Kwa mtindo huu elimu yetu inaangamiza ubunifu

Muktasari:

  • Kuanzia mwaka 1982 hadi 1986, nilichukua masomo ya kuelekea shahada ya uzamivu katika chuo kimoja huko Marekani.

Kuanzia mwaka 1982 hadi 1986, nilichukua masomo ya kuelekea shahada ya uzamivu katika chuo kimoja huko Marekani.

Kabla ya hapo nilikuwa nimehitimu shahada ya kwanza katika falsafa na pia shahada katika shahada ya pili.

Kama ilivyo kawaida katika harakati za kuelekea shahada hiyo ya juu kabisa katika elimu, nilipaswa kufanya utafiti wa kina na hatimaye nilifaulu kuandika kurasa 1,074 za utafiti niliofanya huko Marekani, Kenya na hapa Tanzania.

Nilishangaa kwamba niliweza kuandika utafiti wa kiwango hicho cha kurasa, lakini walimu wangu hawakushangaa. Waliniambia kwamba nilikuwa na kipaji cha kuandika tangu nilipozaliwa, lakini mtindo wa elimu nilioupitia hadi kufika huko haukunisaidia kutambua au kuendeleza kipaji hicho.

Hivyo kwa muda mrefu nimekuwa natafakari kuhusu mfumo wetu wa elimu, ili nione kwa vipi unasaidia wanafunzi watambue vipaji walivyo navyo na mpaka sasa sijaona ni mikakati ipi au ni mitalaa gani inawasaidia wanafunzi wafikie hatua hiyo. Bado sijaona.

Hivi majuzi nilisoma maandishi ya mbobezi wa elimu Ken Robinson (1950-2020) kuhusu mhadhara alioutoa mwaka 2006 huko California, Marekani aliuita kwa jina la: Je, shule zinaua ubunifu? (Do schools kill creativity?)

Maelfu wa watu walisikiliza mhadhara huo na baadaye maelfu kama si mamilioni ya watu duniani waliendelea kusoma ripoti ya mazungumzo hayo. Hoja kuu katika mhadhara huo ni kwamba kila mmoja wetu amezaliwa na vipaji vya ajabu, lakini baada ya kuhitimu masomo, wahitimu wamekuwa wakipoteza vipaji hivyo au vimesinyaa ndani yao kwa vile elimu tuliyo nayo haimsaidii mwanafunzi kufahamu na kuendeleza vipaji alivyo navyo.

Huu mfumo duni wa elimu upo katika nchi nyingi duniani, ijapokuwa zipo nchi nyingine kama Finland, Japan, na Korea ya Kusini ambazo zimeachana na mtindo huu wa elimu unaoua vipaji au kufanya visinyae.

Watu wengi waliosikiliza mhadhara huo walikubaliana na Ken Robinson asilimia 100, mimi nikiwa mmojawapo. Wasomaji zaidi ya milioni 300 duniani wameufuatilia mhadhara huo mtandaoni.

Tunavyoua vipaji

Kwa upande wangu, mara baada ya kumaliza kuandika utafiti wangu wa shahada ya uzamivu, nilianza kutambua kwamba elimu tuliyo nayo husaidia kuua vipaji vya wanafunzi hasa kwa kutojua.

Maandishi matakatifu yanasema: Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Na hivyo kwa kukosa maarifa ya uwepo wa vipaji katika kila mwanadamu, elimu yetu hutuangamiza kwa kutotusaidia kufahamu na kuendeleza vipaji vyetu.

Katika utafiti wa shahada ya uzamivu niliyoandika kwa kurasa 1074. Unaweza kujaza vitabu vitano kila kimoja chenye kurasa 200. Walimu wangu wakaniambia kwamba nilizaliwa na kipaji cha kuandika, lakini sikukitambua na mfumo wa elimu niliopitia kuanzia 1954 (chekechea) haukunisaidia kutambua kipaji hicho.

Nimegundua kwamba ninavyo vipaji vingine pia kama muziki, kuimba, kuhamasisha wasikilizaji, ukulima, ualimu, na vingine, lakini mfumo wa elimu niliopitia haujanisadia kuvitambua hadi hapo nilipoandika matokeo ya utafiti wangu.

