Maajabu ya Gidion na ndoto za kuwa mwanasayansi, mbunifu
'Ulemavu sio kikwazo cha kufikia malengo yako' msemo huu umeakisi maisha ya Gidion Moses (14) mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Mwatulole mkoani Geita.
Licha ya ulemavu wa viungo unaomlazimu kusoma kwa kuangalia na kushindwa kuandika kwa kuwa anatetemeka muda wote, Moses ndiye kinara kitaaluma katika darasa hilo.
Namna yake ya kujifunza na uwezo wa kunakili kwa kichwa kile anachofundishwa na mwalimu, ndicho kilicholifanya Mwananchi kufunga safari hadi katika shule anayosoma.
Mwandishi wa makala haya, anasimulia alivyokwenda shuleni hapo na kushuhudia namna pekee ya usomaji wa Moses ambao aghalabu ni nadra kuuona popote nchini na pengine duniani.
Shuleni
Saa nne asubuhi nafika katika shule ya msingi Mwatulole mkoani hapa, naelekezwa na wenyeji walipo wanafunzi wa darasa la sita; lilikuwa darasa lililosheheni wanafunzi.
Haikuwa rahisi kumgundua Moses kwa haraka kwa kuwa wingi wa wanafunzi ulinifanya nione wote wapo sawa, hata hivyo hakukuwa na anayeonekana na taswira ya ulemavu.
Katika makaribisho nikapepesa macho na kuona moja kati ya madawati ya mbele likiwa na wanafunzi wanne na mmoja hakuwa anaandika kama ilivyokuwa kwa wenzake, badala yake alikuwa alielekeza macho yake ubaoni kwa makini.
Nilitambulishwa kuwa huyo ndiye Moses na amewekwa katikati ya wenzake watatu kama kinga ili asianguke kutokana na ulemavu wake.
Tabasamu lake usoni, ucheshi na unadhifu wake ni vigumu kubaini haraka changamoto aliyonayo.
Ulemavu alionao unamfanya kutetemeka muda wote, hali inayomfanya ashindwe kukaa mwenyewe dawatini, kadhalika anatembea kwa usaidizi wa baiskeli ya magurudumu matatu.
Hali hiyo inamfanya kuwa mwanafunzi anayesoma kwa kusikiliza tu, kwani hana uwezo wa kuandika na hata mtihani wake anaufanya kwa kuulizwa maswali na kujibu kwa mdomo.
Uwezo wake darasani
Nikiwa darasani hapo naarifiwa kuwa Moses, alifika shuleni hapo mwaka 2017 akiwa na hali mbaya zaidi ya anayoonekana nayo sasa, kwani hakuweza kuongeza, kuandika, kutembea, kusimama na hata kukaa, kama inavyoelezwa na Marry Francis mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
Kulingana na mwalimu huyo, uwezo wa kuongea ulitokana na kile nilichosimuliwa na mmoja wa walimu wake kuwa, ni mazoezi ya viungo yanayotolewa shuleni hapo, ambayo angalau yamemwezesha kuongea, kusimama na kutembea kiasi.
“Tulimpokea akiwa hawezi kuongea ,hatembei,hasimami tumekuwa tukifanya mazoezi na kwenye kujifunza tuligundua kipawa chake anauelewa mkubwa wa kujifunza ni mtoto wa pekee sana anakipawa cha ajabu anafikiri dakika chache na kupata jibu,” anasema.
Kadhalika, Moses ana uwezo wa kutumia mguu wake kula chakula na hata kuandika.
Naambiwa ndiye mwanafunzi kinara katika darasa hilo, mwenye uwezo mkubwa wa kujibu maswali.
Itakushangaza zaidi pale ambapo mwanafunzi huyu aligomea uamuzi wa kutoruhusiwa kufanya mtihani wa somo la hisabati kwa kuwa hana uwezo wa kuandika.
Kwa mujibu wa mwalimu wake, uamuzi huo wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), ulimsababisha agomee kufanya mitihani ya masomo mengine yote hadi pale atakaporuhusiwa kufanya wa hisabati kwa kuwa ndilo somo analolipenda zaidi.
