Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtalaa mpya ulivyobadili mbinu za kutathmini ujifunzaji darasani

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu mitihani imekuwa ikipewa uzito mkubwa kuliko ujifunzaji. Tunafahamu wapo walimu wanaofundisha kwa mtindo wa kuwafanyisha wanafunzi maswali.

“Tunaomba kwenye mafunzo haya mkazo uwe namna ya kutunga maswali yanayoendana na mtalaa mpya,” nasisitizwa na mkuu wa shule aliyekuwa ameandaa mafunzo ya walimu wake kujifunza namna ya kutekeleza mtalaa mpya.

Tofauti kabisa na msisitizo huo, wakati wa uchambuzi wa uzoefu wa walimu wake kabla ya mafunzo, nilibaini tatizo lilikuwa namna walimu wanavyoutazama ujifunzaji na namna ya kuupima na sio utungaji wa maswali.

Nilikumbuka tahadhari iliyowahi kutolewa na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa kuwa tamaa ya ufaulu imekuwa kikwazo kikubwa katika utoaji wa elimu.

Katika mahojiano aliyofanya na kituo kimoja cha televisheni mwanzoni mwa mwaka huu, Kamishna alinukuliwa akikemea vikali utamaduni mpya wa shule na wamiliki wa shule, kuthamini zaidi mitahani na ufaulu kuliko ujifunzaji.

Kwa muda mrefu mitihani imekuwa ikipewa uzito mkubwa kuliko ujifunzaji. Tunafahamu wapo walimu wanaofundisha kwa mtindo wa kuwafanyisha wanafunzi maswali. Hata pale mwalimu alipofundisha, kipindi kizima kingegeuzwa kuwa uwanja wa mwalimu kuhutubia na kuongea na ubao, bila kufanya tathmini kuona kama mwanafunzi anajifunza.

Mazoea haya yanabadilishwa katika mtalaa ulioboreshwa. Ufundishaji wa mtalaa mpya, kwa mfano, unalazimisha tathmini iwe sehemu kamili ya ujifunzaji.

Mwalimu hawezi kufundisha chochote bila kukusanya ushahidi unaomsaidia kujua ikiwa mwanafunzi anapata kile anachotarajiwa kujifunza. Lengo la tathmini linakuwa si kumpa mwanafunzi alama kama ilivyokuwa kwa mtalaa wa zamani bali kubaini maeneo anayohitaji msaada katika kujenga mahiri.

Kwa hivyo badala ya mwalimu kuhutubia na hatimaye kutoa zoezi mwishoni, kwa mtalaa mpya mwalimu analazimika kuandaa shughuli za ujifunzaji zenye vigezo mahususi vya upimaji.

Katika makala haya ninaonesha namna gani mwalimu anaweza kufanya tathmini ya ujifunzaji wakati somo linaendelea, nje ya kipindi chake na hata kupima ujifunzaji baada ya ujifunzaji, yaani kwa kutumia mitihani.


Upimaji wakati wa somo

Katika ufundishaji wa zamani, kwa kiasi kikubwa, upimaji haukuwa endelevu na hata pale ulipofanyika, mwalimu asingekuwa na kigezo kinachoeleweka.

Kwa mfano, mwalimu angeandika; “Kuangalia kama wanafunzi anajadiliana vizuri na wenzake,” “Kuchunguza ikiwa wanafunzi wanaandika, wananukuu au kusikiliza kwa umakini.”

Upimaji wa namna hii ulilenga zaidi kufuatilia ikiwa mwanafunzi anaheshimu kile kinachofanywa na mwalimu darasani badala ya kutusaidia kujua ikiwa kweli anajifunza.

Mtalaa wa sasa, tofauti na ilivyokuwa awali, umeweka bayana vigezo vya upimaji kwa kila shughuli kuu ya ujifunzaji inayoonekana kwenye muhtasari wa somo.

Kazi ya mwalimu haiishii kufuatilia usikivu, utulivu na nidhamu ya mwanafunzi wakati yeye akilitawala darasa, bali kutengeneza vigezo vinavyopimika wakati shughuli ya ujifunzaji inatekelezeka.

Mfano, katika somo la Maarifa ya Jamii mwalimu ameandaa shughuli ya uhusianishaji inayosema, “Katika makundi ya wanne wanne, wanafunzi watabaini sababu kubwa iliyochangia malalamikio mengi kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.”

Shughuli hii haitokuwa na maana ikiwa mwalimu hana kigezo cha kufuatilia kile mwanafunzi anachojifunza.  Kigezo kinaweza kuwa, “Vyanzo vinne vya malalamiko ya uchaguzi vimebainishwa na kuhusianishwa na malengo ya somo.”

Katika hatua ya mwanafunzi kujenga maarifa ya msingi kwenye somo hilo hilo hilo, mwalimu anaweza kuonesha video inayoonesha maelezo ya makundi mbalimbali yanayoyalalamikia uchaguzi na kisha wanafunzi watajadili kile walichokisikia katika makundi yao na kuchora mchoro unaoonesha visababishi vya malalamiko. 

Kigezo cha upimaji hapa kinaweza kuwa, “Mchoro unaonesha visababishi vinne na uhusiano wake na malalamiko ya wadau.”

