Prime
Maofisa elimu, wakuu wa shule kikwazo utekelezaji elimu jumuishi -2
Muktasari:
- Tathmini iliyofanywa imebaini baadhi ya maofisa elimu maalumu hawajatekeleza wajibu wao kwa kiwango kinachotarajiwa, jambo linalokwamisha utekelezaji wa elimu jumuishi
Dar es Salaam. Wakati upungufu wa walimu na vifaa saidizi vikibainishwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazokwamisha elimu jumuishi, utafiti uliofanywa na Serikali unawagusa maofisa elimu maalumu na wakuu wa shule kama sehemu ya tatizo hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi katika baadhi ya shule zilizopo wilayani za Bagamoyo mkoani Pwani na Kilombero mkoani Morogoro umebaini watoto wenye mahitaji maalumu wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowazuia kupata elimu kwa usawa.
Miongoni mwa hizo ni ukosefu wa vifaa saidizi kama vitimwendo, vifaa vya mazoezi tiba, vitabu vya nuktanundu (braille) na vifaa vya usikivu, hivyo kuwa kikwazo katika utekelezaji wa utoaji elimu jumuishi.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Elimu Maalumu, Wizara ya Elimu, Dk Magreth Matonya anasema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji kwa watoto wenye mahitaji maalumu ili kuhakikisha hawaachwi nyuma kwenye mfumo wa elimu.
Hata hivyo, anakiri bado kuna changamoto zinazokwamisha jitihada hizo, mojawapo ikiwa ni uwepo wa maofisa elimu maalumu wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.
Anasema tathmini iliyofanywa imebaini baadhi ya maofisa elimu maalumu hawajatekeleza wajibu wao kwa kiwango kinachotarajiwa, jambo ambalo Serikali imeanza kulifanyia kazi.
“Baadhi wamekuwa wakibaini watoto wenye mahitaji maalumu lakini hawafuatilii maendeleo yao baada ya kujiunga na shule. Wengine hushindwa kuratibu mawasiliano kati ya shule ya awali na ile anayohamia mwanafunzi baada ya kuhitimu hali inayoweza kuathiri mwendelezo wa masomo,” anasema na kuongeza:
“Tumefanya tathmini kwa kushirikiana na Tamisemi na kubaini maeneo yenye upungufu. Julai tutakutana na maofisa hao kwa ajili ya kuwapatia miongozo na maelekezo yatokanayo na matokeo ya uchambuzi wa hali ya utekelezaji wa elimu jumuishi katika elimu ya msingi.”
Dk Matonya anasema wadhibiti ubora wamekuwa wakifuatilia kwa karibu ufundishaji darasani na kutoa mrejesho unaosaidia kuboresha utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Kupitia wadhibiti ubora tunafuatilia sababu zinazowafanya baadhi ya watoto kuacha shule. Mtoto akieleza hana kitimwendo, tunatafuta namna ya kumpatia. Akisema changamoto ni usafiri, tunashirikiana na wazazi na wakati mwingine kumwezesha kuishi bweni ili aendelee na masomo,” anasema.
Ukosefu vifaa saidizi
Akizungumzia kuhusu watoto kukosa vifaa saidizi, Dk Matonya anasema hali hiyo inachangiwa na walimu wakuu na maofisa elimu maalumu kushindwa kutimiza wajibu wao.
“Sisi tunategemea taarifa kutoka kwa walimu wakuu na maofisa elimu maalumu, wao ndio wanajua kwenye maeneo yao kuna watoto wenye mahitaji maalumu wangapi na vifaa gani vinahitajika, wakileta taarifa hizo tunapeleka vifaa. Hapo kuna kutowajibika, hawa ndio wanatuchelewesha; hili tumeshaliona na tunalifanyia kazi,” anasema.
Anaeleza: “Tulikubaliana mwanafunzi akishabainishwa lazima vifaa vyake vinunuliwe, hata kama mtoto akibanika mahitaji yake baada ya muda wa ubainishaji kwisha, wizara tunayo bajeti ya kununua vifaa, kilichopo kwenye hizo shule hawajatoa taarifa hilo siyo tatizo la Serikali.”
Anasema Serikali imegawa vifaa vya Sh10 bilioni nchi nzima na kwamba vipo vya akiba akieleza: “Nikipata taarifa za uhitaji wa vifaa mfano vitimwendo, vifaa vya usikivu najua wapi tunapata kwa sababu kuna shule vinapelekwa kwa wingi hivyo vinahifadhiwa huko.”