Kuna hadithi ya kweli ya binti mmoja huko India aliyekuwa mbobezi wa kuimba na kucheza dansi kiasi cha kufikia ufahari wa kuwa mcheza dansi namba moja katika taifa hilo. Baadaye alipata ajali na akapoteza miguu yote miwili.

Kila mmoja akaamini kwamba binti huyo hangeweza kucheza tena dansi. Lakini yule binti alipata miguu bandia akaanza kufanya mazoezi ya dansi. Muda si mrefu akafikia tena kuwa namba moja katika taifa hilo.

Kumbe kipaji cha kuimba na kucheza hakikuwa miguuni kwake, kilikuwa rohoni mwake. Vipaji vipo rohoni kisha huratibiwa na akili na kujionyesha kupitia miili yetu.

Ndio maana mwanafalsafa Martin Heidegger (1889-1976) anasema: Binadamu si kwamba ana vipaji: yeye mwenyewe ni vipaji. Ni kama kusema ukimwona mtu, unaangalia mlundikano wa vipaji ndani yake.

Na ndio maana tunaona watoto wasio na mikono wanaandika kwa kutumia miguu yao au midomo yao. Tumeona watoto waliofukuzwa shule kwa kutotaka kusoma wakiwa baadaye wanamuziki wa kutisha. Tumeona wafanya biashara wakubwa kama Bill Gates ambao hawakumaliza shule.

Mifano ni mingi. Turudi tena kwa utafiti nilioufanya kati ya 1982 na 1986. Sijakoma kushangaa kwamba niliandika kuhusu mtu anavyoweza kutambua na kuendeleza vipaji vyake.

Baada ya kumaliza utafiti huo na kupata shahada ya uzamivu mwaka 1986, nimeendelea kuandika na mpaka sasa nimeandika vitabu vitatu na cha nne kipo mbioni kuchapishwa mwaka 2023, na cha tano kipo kinaiva akilini mwangu.

Kuanzia 2021 hadi leo nimeandika makala 83 katika gazeti letu la Mwananchi, na sioni ukomo wa kuendelea kuandika. Hebu fikiria taifa letu lenye watu milioni 61.7 sasa hivi, kama wengi wetu tungetambua vipaji vyetu taifa hili lingefikia wapi?

Kinyume chake tunashuhudia wahitimu wa vyuo vikuu maelfu kwa maelfu ambao hawana ajira. Huu ni ushahidi tosha kwamba mfumo wetu wa elimu umeua vipaji vyao na sasa wanazunguka mitaani kutafuta ajira.

Hawa wanaotafuta ajira wana vipaji ambavyo vimeuwawa shuleni kiasi cha mhitimu kujiona kwamba hana uwezo wa kujipatia kipato kwa kutumia vipaji vyake.

Ukimwona huyu mhitimu wa chuo kikuu ukamuuliza: wewe una kipaji gani? Wengi watasema hawajui wana vipaji gani. Inasikitisha! Mbona huko Burkina Faso mtoto akizaliwa wakunga wanamwuliza: umetuletea nini?

Maana ya swali hili ni kwamba: wewe mtoto uliyezaliwa sasa hivi una vipaji umevileta na ni jukumu la familia na jamii kuvitambua na kuvikuza hivyo vipaji vyake, ili baadaye vimjenge yeye na jamii yake.

Tuna vipaji si kwa ajili yetu tu, bali kwa lengo la kujenga familia zetu na taifa letu. Hivyo tufanye nini? Kwanza sisi wote tuamke usingizini tutambue kwamba kila mtoto anayezaliwa ana vipaji vyingi na ni jukumu letu kama jamii na kama mfumo wa elimu kumsaidia huyu mtoto avitambue na aviendeleze vipaji vyake.

Kisha tuanze mapinduzi makubwa katika vyuo vya ualimu ili walimu wapya wajue wajibu wao wa kuwasiadia wanafunzi watambue vipaji vyao. Tuachane na huu mtindo wa kuwapangia kozi za ualimu wanafunzi ambao hawana kipaji cha kufundisha. Ni walimu hawa wanaoua vipaji vya watoto wetu. Au tuseme kuwa sikio la kufa halisikii dawa?