Kukosekana soko la maziwa wafugaji wapasua vichwa
Muktasari:
Kilio cha wafugaji wa Kinondoni kinafanana na cha wafugaji wengine nchini Tanzania. Wakati wafugaji hao wakilalamikia soko la maziwa, kuna maeneo mengine watu wanahitaji maziwa lakini hawayapati.
Kilio cha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, ni ukosefu wa soko la maziwa. Wanafuga ng’ombe lakini hawana uhakika wa soko lake, wanauza kwa rejareja katika mitaa wanayoishi. Wanasema wakati mwingine wanalazimika kuyamwaga wanapokosa soko.
Kilio cha wafugaji wa Kinondoni kinafanana na cha wafugaji wengine nchini Tanzania. Wakati wafugaji hao wakilalamikia soko la maziwa, kuna maeneo mengine watu wanahitaji maziwa lakini hawayapati.
Kwa mfano, katika maeneo mengi ya mijini na vijijini ni rahisi kupata kinywaji kama soda na juisi, lakini ni vigumu kukuta maziwa.
Hivyo, pamoja na umuhimu mkubwa kiafya wa maziwa kwa binadamu, watu wengi wamejikuta wakinywa vinywaji hivyo kwa sababu ndiyo vinapatikana kwa urahisi.
Wakati wafugaji hao wakitafuta soko la maziwa, takwimu za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) zinaonyesha unywaji wa maziwa nchini ni wastani wa lita 47 kwa mtu mmoja kwa mwaka, wakati Shirika la Chakula Duniani (FA0) linapendekeza lita 200 zinywewe kwa mtu mmoja kwa mwaka.
Kwa upande wa Kenya, unywaji wa maziwa ni wastani wa lita 120 kwa mtu mmoja kwa mwaka wakati Uganda ni wastani wa lita 50 kwa mtu mmoja.
Takwimu hizo zinaonyesha unywaji wa maziwa Tanzania uko chini ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Wenzetu Kenya unywaji wa maziwa ni zaidi ya nusu ya idadi ya lita zilizopendekezwa na Fao. Tanzania ni ya tatu barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe ikitanguliwa na Ethiopia na Sudan.
Wakati Tanzania ikiwa na jumla ya ng’ombe milioni 28, lakini ina idadi ndogo ya ng’ombe wa maziwa wanaofikia 782,000.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) zinaonyesha Kenya ina ng’ombe wa maziwa 5 milioni ikiizidi Tanzania kwa zaidi ya ng’ombe 4 milioni.
Kuanzishwa mtandao
Kutokana na changamoto hiyo, wafugaji wa Wilayani Kinondoni wameamua kuanzisha Mtandao wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa utakaowaweka pamoja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Katibu Mkuu wa mtandao huo, Faustine Mbassa anasema kuna changamoto ya kuwapata wateja wanaohitaji maziwa.
“Kwa kweli kuna wakati tunalazimika kumwaga maziwa kwa kukosa wa kumuuzia,” anasema.
Anasema ndiyo maana wameanzisha mtandao huo ili wawe na umoja katika kutafuta masoko ya maziwa.
Anasema pamoja na kwamba uzalishaji wa maziwa kwa Tanzania uko chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, bado maziwa yanakosa soko.
“Tukiwa na mtandao wa wauzaji wa maziwa tutafikia hatua ya kuyauza kwa pamoja,”anasema.
Changamoto nyingine ni upatikanaji wa chakula cha mifugo ambacho bei yake ni kubwa pamoja na gharama za dawa za mifugo.
“Gharama hizi husababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa na hivyo kushindwa kufuga kwa faida,” anasema.
Mfugaji wa Mbezi Beach, Betweli Mollel anasena changamoto nyingine ya wafugaji ni ugumu katika utekelezaji wa Sheria ya Ufugaji Mijini na Vijijini.
“Sheria hii inataka kila kaya kufuga ng’ombe wanne tu. Sasa ng’ombe wakizaa ndama tunafanyaje tuwaue au tufanyeje kwa sababu watakuwa wamezidi idadi,” anasema.
Changamoto nyingine ambayo wanataka itatuliwe kupitia mtandao huo, ni upatikanaji wa mbegu bora ya ng’ombe ili waweze kutoa maziwa ya kutosha.
Ombi kwa serikali
Mwenyekiti wa mtandao huo, Joakim Lyaupe anasema mtandao huo wenye muungano wa vikundi 13 vyenye wanachama 261, wanaiomba Serikali wilayani huo kuwapa eneo la wazi kwa ajili ya kuuzia maziwa.
“Tunauza maziwa kwa mtu mmoja mmoja mitaani, tukipata eneo la wazi la kuuzia maziwa wananchi watafahamu wapi wafuate bidhaa hii, tutakuwa tumejitangaza,” anasema.
Anasema kwa kuwa wakipata eneo itawasaidia kupata soko la maziwa kwa bei nzuri. Kwa sasa maeneo mengi maziwa yanauzwa kwa Sh2,000 kwa lita.
Anaiomba serikali kuongeza idadi ya maofisa ugani waweze kutoa huduma ya elimu kwa wafugaji. Kwa mujibu wa viongozi wa mtandao huo, maofisa ugani bado ni wachache ikilinganisha na idadi ya watu wengi wanaowahudumia.
Licha ya uchache wao pia maofisa hao hawana vitendea kazi ukiwamo usafiri wa kuwawezesha kuwatembelea wafugaji wengi zaidi.
Bodi ya Maziwa
Uzalishaji wa maziwa ni lita bilioni 2.1 kwa mwaka, asilimia 70 ya maziwa yanatoka kwa ng’ombe wa asili.
Kaimu Msajili wa TDB, Mayasa Simba anasema Tanzania ina ng’ombe wa maziwa 782,000 kati ya ng’ombe milioni 28 waliopo. Anasema lengo ni kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya ng’ombe wa maziwa hadi kufikia milioni 1.5.
Kuhusu soko la maziwa, anasema bodi inahamasisha wafugaji kuanzisha mitandao itakayowawezesha kuwa na soko la maziwa la pamoja.
“Mitandao hii imeshaanzishwa katika baadhi ya wilaya na mikoa, lengo ni kuwa na sauti ya pamoja katika kukabiliana na changamoto,” anasema.
Anasema wanapokuwa pamoja jamii itafahamu kwamba wao ndiyo wauzaji wakuu wa maziwa hivyo watapata soko. Bodi hiyo imekuwa ikihamasisha wananchi kujenga tabia ya kunywa maziwa.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Happy alikubali ombi la kuwapatia eneo la wazi kwa ajili ya kuuzia maziwa lakini akawataka wapeleke maombi rasmi.
Anawataka wafugaji hao kumwandikia barua mkuu wa wilaya wakiainisha eneo wanaloliomba. “Hili ni jambo linalowezekana, niandikieni rasmi kuomba eneo la wazi mnalolihitaji,” anasema.
Mkuu wa wilaya anawataka wafugaji kulinda mtandao huo kwa kuwa utawasaidia kuwainua kiuchumi.