Dully Sykes: Kazi yangu kupagawisha

Dully Sykes

Muktasari:

Mashabiki wake wanamwita Dully Sykes na ndiyo jina lake la jukwaani wakati akisaka tonge, lakini jina kamili alilopewa na wazazi wake anaitwa Abdulwaheed Sykes.

Unaweza kumwita mburudishaji badala ya msanii kutokana na aina ya muziki anayofanya, nyimbo zake nyingi ni za kucheza na siyo kusikiliza.

Mashabiki wake wanamwita Dully Sykes na ndiyo jina lake la jukwaani wakati akisaka tonge, lakini jina kamili alilopewa na wazazi wake anaitwa Abdulwaheed Sykes.

Dully anaeleza sababu zinazomfanya aimbe muziki unaochezeka na kuachana na mashairi ya kubembeleza ni kutokana na mabadiliko ya muziki kwa sasa.

Alisema siku za nyuma watu walikuwa wanakwenda kwenye majumba ya starehe kusikiliza muziki au kumuangalia msanii anafanya nini jukwaani.

Alifafanua kuwa hivi sasa kila shabiki anataka kucheza zaidi kuliko kusikiliza, hata aliyeko nyumbani anafanya hivyo.

Alisema muziki umebadilika wakati wa albamu ingekuwa rahisi kuimba muziki wa mashairi na kubembeleza, “Hatutoi albamu, kwa hiyo hakuna anayesikiliza muziki sebuleni akiwa amekaa, mashabiki wangu vijana na wanataka kujirusha kazi yangu moja tu kuwarusha na ninaona nafanikiwa, “alisema Dully.

Baadhi ya nyimbo za Dully ambazo zikipigwa klabu ni fulu shangwe ni pamoja na Bongofleva, Beberon, Shikide, Mtoto wa Kariakoo na Togola.

Mbali na kupiga muziki wa kuburudisha zaidi Dully alisema kuwa anajipanga kama kufanya kolabo na wasanii wakongwe a nchini Kenya akiwamo Amani.

“Sifanyi kolabo kwa kuiga, nafanya kwa sababu maalumu na sasa ninayo, kuna wasanii wanaotakiwa kujivunia kuwapo kwenye fani kwa muda mrefu kama mimi akiwamo Amani wa nchini Kenya, Jose Chameleone wa Uganda, nikiweka mambo yangu sawa nitafanya nao kazi moja ya kujipongeza kwa kulimudu gemu la muziki, “alisema Dully Sykes.

Dully alisema kuwa silaha kubwa ya kudumu kwenye muziki kwa muda mrefu bila kuchuja ni kutoa wimbo mmoja kila mwaka na kuacha mashindano ya kutoa nyimbo bila kuwa na malengo maalumu.

Alisema haoni haja ya kutoa nyimbo mfululizo ilihali tayari ni maarufu na muziki anaufahamu, anaacha mashabiki waburudike na ngoma kwa muda huku akitumia nafasi hiyo kujipanga na kuja na kitu kingine kitakachomuweka juu.

Alifafanua kuwa akitoa wimbo kila mara mashabiki zake watamchoka na kama binaadamu anaweza kuteleza akatoa kazi isiyokuwa makini, kitu ambacho hataki kitokee.

“Kama unavyofahamu nina studio, mashairi natunga mwenyewe, hivyo sina sababu inayonifanya nitoe wimbo kwa mwaka mara moja zaidi ya kutaka mashabiki wangu watarajie ujio mpya na wa maana, huku wakifurahia nyimbo iliyotangulia kwa mwaka mzima, “alisema Dully.