Mchujo kwa walimu bado sintofahamu kwenye elimu
Mitihani ya mchujo ni moja ya mbinu za kupata wafanyakazi bora katika eneo husika, ambayo mara nyingi hufanywa ili kuhakiki uwezo alionao mwombaji wa ajira kulingana na utaalamu stahiki.
Mitihani ya mchujo hulenga kupima zaidi stadi alizonazo mhitimu ili kukidhi vigezo vya kazi iliyotangazwa na waajiri. Vigezo vya mitihani ya mchujo huwekwa na bodi maalumu.
Taaluma ya ualimu bado haijawa na bodi yake kama zilivyo bodi za makandarasi madaktari na wanasheria, lakini mitihani ya mchujo imeingia katika taaluma hii ‘adhimu’ ambayo hapo awali iliaminika kuwa chaguo la mwisho baada ya wanafunzi kukosa fursa nyingine za ajira.
Serikali imezidi kutangaza utaratibu huu mpya wa walimu kufanya mitihani ya mchujo, huku wadau wa elimu wakihoji; iweje tena Serikali yenye dhamana ya kudhibiti mitihani itilie shaka ufaulu wa walimu na kuwataka kufanyisha tena mitihani mingine kama kigezo cha kuwapa kazi?
Utaratibu huu wa mchujo, kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, unalenga kupima uwezo wa mwalimu ili aweze kikidhi vigezo vya ajira.
Tangu awali ajira ya ualimu ilitolewa baada ya wahitimu kujaza fomu ya chaguzi za mikoa na shule wanazozitaka pindi wakiwa vyuoni kabla ya kufanya mitihani ya kuhitimu.
Kipindi hicho walimu tulikuwa tunaomba sehemu nzuri, zenye miundombinu na fursa za kujiendeleza kimasomo, hasa miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Kwa sasa ajira zinapatikana kwa kutuma maombi katika tovuti maalum ya maombi ya ajira, kisha anayepata nafasi hufanyiwa usaili na kupangiwa eneo la kazi.
Utaratibu huu mpya wa ajira za ualimu, ulitangazwa Juni 16, 2023 na Profesa Mkenda wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walimu walioshinda shindano la kwanza la stadi za kufundisha kuhesabu na hisabati, lililoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Mbinu hii mpya umekuja wakati Serikali ikizidi kubuni njia ya Tehama kutumika katika ufundishaji ili kukabiliana na tatizo la walimu nchini, huku shule zilizoko mkoani Pwani zikiwa kinara wa jaribio hilo.
Katika kupigia chapuo ufundishaji kwa njia ya mtandao, wadau wa elimu wanahisi utapunguza uhaba wa walimu kwani mwalimu mmoja ataweza kufundisha zaidi ya wanafunzi 200 kwa njia ya Tehama.
Mtihani wa mchujo
Linapokuja sula la mchujo kwa kuwataka walimu wafanye mitihani ili kupata ajira, ni bora pia tujiulize mitihani ya mchujo itatungwa kwa kiwango gani na kusahihishwa na walimu gani?
Nauliza maswali haya kwa sababu mwaka jana Profesa Mkenda alinukuliwa bungeni akisema zinapotoka nafasi za ualimu, wabunge wamekuwa wakitoa vimemo na kuleta kero kwenye taasisi za ajira katika kushawishi watu wao wapate ajira.
Wadau wa elimu wanajiuliza; je mitihani ya mchujo itakuwa suluhu ya vimemo hivyo?
Hii ni kwa sababu bado hata Baraza la Mitihani linalotoa matokeo kila mwaka linashutumiwa kwa kuzalisha baadhi ya wahitimu wasio na tija kwenye soko la ajira.
Kwa kuwa waziri kaonelea mitihani ya mchujo kuwa mwarobaini wa kupata walimu bora, ni sharti tujiulize ubora wa hiyo tathmini na wahakiki wa mchakato huo, hasa kipindi hiki ambacho wahitimu wa tangu mwaka 2015 wamejaa mtaani.
Idadi ya wahitimu wa taaluma ya ualimu ni kubwa mno ambapo kuwakurupusha huko walipo kufanya mtihani wa mchujo ili wapate kazi, inaweza kuleta taharuki na huenda wengi walikiwisha sahau hata sayansi ya ufundishaji (pedagogy).
Ikiwa mtihani wa mchujo utafanywa kwa vitendo, basi hadhira iwekwe chonjo kushuhudia haki ikitendeka katika utoaji wa hizi ajira, maana sidhani kama kutakuwa na mfumo wa kudhibiti vimemo vilivyomkasirisha Waziri Mkenda.
Tanzania si nchi pekee inayonuia kutoa mitihani ya mchujo wa kuwezesha walimu kupata ajira. Kwa mujibu wa utafiti wa elimu linganishi uliofanywa na Shirika la Kupima Viwango vya Elimu na walimu Duiani (ETS), nchini Singapore, walimu huajiriwa baada ya kuwa wemefuzu mtihani wa umahiri katika lugha ya Kiingereza.
Kwa mujibu wa utafiti huo, nchini Marekani ambapo ajira hutolewa kwenye majimbo stahiki, mwalimu hutakiwa kufanya mitihani ya vitendo ili kushawishi jopo la waajiri kama anastahili kupewa kazi.
Nchini Ujerumani, pamoja na mwalimu kuhitimu masomo na kupewa cheti kizuri, bado hupimwa kwa mitihani ya kisaikolojia ili kuhakiki kama ana wito wa kuweza kuhudumia na kuwapenda watoto ndipo hupewa kazi ya kufundisha.
Nchi hizi zilizoendelea huenda zikawa chachu ya kutufanya kama taifa tujue namna ya kupata walimu bora.
Lakini wadau wa elimu nchini wanahisi mitihani ya mchujo si njia ya kupata walimu stahiki, bali inalenga kuwapunguza wahitimu wa fani hii katika kinyang’anyiro cha ajira baada ya kuonekana ni wengi dhidi ya bajeti iliyopo.
Kwa mujibu wa Haki Elimu, Serikali inapaswa kuajiri walimu 25,000 kila mwaka na italazimika kufanya hivyo kwa miaka mitano mfululizo ili kukabiliana na upungufu ulipo.
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ilieleza kuwa hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika shule za msingi yalikuwa ni 362,189 kwa kutumia uwiano wa 1:45 (mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45).
Hata hivyo, walimu waajiriwa walikuwa ni 175,864 ambao hufundisha wanafunzi milioni 12.36 waliopo nchi nzima katika ngazi hiyo ya elimu. Hiyo ni sawa na kusema kwa wastani, mwalimu mmoja hufundisha wanafunzi 70.
Tamisemi inaeleza kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari hadi kufikia Februari mwaka jana yalikuwa ni 174,632.
“Waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5. Mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari yanatokana na masomo yanayofundishwa,” alisema Waziri wa Tamisemi wakati huo, Angela Kairuki.
Wachambuzi wa masuala ya elimu akiwemo Richard Mabala wanasema uhaba wa walimu unawakosesha fursa wanafunzi kupata maarifa kwa ukamilifu ili kuwawezesha kufaulu mitihani yao na kupata stadi muhimu kuboresha maisham yao na Taifa kwa ujumla. Je, mtihani wa mchujo utakuwa suluhisho?