Uamuzi wake huo, uliilazimu idara ya elimu Halmashauri ya Geita kumwombea kwa Necta ili aruhusiwe kufanya mtihani wa somo hilo na alipoufanya alifaulu kwa kupata daraja A.
Anavyoishi na hali ya ulemavu
Baada ya mapumziko, napata nafasi ya kukaa kando kwa mazungumzo na Gidion , anasema kwa sasa anatumia mguu kula chakula jambo analosema limepunguza majukumu kwa mama yake.
Anasimulia tangu alipozaliwa hadi akiwa na umri wa miaka sita, amekuwa akilishwa chakula na mama yake.
“Nilikua namhurumia sana mama muda wote ananihudumia nilianza kidogokidogo namwambia kaka aweke kijiko kwenye vidole vya mguu niliendelea na mazoezi hadi siku moja nikamwambia mama anichanganyie ugali na mboga aniwekee nikawa nakula kwa mguu,” anasema.
Si kula pekee, Gidion anasema kwa kutumia mguu wake, anaweza kutumia kompyuta mpakato na kishikwambi kuandika na sasa anajifunza kuandika kwa kutumia kalamu.
Ndoto zake
Mwanafunzi huyo ana kiu ya kuwa mwanasayansi mbunifu, lakini ana shaka na kutimia kwa ndoto hiyo kwa kile anachofafanua kuwa, mazingira ya nyumbani na umasikini unaoikabili familia yake.
Kutokana na hilo, anaiomba Serikali msaada wa vifaa na kuendelezwa katika elimu, akiamini atafanya makubwa zaidi atakaposaidiwa hayo.
Changamoto
Wingi wa wanafunzi katika darasa analosoma, anasema ni moja ya vitu vinavyomlazimu kutumia nguvu kumwelewa mwalimu.
“Namsikiliza tu mwalimu siwezi kuandika useme nitasoma baadaye sasa wanafunzi wakiwa wanaongea huku mwalimu anafundisha napata shida kuelewa tofauti na mwanafunzi mwingine ambaye hata asipoelewa darasani akifika nymbani akijisomea atakumbuka,” anasema.
Safari yake kwenda shule kila asubuhi, anasema inafanikishwa kwa usaidizi wa rafiki yake anayempitia kila asubuhi kwa ajili ya kumsaidia kusukuma baiskeli yake na hubaki nyumbani iwapo mwenzake huyo atapata dharura.
“Natamani kupelekwa shule ya bweni kwa sababu sasa hivi rafiki yangu akiugua au asipokuja shule inabidi na mimi niugue sina wa kunipeleka shule nakosa masomo wakati ambao nahitaji kusoma,” anasema.
Hafurahishwi na kuogeshwa nje, akisema amekua sasa anahitaji faragha, huku chooni pia analazimika kutafuta mtu wa kumsaidia kumwagia maji jambo ambalo anasema ni aibu kwake, angetamani kufanya mwenyewe.
Gidion anatamani kusaidiwa kompyuta mpakato na kupelekwa shule maalumu kwa hali yake.
Wasemaavyo walimu wake
Mwalimu Mary anasema hata vifaa alivyonavyo sasa ikiwemo baiskeli aliipata kwa wafadhili, kwa kuwa awali alikuwa akipelekwa shuleni hapo kwa kubebwa mgongoni na mama yake.
“Huyu mtoto ana uwezo mkubwa kwenye kichwa anaweza kujibu maswali kwa kichwa na kufanya hesabu kichwani kila kitu anafanya kichwani” anasema.
Mwalimu huyo anasema pamoja na kuhama na kwenda kusoma na wanafunzi wasio na ulemavu, bado anaendelea kufanya mazoezi yatakayomwezesha kujitegemea kama kula na kuandika kwa mguu.
Familia yake
Dorcas Manyanda ni mama yake mzazi, anasema hali aliyonayo mwanawe ilianza kujitokeza alipofikisha miezi sita baada ya kuzaliwa.