Kuhusu ubainishaji, anasema mchakato hufanyika Oktoba hadi Machi na kwamba, timu ya ubainishaji huzunguka ngazi ya nyumba 10 kwenye mitaa na vijiji kubainisha wenye mahitaji maalumu.
Hata hivyo, anakiri si kila halmashauri ina kituo cha upimaji ila vinapatikana ngazi ya mkoa, hivyo kuwa changamoto kwa wengi kuvifikia.
Katika kushughulikia hilo, anasema umetengenezwa mpango wa kuwa na timu za kwenda kuwafuata wananchi ngazi ya nyumba 10 na kisha mtoto anapobainishwa inasimamia kufikishwa kwenye kituo cha upimaji.
“Timu hii inayokuwa na walimu wa aina tano za ulemavu, mdhibiti ubora wa elimu, ofisa ustawi wa jamii, daktari na ofisa elimu maalumu inakwenda kwa balozi wa nyumba 10, yeye ndiye anatuambia kama kuna mtoto mwenye ulemavu. Timu inamfanyia uchunguzi kubaini changamoto alizonazo na mahitaji yake kama ni ya elimu au matibabu, kuanzia hapo tunamsajili na kuanza kumfuatilia,” anasema.
Changamoto ya walimu
Akizungumzia uhaba wa walimu wa elimu maalumu, Dk Matonya anasema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha upatikanaji wa walimu wenye utaalamu wa elimu jumuishi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini.
Anasema awali Chuo cha Ualimu Patandi pekee ndicho kilichokuwa kikitoa wahitimu wa elimu maalumu, kikizalisha takribani walimu 200 kwa mwaka, lakini sasa Serikali imepanua mafunzo hayo katika vyuo vya Kabanga na Mpwapwa, hivyo kuongeza wahitimu hadi zaidi ya 1,000 kwa mwaka.
Anasema elimu jumuishi na lugha ya alama imefanywa kuwa masomo ya lazima kwa wanafunzi wote wa ualimu katika ngazi mbalimbali za elimu ili kuhakikisha kila mwalimu anayehitimu anakuwa na uelewa wa msingi wa kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Kuanzia mwaka ujao kila mwalimu atakayehitimu atakuwa na maarifa ya msingi na uwezo wa kuwasaidia watoto wenye changamoto mbalimbali,” anasema.
Kwa walimu waliopo kazini wasio na mafunzo hayo maalumu, anasema Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya kuongeza uwezo kupitia programu mbalimbali zinazofadhiliwa na miradi tofauti.
“Pia tumeanzisha vilabu vya lugha ya alama shuleni ambavyo vinawasaidia walimu na wanafunzi kujifunza na kufundishana,” anasema.
Elimu jumuishi inatolewa kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022/2026, msukumo pia umewekwa kwenye Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kupitia vifungu vya 27 na 28 vinavyozitaka taasisi za elimu kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata elimu sawa na wengine, pamoja na kuwekewa mazingira rafiki ya kujifunzia bila ubaguzi wowote.
Katika kifungu cha 27(4), shule zinatakiwa kuwapatia wanafunzi wenye ulemavu huduma maalumu za usaidizi ikiwemo walimu wa elimu maalumu, vifaa vya kujifunzia na mbinu mbadala za mawasiliano.
Hali ilivyo shuleni
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pengo kubwa kati ya matakwa ya sheria na utekelezaji wake, mfano ukiwa katika Shule ya Msingi Lipangalala, wilayani Kilombero mkoani Morogoro, ambayo ina watoto 21 viziwi lakini kuna mwalimu mmoja pekee wa kuwafundisha.
Upungufu wa walimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu pia umebainika kwenye kituo cha Nianjema, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani chenye wanafunzi 65 wenye aina mbalimbali za mahitaji maalumu ambacho kina walimu watatu.
Uwiano huu ni tofauti na inavyopaswa kuwa katika madarasa ya watoto wenye ulemavu ambapo inaelekezwa wastani wa wanafunzi watano wanatakiwa kufundishwa na mwalimu mmoja.