Kwa msingi huo, tathmini ya ujifunzaji wa mwanafunzi inakuwa rahisi kufanyika kupitia vigezo hivi vya upimaji ambavyo mwalimu anakuwa ameviandaa wakati wa kuandaa shughuli za ujifunzaji. Faida yake ni kumwezesha mwalimu kufuatilia namna gani mwanafunzi anaendelea kufikia kigezo hicho wakati shughuli ya ujenzi wa maarifa inaendelea.


Tathmini ya ujifunzaji nje ya darasa

Tofauti na ufundishaji wa zamani uliotarajia mwanafunzi ajifunze zaidi akiwa ndani ya kipindi, katika mtalaa mpya mwalimu anatarajiwa kuweka mazingira ya mwanafunzi kukutana na maarifa ya msingi kabla ya kipindi na pia kupanua maarifa hayo baada ya kipindi.

Kwa kulizingatia hili, mwalimu anawajibika kuandaa shughuli nyingi za ujifunzaji zinazomlazimisha mwanafunzi kuchunguza mazingira yake, kujenga udadisi, kuchambua taarifa zaidi, kubuni namna mpya ya kutazama mambo, na hatimaye kujenga uelewa mpya zaidi ya kile alichojifunza darasani.

Kama ilivyokuwa katika shughuli za ujifunzaji ndani ya darasa, mwalimu anawajibbika pia kutengeneza vigezo kadhaa (rubrics) atakavyovituma kupima maendeleo ya mwanafunzi kadri anavyojifunza.

Mfano wa shughuli ya ujifunzaji nje ya darasa inayokuza mahiri ya utatuzi wa matatizo anayopewa mwanafunzi, shughuli inaweza kusomeka kama ifuatavyo, “Kijiji chetu kinakabiliwa na tatizo la maji machafu yanayosababisha magonjwa. Tumia kitabu cha Sayansi ya Maji ukurasa wa 34 – 42 kubuni suluhisho rahisi linaloweza kutumika nyumbani au shuleni.”

Tathmini ya ufanisi wa shughuli hii inaweza kuzingatia vigezo vitatu kama ifuatavyo: Kigezo cha kwanza: (nzuri) -tatizo linachambuliwa kwa kutumia ushahidi uliopo kwenye kitabu na suluhisho linalobuniwa linatekelezeka.

Kigezo cha pili: (wastani) tatizo linachambuliwa bila ushahidi wa moja kwa moja na ufumbuzi unaopendekezwa unatekelezeka kidogo. Kigezo cha tatu:  (dhaifu -tatizo linachambuliwa kinadharia na hakuna ufumbuzi unaoonekana.


Utungaji wa maswali yanayopima mahiri

Mitihani ni hatua ya mwisho ya upimaji wa kile alichojifunza mwanafunzi. Maswali mazuri huzingatia nadharia ya Benjamin Bloom inayopendekeza kupima ukuaji wa maarifa kwa hatua sita muhimu, yaani kukumbuka maarifa ya msingi, kuyaelewa, kuyatumia, kuyachambua, kuyatathmini, na kuyajenga maarifa mapya.

Kwa msingi huo, tathmini ya ujifunzaji wa maarifa inaweza kufanywa kwa kulibadilisha swali hilo ili kupima maarifa kwa husika.

Katika somo la sayansi, kwa mfano, swali linaweza kuanza na hatua ya kupima kumbukumbu, “Taja hatua kuu nne za mchakato wa mmea kujitengenezea chakula chake.” Swali hili linapima ngazi ya chini kabisa ya uelewa. Kinachotarajiwa hapa ni mwanafunzi kukumbuka orodha sahihi.

Swali hili hili linaweza kukuzwa kidogo kuliwezesha kupima uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa katika hali halisi: “Ikiwa mimea shambani inaonesha dalili za rangi ya majani manjano, unaweza kufanya nini kurekebisha hali hiyo na kwa nini?” Kinachotarajiwa ni pendekezo la vitendo (mfano kuongeza mbolea au kumwagilia maji) pamoja na sababu.

Hatua ya juu zaidi ya ujifunzaji, kwa mujibu wa Benjamin Bloom swali linaweza kuwa: “Buni jaribio rahisi la kujaribu aina mpya ya mbolea na utabiri matokeo yake.  Swali hili linaangukiwa katika ngazi ya juu kabisa ya ujifunzaji kwa vile linahitaji mwanafunzi abuni kitu kipya. Kinachotarajiwa hapa ni mpango wa jaribio unaonesha ubunifu.

Katika ufundishaji unaolenga kukuza mahiri, upimaji endelevu ni suala lisilo na mjadala. Hatusubiri mitihani kupima uelewa wala hatutumii mitihani kama mbadala wa shughuli za ujifunzaji. Unachohitaji ni mwalimu anayejua kutengeneza vigezo sahihi vya upimaji na kuvifuatilia. Tukifanya hivi, hatutakuwa taifa linalofikiri mitihani ndio ujifunzaji.

Mwandishi ni mhadhiri, mtafiti na mshauri elekezi wa sayansi ya ujifunzaji katika Chuo Kikuu cha Dodoma.