“Alikua ameanza kukaa ghafla hali ilibadilika akashindwa kukaa nilimpeleka hospitali wakasema ana ngiri baadaye wakasema uti wa mgongo wakanifundisha jinsi ya kumfanyisha mazoezi, haikusaidia ndio mwisho nikaambiwa atakuwa alizaliwa hivyo,” anasema.
Kwa msaada wa wasamaria wema, Dorcas anasema aliwahi kulazwa miezi sita katika Hospitali ya Bugando kutibu tatizo hilo bila mafanikio, badala yake viungo vilizidi kulegea.
Alivyokataa asisome
Safari ya kupata elimu kwa mwanafunzi huyo ilianza kwa vikwazo kutokana na kile kinachosimuliwa na mama yake kuwa, aliugomea uongozi wa shule hiyo kumwandikisha Gidion, akiamini mwenye ulemavu hasomi.
“Mimi niliwashangaa walimu wanaotaka mtoto ambaye haongei, hawezi kukaa wala kujihudumia aende shule nilikataa nikawaambia sina uwezo.
“Wakaondoka lakini baada ya miezi kadhaa walirudi na kuniambia kama sitamwandikisha shule, Serikali itanichukulia hatua niliogopa nikampeleka,” anasema.
Safari ya kuamka saa 12 asubuhi akimpeleka shule mwanawe kwa baiskeli akiwa mgongoni ilianza na saa tano anamfuata kumrudisha nyumbani.
Kuna wakati, anasema alilazimika kumwacha nyumbani hadi wiki mbili kwa kukosa nauli ya Sh1,000 anayotumia kukodi baiskeli wanayopakiwa na mwanawe.
“Walimu waliona shida yangu na kunitafutia baiskeli ya magurudumu yaani ilikua ni mateso nimeteseka nae sana unatafuta kazi ili upate nauli lakini hata kwenye kazi huwezi kukaa maana asubuhi ukienda shule saa tano lazima urudi ukamchukue umlishe ni maisha magumu,” anasema.
Mama huyo anasema walimu wamekuwa msaada muhimu kwenye malezi ya Gidon kwani walimuunganisha na wafadhili waliompeleka Njombe kwa ajili ya mazoezi.
Anawashauri wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka shuleni kwani ndiko watakakopata ujuzi na maarifa ya kujisaidia.
Rafiki yake
Kama kuna tuzo anayostahili kupewa rafiki bora, basi Francis Simon rafiki wa Moses anastahili.
Simon amejitolea kumpeleka shule na kumrudisha kwa miaka mitatu sasa kazi anayoifanya kila siku tangu apate baiskeli ya miguu mitatu.
Anasema pamoja na kuishi mbali na nyumbani kwa kina Moses, amekuwa akiamka mapema kumfuata rafiki yake na kumpeleka shule, kadhalika humsaidia na mambo mengine wanapokuwa shuleni.
“Anahitaji msaada hata kwenda msalani hivyo lazima niwe karibu naye ila wakati wa mvua anakosa masomo, maana hana mwavuli lakini wingi wa wanafunzi darasani unamfanya asome kwenye mazingira magumu,” anasema.
Ofisa Elimu
Ofisa Elimu maalum idara ya elimu msingi Halmashauri ya Mji wa Geita, Zunaida Alphonce anasema kwa upande wao mara nyingi wanahangaikia mahitaji ya mwanafunzi huyo na kumtafutia wafadhili wanaomsaidia kupata matibabu ya viungo mkoani Njombe.
Anasema wameshindwa kumpeleka katika shule ya bweni kutokana na hali yake ya kushindwa kujihudumia, na kwamba watafanya hivyo baada ya kuimarika kutokana na mazoezi anayofanyishwa.
Halmashauri hiyo ina wanafunzi 687 waliopo kwenye vitengo 10 maalum pamoja na shule jumuishi wakiwa na ulemavu wa aina mbalimbali kama uziwi, upofu na akili.