“Tuna wanafunzi 65, wavulana 34, wasichana 31. Hapa kwenye kitengo tuna watoto wenye usonji, wenye ulemavu wa viungo na akili na wale wasiokuwa na utulivu,” anaeleza Suzan Nkya, Mkuu wa kitengo cha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Nianjema.
Upungufu huo pia umebainika katika kitengo cha elimu maalumu kwenye Shule ya Msingi Ifakara, wilayani Kilombero mkoani Morogoro chenye wanafunzi 51 na walimu wawili.
Ubainishaji watoto
Uchunguzi unaonesha katika shule nyingi walimu wanakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu vya uchunguzi wa awali vinavyotumika kubaini changamoto za kuona, kusikia, kujifunza na aina nyingine za ulemavu kwa watoto.
Hata katika maeneo ambako vifaa hivyo vinapatikana, matumizi yake hayajakidhi mahitaji halisi au hata vifaa hivyo kushindwa kutumika kwa ufanisi kwa sababu utambuzi haujafanyika kuwafikia walengwa.
Oktoba 2022 Serikali ilitoa Mwongozo wa Utekelezaji Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi ambao pamoja na mambo mengine ulitoa maelekezo kwa halmashauri kuratibu uanzishaji na uendeshaji wa vituo vya upimaji wa kubaini mahitaji maalumu (ESRAC).
Hata hivyo, hadi Juni 2026 ni halmashauri 34 zilizoanzisha vituo hivyo kati ya halmashauri 184, vituo hivyo kwa sasa viko ngazi ya mkoa hivyo wahitaji hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo hali inayosababisha wengine kushindwa kumudu.
Mdau wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu, Daniel Reuben, anasema kutokuwepo kwa mifumo madhubuti ya kupima na kubaini watoto wenye mahitaji maalumu kunasababisha changamoto kubwa katika utekelezaji wa elimu jumuishi.
Reuben mwenye ulemavu wa kutosikia anasema hatua ya kwanza katika elimu jumuishi ni kumtambua mtoto na mahitaji yake kinyume cha hilo shule hushindwa kumpatia mazingira na huduma zinazolingana na hali yake.
“Wakati mwingine mtoto huonekana hana akili au hajitumi, ilhali tatizo ni kwamba hajatambuliwa na hajapatiwa msaada unaohitajika. Mwishowe anaweza kukata tamaa na kuacha shule,” anasema.
Anasema athari za kutowatambua watoto wenye mahitaji maalumu zinaonekana pia katika ufaulu wa wanafunzi, ubora wa ufundishaji na hata maendeleo ya mitalaa.
“Tunaposhindwa kujua mahitaji halisi ya wanafunzi, tunashindwa kufanya maboresho katika mtalaa, sera na mifumo ya ufundishaji. Utambuzi wa mapema ndiyo msingi wa kuboresha elimu jumuishi na kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya kujifunza,” anasema.
Digna Mushi, Mkuu wa Miradi wa Shirika la Ocode linalofanya shughuli za elimu katika Wilaya ya Bagamoyo, anasema kukosekana kwa vituo vya kitaalamu vya upimaji vinavyoweza kubaini kwa usahihi mahitaji yao kabla ya kupewa vifaa saidizi kunasababisha baadhi ya watoto kupewa vitimwendo visivyolingana na mahitaji yao halisi.
“Vitimwendo ni sawa na dawa. Vinapaswa kumsaidia mtoto kuimarika, lakini mara nyingi vinatolewa bila kufanyika upimaji wa kitaalamu. Matokeo yake baadhi ya watoto hupata matatizo zaidi ya viungo kwa sababu vifaa hivyo havijalinganishwa na mahitaji yao,” anasema.
Anabainisha kuwa changamoto kubwa inayojitokeza ni ukosefu wa miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu katika shule nyingi, akitoa mfano katika shule nne ambazo wanatekeleza mradi, ni moja pekee yenye choo maalumu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu.
Vilevile, anasema uhaba wa walimu wenye stadi za kufundisha katika madarasa jumuishi unaendelea kuwa kikwazo kikubwa.
“Walimu wengi waliopo kazini hawakupata mafunzo ya kutosha kuhusu elimu jumuishi. Wapo ambao hawajui hata lugha ya alama, jambo linalowafanya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia kushindwa kushiriki kikamilifu katika masomo,” anasema.
Itaendelea kesho kwa kuangalia mapendekezo ya wadau ili kufanikisha mkakati wa elimu jumuishi