuhudumia benki za ushirika za kanda na zenyewe zikaendelea kufanya kazi na vyama vidogo vilivyopo mikoani, wilayani na maeneo mengine, na mzunguko huu utaleta faida kubwa na wa haraka. Tukifanikiwa kupata benki kuu ya ushirika tutakuwa na uhakika wa vyama vidogo vya msingi kupata mikopo mikubwa kwa wakati ambayo itatumika kwenye shughuli za kilimo cha kisasa kwa kutumia vifaa vizuri na vikubwa kutokana na uwapo wa mtaji wa kutosha na uhakika.
Lakini, vyama vya kuweka na kukopa vinaweza kunufaika kwa kupata mikopo nafuu yenye masharti rahisi na rafiki ili kukabiliana na changamoto ya ukwasi wakati wateja na wanachama wanapohitaji kwa haraka mikopo ama kutoa fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Benki hii itakuwa chachu ya kuifanya sekta ya fedha hasa vyama vya kuweka na kukopa kutumia teknolojia na njia rafiki zinazokwenda na wakati kwa wanachama wake kwa kutengeneza mtandao ambao unaweza kuruhusu kupatikana huduma za fedha mahali popote kwa mifumo rahisi na haraka.
Mifumo hiyo inaweza kuwa ATM (Automated Teller Machines) na mingine kama vile matumizi ya simu za mkononi na intaneti vitu ambavyo wateja wa vyama vya ushirika wanaviona na kuvisikia kwa wateja wa taasisi nyingine za fedha.
Itachangia kuimarika kwa uchumi wa viwanda kupitia vyama vya ushirika ambavyo vingi vinafanya uzalishaji wa malighafi kutoka shambani. Tukiwa na benki ni rahisi kukopa na kupata mtaji kwa ajili ya mitambo na kutumia malighafi hasa za ndani kutengeneza bidhaa nzuri na kuzitafutia soko hata la kimataifa, hii itaongeza thamani ya kilimo kwa mtu mmoja na chama kwa ujumla.
Ushirika ni biashara kubwa na yenye uhakika kutokana na kuwa na watu wengi. Tutumie nafasi hii kutengeneza biashara imara ya fedha yenye nguvu itakayoleta mapinduzi kwenye ushirika kama sekta na kuleta ushindani mkubwa kwa benki kubwa za biashara.
Tukifika huku basi ujasiriamali wa kilimo, ufugaji, elimu za biashara na fedha utakuwa umefikishwa karibu na kundi kubwa lenye uhitaji wa kweli na kuusukuma kwa kasi uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa letu kwa ujumla.